Karibu kila mtu huwa ana ndoto yake kubwa ya kuibadili dunia kwenye eneo fulani.

Labda ni mwalimu ana ndoto ya kuibadili dunia kupitia maarifa anayotoa kwa wengine.

Au ni daktari anataka kuibadili dunia kwa kuboresha maisha ya wengine.

Au ni injinia anataka kuibadili dunia kwa kuja na ugunduzi wa kitofauti kabisa.

Ni rahisi kufikiria na kusema utaibadili dunia, lakini ni vigumu sana kufanya hivyo.

Naweza kusema kwamba, lengo au maono ya kuibadili dunia, ni moja ya malengo magumu sana unayoweza kujiwekea.

Kwa sababu kwanza, watu hawapendi kubadilishwa, hivyo kukazana kuwabadili, inakuwa kazi ngumu.

Pili, kazi kubwa na ambayo wengi wamekuwa wanaikwepa ni kujibadili wao wenyewe. Kila mtu anapenda mabadiliko, lakini ni wachache sana ambao wanaweza kukamilisha mabadiliko hayo.

mother Theresa

Hivyo basi rafiki yangu, kama ambavyo nimekuwa nakuambia, usikazane kuibadili dunia, bali kazana kujibadili wewe mwenyewe kwanza.

Kupitia maisha unayoishi, kupitia kazi unazofanya, kazana wewe kuwa bora kwanza, kazana kuwa na kile ambacho unataka wengine wawe nacho.

SOMA; UKURASA WA 720; Kitu Pekee Unachomiliki Na Unachoweza Kubadili Kwenye Maisha Yako…

Kwa njia hii, utawavutia wale wanaoweza kuenda na kile unachoenda nacho. Lengo linaacha kuwa gumu na linaanza kuwa la kawaida na linalotekelezeka.

Sasa wengi hufikiria ni vigumu sana kujibadili wao wenyewe, kwamba kuna kazi kubwa wanapaswa kuifanya ili kuweza kuwa wapya kabisa.

Ondokana na dhana hiyo, huhitaji kuwa mpya kwa asilimia 100 mara moja ndiyo ujibadili na kuwabadili wengine. Badala yake unahitaji kuwa bora kidogo kidogo kila siku.

Kwa mfano, kila siku unakazana kuwa bora kwa silimia 1 tu zaidi ya ulivyokuwa siku iliyopita, kwenye kila eneo la maisha yako.

Sasa ukizikusanya asilimia hizi ndogo ndogo, baada ya muda yanakuwa mabadiliko makubwa sana.

Mother Theresa aliwahi kunukuliwa akisema, kama unataka kuibadili dunia, nenda nyumbani na kaipende familia yako. Nakubaliana naye kwamba, hakuna sehemu bora ya kuanzia kuibadili dunia kama kwenye familia yako.

Na njia pekee ya kuibadili na kuiboresha familia, ni kuwa mfano wa kile ambacho unataka wengine wawe nacho.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog