A man who suffers before it is necessary, suffers more than is necessary. – Lucius Annaeus Seneca

Habari za asubuhi ya leo mwanamafanikio?
Hongera kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo, siku bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudinkubwa ili kuweza kupata matokeo bora kabisa.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwaka huu 2018 tunaongozwa na TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo tunatatua matatizo magumu, kufanya maamuzi muhimu na kuwapa watu sababu ya kutufuata.

Asubuhi ya leo tutafakari USIJITESE KABLA YA MUDA…
Mtu mmoja amewahi kusema kwamba, watu jasiri hufa mara moja, lakini waoga hufa mara elfu.
Watu wengi wamekuwa wakijitesa na kuteseka kabla ya muda.
Na hili linachochewa zaidi na hofu ambazo wengi huwa wanakuwa nazo.

Mtu anakuwa na hofu kwa kitu ambacho bado haya hakijatokea, hofu inakusumbua na kukutesa, halafu kitu hicho wala hata hakitokei kama ambavyo mtu alifikiri kitatokea.

Rafiki, usikubali kabisa hofu ikutese, kwa chochote unachofikiria na kuhofia, jiambie kwamba wakati ukifika utapata jawabu. Au jambo likishatokea utakuwa na njia ya kulitatua.
Usijitese kwa kabla ya muda, kwa mambo ambayo kwa nafasi kubwa wala hayatatokea kama unavyofikiri yatatokea.

Ishi kwa wakati uliopo, ishi leo kwa kuweka juhudi kwenye kile ulichopanga kufanya leo.
Na kama kuna chochote kuhusu kesho kinakusumbua leo, jiambie hiyo ni kesho, hivyo utasumbuka nacho ikifika kesho. Ila kwa sasa, kazana na kile unachoweza kufanya, kile ulichonacho sasa.

Usijitese kwa mambo yajayo, subiri yatafika na mara nyinyi hayatakuwa kama ulivyofikiri.
Pia usijitese kwa mambo yaliyopita, hakuna unachoweza kubadili.
Ishi sasa, ishi kwa wakati uliopo na hutakuwa na sababu ya kujitesa.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha