Kila mtu huwa anapata hasira, lakini kinachowatofautisha wale wanaoonekana wana hasira sana na ambao hawana hasira, ni namna gani wanaichukulia na kuishughulikia hasira wanayokuwa nayo.

Watu kwa kujua au kutokujua, huwa wanatuudhi au kufanya mambo ambayo hatukutegemea wafanye. Hili huleta hasira kwa kila mtu, lakini wapo ambao hasira zao zinaishia hapo na wapo ambao huendeleza hasira hizo. Wapo wanaojiapiza kabisa kwamba hawatasamehe kabisa katika hali fulani.

Zawadi Kubwa

Kipo kitu ambacho kinachochea hasira kwa wale ambao ni watu wa hasira muda wote. Kitu hichi ndiyo kinawafanya waendelee kuwa na hasira, ambayo inaishia kuwaumiza badala ya kuwasaidia.

Kinachochochea hasira kwa wengi ni ile hadithi ambayo watu wanatengeneza kwenye mawazo yao juu ya kile kilichowaletea hasira. Baada ya tukio linalosababisha hasira kutokea, watu hubaki na hadithi kwenye akili zao.

Kwa nini alifanya vile? Amenidharau sana, hanithamini, alifanya makusudi na hadithi nyingine za aina hii. Ni hadithi hizi ambazo watu wanabaki nazo ndiyo zinaendelea kuchochea hasira.

SOMA; UKURASA WA 936; Tatizo Ni Kutafuta Furaha Sehemu Ambapo Haiwezi Kupatikana…

Lile tukio lililosababisha hasira linakuwa limeshapita, lakini ile hadithi inaendelea kuzunguka kwenye akili, na inaendelea kukumbusha kwamba kilichotokea ni cha kukasirisha.

Kama utaweza kuondokana na hadithi unazojijengea baada ya tukio lolote lile utakuwa huru. Na hata kama mtu atakuwa amekukasirisha kiasi gani, utaelewa amekukasirisha, lakini hutakuwa na sababu ya kuendelea kuumia kwa tukio ambalo tayari limepita.

Tatizo la hasira ni kwamba, kama mtu amekuudhi na wewe ukakasirika, wewe ndiye unayeendelea kuumia na hasira wakati aliyekukasirisha akiwa anaendelea kula maisha kwa raha zake.

Usijifanyie hili la kujiumiza, acha kulinda hadithi za hasira kwenye akili yako, ziachilie na uwe huru.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog