Siku kama ya leo, miaka mitatu iliyopita, nilipata wazo hili la kuandika makala fupi kila siku, na kuzipa jina la KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO.

Kabla ya makala hizi za kurasa, nilikuwa tayari nimejenga utaratibu wa kujiandikia kila siku, lakini zilikuwa makala ambazo ni kwa ajili ya mada maalumu. Labda biashara, fedha, uwekezaji, mafanikio na kadhalika.

Lakini nilipopata wazo hili la makala za kurasa, nilipata uhuru wa kuandika chochote ambacho naweza kuwashirikisha marafiki na wasomaji wangu. Siyo lazima kiwe kitu kikubwa sana, na wakati mwingine kinaweza kuwa kitu kidogo cha kuchukua hatua ndogo.

Tangu hapo mpaka sasa kurasa zinachanja mbuga, na zimekuwa sehemu ya wengi kupata kitu cha kuanza siku, kitu cha kuweza kufanyia maamuzi.

wp-image--1427239600

Nimeiona kwa hakika nguvu ya kufanyia kazi wazo, kwa sababu wazo hili la kuandika makala za kurasa nililipata baada ya kutumiwa ujumbe wa mwaka mpya kutoka kwa mmoja wa marafiki zangu akiniambia leo ni ukurasa mpya wa mwaka mpya. Na kuona kumbe kila siku tunayoishi inaweza kuwa ukurasa mpya wa maisha yetu.

SOMA; UKURASA WA 1000; Siku Elfu Moja (1000) Za Kuandika Kila Siku Bila Ya Kuacha Hata Siku Moja.

Tutaendelea na makala hizi za kurasa za maisha ya mafanikio, na kuichukulia kila siku kama ukurasa mpya wa sisi kuweza kuchukua hatua na kufikia mafanikio zaidi.

Wito wangu kwako rafiki yangu, chochote unachofanya kwenye maisha yako, yapo mawazo madogo madogo unayoweza kuwa unakutana nayo. Ni rahisi kuyadharau na kuona hayana madhara makubwa. Lakini mawazo hayo kama utayafanyia kazi, yanakuwa na matokeo bora sana baadaye.

Mwaka huu 2018, chagua wazo lolote dogo ambalo unaweza kulitekeleza kila siku, hata kama ni kwa dakika tano pekee, fanyia kazi kila siku na baada ya muda utaona matokeo yake kwenye maisha yako.

Inaweza kuwa kujisomea kitabu, angalau kurasa kumi kila siku, kufanya meditation angalau kwa dakika tano kila siku, au hata kupata muda wa kuandika chini yale unayoshukuru kuwa nayo kwenye maisha yako.

Unaweza kuona ni vitu vidogo na visivyo na maana kubwa kwenye maisha yako, lakini kadiri unavyofanya ndivyo utakavyoona nguvu yake.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog