Tangu enzi na enzi, binadamu tumekuwa viumbe ambao maisha yetu tunayaendesha kwa juhudi zetu wenyewe. Tangu enzi za uokotaji na uwindaji, mpaka enzi za kilimo, kila mtu aliishi kulingana na juhudi ambazo alikuwa anaweka.

Aliyeweza kuamka asubuhi na kuwahi kuwinda alipata chakula cha kutosha na maisha yake na familia yake yalikwenda vizuri. Aliyekuwa mvivu alikosa chakula na maisha yake kuwa magumu.

Miaka 200 iliyopita, yalitokea mapinduzi ya viwanda, na hapa mambo yalibadilika kwa kasi sana. Kwanza viwanda viliweza kuzalisha kwa kiasi kikubwa kuliko mtu mmoja mmoja. Na pili, viwanda vilihitaji watu wa kufanya kazi, watu ambao wataendelea kufanya kazi siku zote.

Kwa hali ilivyokuwa kipindi hicho, ilikuwa ni vigumu kuwapata watu wa kufanya kazi za viwanda, ambazo zilikuwa nyingi na zenye uhitaji mkubwa wa watu. Hivyo wenye viwanda walitafuta njia ya kuhakikisha wanapata watu wa kuweza kufanya kazi hizo. Na hapa ndipo wazo la ajira lilipoanza.

Hapa ndipo watu walipoanza kuajiriwa na kulipwa kwa siku, wiki au mwezi, huku wakiahidiwa kwamba iwapo watafanya kazi zao vizuri, basi watakapofikia mwisho wa kazi zao, yaani wamezeeka na hawawezi tena kufanya kazi, watalipwa mafao kwa kazi walizofanya.

Hapa ndipo watu walipoanza kuajiriwa na ndipo ajira zilipoanza kuonekana kitu muhimu kuwa nacho.

Kama hiyo haikutosha, palikuwa na ngazi kwenye ajira kulingana na kiwango cha elimu ambacho mtu anacho. Kwa wenye elimu kubwa kulipwa kiasi kikubwa na kufanya kazi ambazo siyo ngumu. Na hapa ndipo mchezo ulipotengenezwa kwamba ukisoma kwa bidii, ukafaulu vizuri, utapata kazi nzuri na inayolipa.

Mmoja wa wamiliki wa viwanda, Bwana Henry Ford alifanya jambo moja ambalo liliwashangaza wenzake. Alichofanya kwa kipindi hicho, ni kupunguza muda wa kufanya kazi na kuongeza mshahara. Kabla ya Ford kufanya hili, watu walikuwa wakifanya kazi muda mrefu kwa siku, zaidi ya masaa 10 na siku sita za wiki.

Wenzake walipomuuliza Ford kwa nini amefanya hivyo? Kwa nini apunguze muda wa kufanya kazi, kuwa masaa nane kwa siku na siku za kufanya kazi kuwa tano huku siku mbili kuwa za kupumzika? Na kwa nini aongeze malipo?

Ford aliwajibu kwa kuwaambia, ili hawa watu wawe wafanyakazi wa kudumu, lazima tuwape muda wa kutumia fedha tunazowalipa. Hivyo kuwapa kipato kizuri na muda mrefu nje ya kazi, watatumia zaidi na kuhitaji kazi zaidi. Sasa fikiria mtu unalipwa ijumaa, halafu jumamosi na jumapili huna kazi, ukiamka jumatatu utakuwa na fedha kweli? Lazima uende tena kazini ili kupata fedha ya kutumia.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

Na hapa ndipo utegemezi wa ajira ulipoanza rasmi, watu kuanza kuwa tegemezi kwenye ajira, kutumia fedha ambazo hawana wakiamini watalipa wakilipwa kwenye ajira zao.

Lakini sasa mambo yamebadilika, zile ajira za uhakika hakuna tena, na sayansi na teknolojia inakuja na njia za kuwapunguza watu kwenye kazi. Hivyo sasa tunarudi kule ambako tulitokea, kule kwa kula kulingana na ulichowinda, au ulicholima na kadhalika.

Na hii ndiyo sababu kubwa nimekuwa nashauri sana kila mmoja wetu awe na biashara. Hata kama ni biashara ndogo, lakini kuwa na biashara kunaleta tofauti kubwa sana kwenye maisha ya mtu.

Na hata kama upo kwenye ajira, ambayo unajiambia imekubana na huna muda wa kufanya mambo mengine, wewe ndiye unahitaji zaidi kuwa na biashara ili kuweza kutengeneza uhuru kwenye maisha yako.

Ujumbe wangu mkuu kwako rafiki yangu, mwaka huu 2018 hakikisha unakuwa na biashara. Kama hujaanza biashara basi anza, na kama ulishaanza basi kuza zaidi biashara yako.

Zipo sababu nyingi mno kwa nini kila mtu anapaswa kuwa na biashara, lakini hapa nimekuandalia zile kumi muhimu, ambazo kila wakati unapaswa kuzifikiria.

 1. Uhuru wa kifedha na utajiri.

Kuna watu wakisikia neno utajiri wanajisikia vibaya, watajisifia kabisa kwamba mimi sitaki utajiri, nataka maisha mazuri. Sasa sijui mtu unawezaje kuwa na maisha mazuri kama huna uhakika wa hela ya kula miezi mitatu ijayo. Kama kipato chako ni kidogo kuliko matumizi yako, maisha mazuri unayapataje?

Hivyo tuachane na hilo la kama utajiri ni mzuri au la, utajiri ni muhimu. Na kamwe hutakuwa tajiri kupitia ajira. Unaweza kuwa na fedha nyingi, unaweza kuwa na mali nyingi, lakini hutafikia utajiri na uhuru wa kifedha kupitia ajira. Haiwezekani, kabisa. Hii ni kwa sababu ajira ina ukomo wa muda wa kufanya na ukomo wa kiasi unacholipwa.

Njia ya uhakika ya kufikia uhuru wa kifedha, ni kuwa na biashara, kuiendesha vizuri na ikazalisha faida. Njia nyingine bora ni kuwekeza maeneo ambayo yanazalisha.

 1. Usalama wa kazi na kipato.

Siku za nyuma watu waliambiwa ukitaka kuwa na usalama wa kazi na kipato basi ajiriwa, tena ukiajiriwa serikalini basi ajira yako ni ya kudumu. Nina imani upo macho na unaona namna ajira zimekuwa ngumu kwa wengi, watu wakifukuzwa na kipato kikiwa kidogo na ambacho hakiongezeki.

Usalama pekee wa kazi na kipato unaoweza kuupata kwa zama hizi ni kuwa na biashara yako mwenyewe, ambayo unaweza kuweka juhudi kubwa na kupata matokeo bora kabisa. Ambapo unaweza kuongeza kipato chako kwa kuongeza juhudi zako.

Kazi nyingi huwa ni za kujirudia rudia, hazina changamoto, ni za kawaida na zinaua ubunifu na uwezo wa watu wa kufikiri. Kufanya kitu kile kile kwa miaka 20, kunamfanya mtu ashindwe hata kufikiri njia tofauti za kufanya mambo.

Kama unataka kujifunza kuhusu maisha, kuhusu tabia za watu, kuhusu uongozi, kuhusu ushawishi, kuhusu masoko na mauzo, basi ingia kwenye biashara. Biashara itakulazimisha ujifunze, kwa sababu kila siku utakutana na vitu ambavyo huvijui.

Na hapa sikuambii ujifunze biashara, nakuambia ingia kwenye biashara, na utalazimika kujifunza mambo mengi.

Changamoto utakazokutana nazo kwenye biashara zitakusukuma ujifunze mambo mengi zaidi.

 1. Kufanya unachopenda.

Hakuna watu wenye maisha magumu, kama wale ambao wanafanya kazi ambayo hawaipendi, ila hawana namna kwa sababu wanahitaji fedha za kuendesha maisha yao. Hawa ndiyo watu hata ukifuatilia maisha yao binafsi, unakuta ni magumu na yamejaa changamoto. Utakuta hawaelewani na wengine, mahusiano yao yana changamoto na maisha ni magumu.

Kama unataka kuwa na maisha bora, kwanza kabisa lazima upende kile unachofanya. kwa sababu kinachukua sehemu kubwa ya maisha yako, na hivyo kinaathiri maisha yako moja kwa moja.

Unaweza kuwa unapenda ajira uliyonayo, lakini majukumu unayopewa ukawa huyapendi kabisa. Au namna mambo yanavyoendeshwa ikawa haikufurahishi.

Dawa ni moja, kuwa na biashara, ambayo inaendana na kile unachopenda kufanya, na hutafanya tena kazi kwenye maisha yako, bali utafanya unachopenda.

 1. Kufanya kazi na watu unaowapenda, unaowachagua.

Umewahi kusikia kwamba wewe ni matokeo ya watu watano wanaokuzunguka? Kabla hujaingia kwenye ajira unaweza kuwa unawashangaa kweli watu ambao wapo kwenye ajira, unaweza kuona kama hawana akili hivi. Lakini unapoingia na kukaa kwa muda, unakuwa kama wao. Unajikuta unafikiri na kufanya kama wao.

Siyo kwamba wamekuloga, bali ushawishi wa wale wanaotuzunguka huwa ni mkubwa.

Sasa kuna upande wa pili, upande wa kufanya kazi na watu ambao huwapendi. Siyo huwapendi kwa sababu mbaya, bali tu siyo watu ambao unajisikia vizuri kukaa karibu nao, labda kutokana na tabia zao au mitazamo yao. Lakini ukiwa kwenye ajira utakuwa huna namna, mtapangwa mfanye kazi pamoja na huna budi bali kufanya kazi.

Ukiwa na biashara yako mwenyewe, unachagua nani wa kufanya naye kazi, ambaye unapenda kufanya naye kazi. Na kama mtu hujisikii vizuri kufanya naye kazi, unaacha kufanya naye kazi.

 1. Kuwasaidia wengine.

Unapoanzisha biashara, unatatua matatizo mengi kwa wakati mmoja.

Kwanza unawasaidia watu kwa kuwapa bidhaa na huduma wanazohitaji, hivyo unayafanya maisha yao kuwa bora zaidi.

Pili unatoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa wengine. Kadiri biashara inavyokua, ndivyo unavyogusa maisha ya wengi zaidi.

Hivyo niseme tu rafiki yangu, kama unataka kuwa mzalendo wa kweli, anzisha biashara.

 1. Kuwa bosi wako mwenyewe na kuacha kutumwa kama mtoto mdogo.

Kwenye ajira kuna mambo sana, unaweza ukawa unajua kitu sahihi cha kufanya, na unajua namna ya kukifanya, lakini aliyepo juu yako akakuambia ufanye kwa namna nyingine ambayo unajua siyo sahihi. Na kwa sababu yeye ni bosi, huna namna, inakubidi ufanye.

Wakati mwingine unaweza kugombezwa kama mtoto mdogo, wakati wewe ni mtu mzima na una watu wanaokuheshimu na kukusikiliza nje ya ajira.

Hili unaweza kulivumilia kwa muda, lakini usikubali yawe ndiyo maisha yako yote, kwa sababu ukizoea hayo, unakosa hata kujiamini.

Anza biashara yako mwenyewe na uwe bosi wako mwenyewe. Na utaweza kufanya yale ambayo unajua ni sahihi, huku kukiwa hakuna wa kukugombeza. Soko litakufundisha nidhamu na adabu, lakini hakuna wa kukufanya uone maisha yako ni tegemezi kwa mtu mwingine.

Usomaji

 1. Jitihada zinazolipa.

Kwenye ajira, mkishakubaliana mshahara, basi utaendelea kulipwa huo kwa muda kabla haujabadilishwa. Hii ina maana kwamba hata kama utaweka jitihada kubwa sana, na wenzako wakaweka jitihada za kawaida, mwisho wa siku wote mtalipwa sawa. Sasa binadamu wengi huwa tunajifunza kwamba, kama nikiweka juhudi nalipwa sawa na wengine wasioweka juhudi, hakuna haja ya kuweka juhudi, wacha nifanye kama wengine, na hapo ndipo wengi wanapopotea.

Ukiwa kwenye biashara yako, ukiongeza juhudi, na kipato kinaongezeka. Yaani unaona matokeo yake haraka na moja kwa moja kuliko kwenye ajira. Kama unataka kulipwa kulingana na juhudi zako, ingia kwenye biashara.

 1. Rasilimali na fursa ni nyingi.

Zamani watu walishindwa kuingia kwenye biashara kutokana na uhaba wa fursa, na uchache wa rasilimali. Kwa mfano ili uanzishe biashara ilibidi uwe na mtaji mkubwa, uwe eneo ambalo wengi wanaona na kuweza kutangaza kwa gharama kubwa kwenye vyombo vya habari.

Lakini sasa hivi, unaweza kuanza biashara bila hata ya kuwa na fedha kabisa. Unaweza kuwa na biashara bila hata ya kuwa na eneo la biashara. Unaweza kuwa na bidhaa au huduma zako, unazosambaza moja kwa moja kwa watu na kutangaza kupitia mitandao ya kijamii.

Hii ni fursa ya kipekee sana kwako kuweza kuanza na kukuza biashara yako kwa uwepo wa rasilimali hizi.

 1. Kuacha kufanya vitu ambavyo hupendi kufanya.

Kwenye ajira, huna nguvu kubwa ya kuchagua majukumu yapi unataka kufanya hata kama ndiyo majukumu muhimu. Mara nyingi utafanya kile ulichopangiwa kufanya, hata kama hakiendani na uwezo mkubwa uliopo ndani yako.

Lakini ukiwa na biashara yako mwenyewe, una uwezo wa kuweka vipaumbele, kuchagua majukumu ambayo unapaswa kuyafanya wewe, na yale mengine unawapa wengine wafanye.

Kwa kifupi kwenye biashara, kama kuna kitu hutaki kufanya, hukifanyi, badala yake unatafuta wengine wakufanyie. Na wewe unaweka muda na nguvu zako kwenye yale ambayo ni muhimu zaidi.

Hizi ndiyo sababu 10 kwa nini unapaswa kuwa na biashara kwa mwaka huu 2018. Bado tupo mwanzoni mwa mwaka, na hivyo bado una nafasi ya kuweza kuanza na kukuza biashara yako.

Chukua hatua sasa ya kuanza biashara, au kukuza biashara yako kama ulishaanza.

Rasilimali nilizokuandalia za kuanza biashara 2018.

Hapa kuna rasilimali nimekuandalia za wewe kuanza biashara 2018.

 1. Kitabu; BIASHARA NDANI YA AJIRA, ni kitabu kitakachokuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako hata kama ajira imekubana. Kinapatikana kwa hardcopy na softcopy. Kukipata tuma ujumbe kwenye wasap namba 0717396253.
 2. Kundi la KISIMA CHA MAARIFA, hii ni sehemu sahihi ya wewe kujifunza kila siku na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua zaidi. Kuweza kujiunga tuma ujumbe kwa wasap namba 0717396253 wenye neno KISIMA CHA MAARIFA.
 3. Programu ya PERSONAL COACHING ambapo mimi nakuwa kocha wako moja kwa moja kwa kipindi cha mwezi mzima. Unaweza kupata maelezo zaidi hapa kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog