Kila mtu huwa anakuwa na ndoto fulani. Tena ndoto ambazo ni kubwa na za ajabu na wengi huwa hawazisemi wazi wazi kwa sababu wanaogopa wengine watawacheka au kuwakatisha tamaa.

Ungekuwa na uwezo wa kusoma ndoto za watu ndani ya akili zao, ungeona jinsi ambavyo dunia imejaa utajiri wa kutisha. Ungeona namna ambavyo dunia ina watu wanaofanya makubwa sana.

Lakini cha kusikitisha sana ni kwamba, ndoto hizi kubwa za wengi, huwa hatuzioni. Tunaishia kuwaona watu wengi wakiwa na maisha ya kawaida, ambayo hayana kikubwa cha kushangaza.

Lakini pia wapo watu wachache sana ambao wanafanyia kazi ndoto zao na wanaleta mapinduzi makubwa sana duniani. Hawa ndiyo washindi ambao tukiwaangalia tunajiuliza wanawezaje kufanya hayo makubwa ambayo wanaweza kuyafanya.

Kwa kuangalia washindi wanaofanyia kazi ndoto zao, na wale wanaoshindwa kuzifanyia kazi, tunaona tofauti moja kubwa sana.

Wale wanaoshindwa, wale ambao hatuoni ndoto zao kubwa, huwa wanaishia kuota na kuendelea kuota zaidi na zaidi. Kila siku wana kitu cha kuongeza kwenye ndoto zao, lakini cha kushangaza hakuna hatua wanayochukua. Wanaweza kuruhusu ndoto zao kukua wawezavyo, ila wao wenyewe wakabaki vile walivyo.

SOMA; UKURASA WA 266; Je Ni Hofu Au Ndoto?

Kwa upande wa pili, wale wanaoshinda, wale wanaofanyia kazi ndoto zao, wamekuwa wanatengeneza mfumo wa kuwawezesha kuchukua hatua na kufikia ndoto zao. Siyo lazima waweze kutekeleza kila kitu, na siyo lazima wafanye makubwa sana, ila wanakuwa na mfumo ambao unawafanya wachukue hatua badala tu ya kuishia kuota.

Kwa kuwa na mfumo mzuri, wanakuwa na hatua za kuchukua ambazo zinawawezesha kusonga mbele zaidi.

Hivyo rafiki yangu, kama unataka ndoto zako ziwe uhalisia, tengeneza mfumo unaokuwezesha kuchukua hatua na kuzifikia. Usiishie tu kuota na kujifurahisha, bali chukua hatua ili kuweza kuishi uhalisia wa ndoto hizo.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog