Habari za leo rafiki yangu?

Ile semina yetu ya kuuanza mwaka 2018 kwa mafanikio makubwa, inayokwenda kwa jina ya MABADILIKO YA NDANI NDIYO MAFANIKIO YA KWELI imeanza leo, badala ya jumatatu kama nilivyokuwa nimeeleza awali.

Ni semina ambayo inafanyika kwenye kundi la wasap la KISIMA CHA MAARIFA. Kwa wale ambao tayari ni wanachama wa KISIMA CHA MAARIFA ila wana changamoto kwa njia ya wasap, wanaweza kufuatilia masomo haya moja kwa moja kwenye blog kupitia anwani hii; www.kisimachamaarifa.co.tz/semina2018

Kama wewe siyo mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, kwa sasa umeshaikosa semina hii, na usifungue hiyo anwani, itakutaka uingize password ambayo huna. Wewe karibu tuendelee kujifunza kupitia makala hizi na kwenye www.amkamtanzania.com

Nafasi za kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA zitakapopatikana nitakujulisha.

Karibu kwenye ujumbe wa leo, ujumbe ambao nimesukumwa sana kukushirikisha, kwa sababu naona namna ambavyo watu wengi wanafanya kosa hili, ambalo linawagharimu.

KWA NINI SIYO TAJIRI

Tuanze na mifano ili tuelewane vizuri zaidi;

Labda kuna watu unaowajua, ambao utotoni mlicheza pamoja, mkasoma pamoja, kila kitu mlikuwa mpo kwenye ngazi sawa. Na unajua kabisa ni mtu wa kawaida, hana uwezo wa tofauti sana kukushinda wewe. Lakini katika maisha kila mtu akaenda njia zake, baadaye mnakuja kukutana, unakuta yeye mwenzako amepiga hatua kuliko ulivyopiga wewe.

Unaangalia ni kipi kimempigisha yeye hatua huku wewe ukiwa umebaki nyuma?

Wakati mwingine hata hamjaachana sana, mpo sehemu moja kabisa, labda ni majirani, au mnafanya kazi pamoja. Mliajiriwa kipindi kimoja wote, na sasa miaka 5, 10, au 20 imepita, wakati wewe mishahara haikutani, mwenzako ana miradi mingi ambayo inamwingizia kipato.

Sasa katika kutafuta nini kimemwezesha mwenzako kupiga hatua kuliko wewe, ndipo ambapo wengi huanguka na kupotea. Kwa sababu hutafuta sababu zote nyingi, ambazo zote siyo sahihi.

Labda unakazana kuangalia na kugundua mwenzako alipandishwa cheo wakati wewe hujapandishwa. Hivyo kupandishwa kwake cheo ndiyo kumeleta tofauti. Au ukaona mwenzako alipewa mtaji na wazazi wake wakati wewe hakuna aliyekujali na kukupa mtaji.

Au unaweza kuona kwamba mwenzako hana utegemezi mkubwa, jukumu lake kubwa ni yeye, wakati wewe una mzigo mkubwa wa watu wanaoutegemea, kuanzia wazazi, ndugu na hata watoto.

Unaweza kuona sababu nyingi utakavyo, lakini zote hizo siyo sababu sahihi. Siyo sababu za kweli zilizopelekea mwenzako kupiga hatua wakati wewe ukiwa umeendelea kubaki pale ulipo.

Ninachotaka kukushirikisha kwenye ujumbe huu wa leo, ni sababu halisi inayowawezesha wengine kupiga hatua wakati wewe umekwama kabisa.

Sababu yenyewe ni kwamba, kuna kitu wanakijua ambacho wewe hukijui. Kama utajua kitu hicho na ukakifanyia kazi, basi na wewe utapiga hatua kama wao. Kama utajua kile ambacho waliokuzidi kwa mafanikio wanakijua, hata wewe utafanikiwa.

Ndiyo zipo sababu za mazingira, zipo sababu za uwezo, vipaji na kadhalika, lakini sehemu kubwa sana ambapo tofauti zinaanzia ni kwenye unachojua.

Sasa, kwa kuwa hatujui tofauti inaanzia kwenye kile tunachojua, huwa hatuhangaiki na kutaka kujua. Na kwa sababu mara nyingi unakuwa umeshajipa sababu ya kwa nini mwingine amekuzidi, si rahisi tena kuona kwamba kuna kitu amekuzidi.

Na hapo ukiweka na wivu, ndiyo kabisa inakuwa vigumu kuona kwamba kuna kitu wenzako wanajua lakini wewe hujui.

Kitu ambacho nataka wewe rafiki yangu uondoke nacho kwenye ujumbe wa leo ni hichi, kama yupo mtu ambaye amepiga hatua kuliko wewe, kuna kitu anajua ambacho wewe hujui.

Hivyo badala ya kutafuta sababu za uongo kwa nini watu wanakuzidi, hebu jiulize kipi wanajua ambacho wewe hujui. Na mara nyingi, njia rahisi ya kujua ni kuwauliza wao wao. Wanajua wanachojua na wapo tayari kuwashirikisha wengine, ila kwa bahati mbaya, hakuna anayeuliza.

Rafiki yangu, uliza na jiulize kwa kila hatua ambayo unaona wengine wanapiga lakini wewe hujapiga. Je ni kipi wanajua wao, ambacho wewe hujui na hivyo kinakukwamisha?

Kuwa tayari kujifunza kupitia kwa wale waliokutangulia, kuna vingi wanavyo ambavyo unaweza kujifunza makubwa kupitia wao.

Kama kuna kitu ambacho kinakuzuia kupiga hatua, basi ni vitu ambavyo huvijui, wakati wengine wanavijua.

Mwisho kabisa, huwezi kujua kila kitu, ndiyo maana maisha yako yote ni ya kujifunza, kujifunza kupitia masomo mbalimbali, uzoefu wako mwenyewe na hata uzoefu wa wengine.

Usikubali usichojua kiwe kikwazo kwako kufanikiwa. Na usiwe na ubaguzi kwamba unaweza kujifunza kwa nani na huwezi kujifunza kwa nani.

Muhimu zaidi, unapoona mwenzako amepiga hatua kuliko wewe, usimwonee wivu, badala yake mpende, mwombee apige hatua zaidi, kwa sababu kwa kuweza yeye ni kiashiria kwamba inawezekana na hamasa kwako kuchukua hatua zaidi.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog