‘Where a man can live, he can also live well’ – Marcus Aurelius
Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa nafasi hii nyingine nzuri sana kwetu, nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA, ni maneno matatu ambayo yanatuongoza kwenye kufanya makubwa kwetu na kwa wanaotuzunguka.
Asubuhi ya leo tutafakari KAMA UNAWEZA KUISHI…
Kama unaweza kuishi, basi unaweza kuishi vizuri, unaweza kuishi kwa furaha na unaweza kuishi kwa maelewano na wengine.
Hivi ni vitu ambavyo haijalishi una mali kiasi gani au una uwezo mkubwa kiasi gani.
Kuwa hai ni kigezo tosha cha kukuwezesha kuwa na maisha mazuri, kama utajua namna ya kuwa na maisha hayo.
Haihitaji elimu wala uwezo mkubwa kuwatendea wengine wema, kusema asante na kuwasaidia wengine kutatua matatizo yao.
Kitendo tu cha wewe kuweza kupumua sasa ni kitendo kikubwa unachopaswa kushukuru na kufurahia pia.
Hivyo kama unajiambia huna maisha mazuri sasa kwa sababu kuna kitu umekosa, au unafikiri ukishakuwa na vitu fulani ndiyo utaweza kuwa na maisha mazuri, unajidanganya.
Kama hapo ulipo sasa huna maisha mazuri kwako, hakuna lolote litakalokuletea maisha mazuri.
Kwa sababu maisha mazuri huwa yanaanzia ndani ya mtu na siyo nje, yanategemea mtu mwenyewe ma siyo chochote anachomiliki.
Kwa kuwa unaishi, basi ishi vizuri,
Fanya tendo la wema kwa mtu leo,
Shukuru kwa kila ulichonacho kwenye maisha yako,
Na tumia vizuri na kuthamini kila ulichonacho kwenye maisha yako.
Kama unaweza kuishi, basi unaweza kuishi vizuri, bila ya kujali upo kwenye hali gani kwa sasa.
Ukawe na siku njema leo, ya kuishi vizuri kwa sababu unaweza.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha