Nimekuwa nasisitiza sana kuhusu usomaji wa vitabu. Nimekuwa nawaambia watu wasome vitabu sana. kwa kifupi natamani TV, redio na hata mitandao yote ingefutwa na watu wapewe vitabu wasome. Nina amini kitabu ni hazina kubwa sana, ambayo mtu akiweza kuitumia hatabaki pale alipo sasa.

Nasema haya kwa sababu nimeona manufaa ya usomaji wa vitabu kwenye maisha yangu binafsi, nimeona namna vitu ambavyo nimejifunza kwa kusoma vitabu, na kuvitumia kwenye maisha yangu, kumenifanya kua bora zaidi ya ambavyo nilikuwa kabla.

Kwa miaka mitano iliyopita, nikijumlisha vitabu nilivyosoma na kusikiliza, ni zaidi ya vitabu 500 sasa. Ndiyo vitabu 500. Siku za nyuma nilikuwa naandaa orodha ya vitabu nilivyosoma kila mwaka na kuwashirikisha marafiki zangu, lakini kwa sasa nasoma vitabu vingi kiasi kwamba itanichukua muda sana kuanza kuandaa orodha ya mwaka.

Sasa pamoja na umuhimu huu wa kusoma vitabu, bado wapo watu wenye changamoto kuhusu usomaji wa vitabu. Nimekuwa nasikia changamoto nyingi kutoka kwa wengi lakini kubwa tatu ni hizi; lugha ambayo ni ngumu kwa mtu kuelewa, kukosa fedha za kununua vitabu na kukosa muda wa kusoma vitabu.

Vitabu

Sasa kwa kuwa mimi wakati naanza usomaji wa vitabu changamoto hizi nilikuwa nazo pia, niliweza kuzivuka mpaka kufikia hatua ya kusoma vitabu vyote hivyo. Na hivyo kwenye makala ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO, ninakwenda kukushirikisha jinsi unavyoweza kupata vitabu vizuri vya kusoma, kwa lugha unayoielewa na kwa gharama nafuu au bure kabisa.

Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu changamoto hii;

Changamoto yangu ni vitabu vya kusoma vya lugha ya Kiswahili naona waandishi ni wachache pia fedha ya kupata vitabu na namna pia ya kupata hivyo vitabu. – ORMERICKI M. S.

Kama ambavyo msomaji mwenzetu ametuandikia, wapo wengi ambao wanakutana na changamoto kama hiyo na wanaishia kutokusoma vitabu, kitu ambacho siyo kizuri kwao.

Zifuatazo ni njia ambazo unaweza kutumia kuondokana na changamoto hizi zinazokuzuia kusoma vitabu.

Changamoto ya lugha.

Ni kweli kwamba vitabu vingi vipo kwa lugha ya Kiingereza, na hii ni kwa sababu ya utamaduni wa wenzetu kusoma vitabu.

Lakini pia vipo vitabu vingi vizuri ambavyo vimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili. Vitabu hivi vinapatikana kwenye maduka mbalimbali ya vitabu, kwa wauzaji wa vitabu kwenye maeneo kama vituo vya magari na pia kwenye maktaba mbalimbali.

Hivyo kama unahitaji vitabu vya Kiswahili kwa ajili ya kujisomea, unaweza kuvitafuta kwenye maeneo hayo na ukaweza kuvipata na kuongeza maarifa yako.

Popote ulipo, tafuta maeneo yanayohusika na vitabu na utaweza kupata vitabu vizuri vya kujisomea.

Pia ili kuweza kupata wigo mpana wa kusoma vitabu vingi zaidi, jifunze lugha ya Kiingereza, hasa kwa upande wa kusoma. Wenzetu wana idadi kubwa ya vitabu na vinavyoeleza kila eneo la maisha, ukivipata na kuvisoma utaweza kupiga hatua kubwa.

Usomaji

Changamoto ya kukosa fedha za kununua vitabu.

Vitabu karibu vyote vinauzwa, lakini gharama zake siyo kubwa. Vitabu vingi gharama zake ni kuanzia shilingi elfu 5 mpaka shilingi elfu kumi. Vipo vitabu vya gharama zaidi ya hapo, lakini kwa kuanza na vya bei hizo yapo mengi ambayo utajifunza.

Hivyo kama utakuwa na utaratibu wa kununua na kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi, bado gharama siyo kubwa sana. Kutenga shilingi elfu 10 kila mwezi kwa ajili ya kujiongezea maarifa ni kitu ambacho kila mtu anaweza kufanya. Ila tatizo ni kwamba wengi hawana vipaumbele kwenye ununuzi wa vitabu. Ndiyo maana watu wanapata fedha za kula, kununua nguo na hata kunywa, lakini hawana fedha za kununua vitabu.

Kama unaweza kula kila siku, basi unaweza kununua vitabu, kama umekua unanunua nguo, basi unaweza kununua vitabu. Swala ni kuweka vipaumbele vyako vizuri ili uweze kufanya lililo sahihi.

Nimekuwa nasema usikubali kununua nguo kabla hujanunua vitabu, kwa sababu unaweza kuvalisha mwili wa nje, huku akili yako ikiwa na njaa, na ulichofanya kikawa hakina maana yoyote.

Kama huna fedha kabisa ya kuweza kununua kitabu, kitu ambacho hakiwezekani kama unasoma hapa, lakini tukubaliane na wewe kwa muda, soma vitabu vya bure. Popote unapoishi, nenda kwenye maktaba ya karibu, jiandikishe na kuwa mwanachama ambapo unalipa gharama ndogo kwa mwaka na unapata nafasi ya kuingia na kujisomea vitabu vingi sana bila ya kuvinunua.

Maktaba zina vitabu vingi, ambavyo kwa kuvisoma utaondoka na mengi ya kuweza kufanyia kazi.

Pia unaweza kusoma vitabu vinavyopatikana bure, kama vitabu vya dini. Kama wewe ni Mkristo unaweza kujisomea Biblia na ukajifunza mambo mengi sana ya kufanyia kazi. Kwa Mwislamu unaweza kusoma Kuran na ukajifunza mengi mno.

Muhimu sana ni wewe upate kitu cha kusoma, ujijengee tabia ya kusoma na ufanyie kazi yale unayojifunza kupitia kusoma ili maisha yako yawe bora sana.

Changamoto ya muda.

Watu wengi wamekuwa wanasema hawana muda wa kusoma vitabu kwa sababu ratiba zao zinawabana sana. Kazi ni nyingi na zinawachosha sana na hivyo hawawezi kupata muda wa kusoma vitabu.

Na hili pia ni kujidanganya, kama mtu anaweza kupata muda wa kula kila siku, anaweza kupata muda wa kusoma vitabu. Kama mtu anaweza kupata muda wa kulala kila siku, ana muda wa kutosha kusoma vitabu.

Anachohitaji mtu ni kusoma kwa hatua, usikazane kusoma kitabu kizima kwa siku moja, wala kukazana kumaliza haraka. Wewe kama muda ni changamoto kwako, basi gawa na usome kitabu kwenye mafungu.

Njia bora ya kusoma vitabu kwa wasio na muda ni kusoma kurasa 10 kila siku. Kurasa kumi tu ambazo kila mtu anaweza kufanya. Unapoamka unasoma kurasa 4, kitu ambacho kitakuchukua dakika 10. Mchana tena unasoma kurasa 3 na kabla hujalala unasoma kurasa nyingine tatu.

Ukijijengea nidhamu ya kusoma kurasa kumi kila siku, kila mwezi utakamilisha kusoma kitabu kimoja, hili litakuwezesha kupiga hatua zaidi.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Kama ungependa kujiunga kwenye kundi la wasap la kusoma kurasa kumi kila siku, fungua www.amkamtanzania.com/kurasa

rafiki, hivi ndivyo unavyoweza kuondokana na changamoto zote zinazokuzuia kusoma vitabu. Haya niliyokushirikisha hapa ni mambo yanayoweza kutekelezeka na yeyote anayejali maisha yake na anayetaka kupiga hatua. Ni imani yangu kwamba umejifunza na utachukua hatua.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog