Ili kuwa na mafanikio unahitajika kuwa na mawazo mazuri na mipango bora ambayo itakufikisha huko. Lakini, ili kuwa tajiri unahitaji kuwa na kitu cha ziada, mbali tu ya mipango na mawazo hayo uliyonayo. Kitu hiki si kingine bali ni kufikiri kitajiri.

Ni rahisi sana kuwa na mipango  mizuri na mawazo mazuri ya kukufanikisha, ikiwa lakini utakosa kufikiri kitajiri yaani ukakosa ile tunaita ‘rich mind set’ swala la kufikia utajiri mkubwa kwako litakuwa ni gumu sana.

Mipango na mawazo yako sio kila kitu kwenye kutafuta utajiri. Wangapi wana mipango na mawazo mazuri, unafikiri kwa nini hawawi matajiri? Hiyo ni kwa sababu ya hiki ninachokiongelea hapa watu hao  hawafikirii kitajiri.

Pengine unawaza ‘duuu,’ mbona leo Imani unanichanganya, sikuchanganyi ila ndio ninakwambia ukweli halisi ambao unatakiwa uelewe na kufanyia kazi. Na ikiwa hautafanya hivyo basi kufanikiwa kwako na kuwa tajiri haitawezekana.

Pasipo ya kwenda mbali sana, naomba nikwambie tu kama unafikiri kwa namna hii hapa huwezi kuwa tajiri;-

b95b4-mind-power1

“Mafanikio nitayapata kwa urahisi.”

Imekuwa ni kama kawaida ikiwa utawafata washauri wa mafanikio wa kwenye ‘facebook au marketing’ wengi wao ni rahisi sana kukwambia kwamba unaweza ukatengeneza kiasi kikubwa sana cha pesa huku ukiwa umelala au kwa muda kidogo wa ziada.

Sina shaka na hilo, ushauri huu najua umeusikia sana na inawezekana unaufanyia kazi na kuamini kabisa. Lakini kabla sijaenda mbali naomba tu ni kwambie kitu hichohicho umekuwa ukiambiwa sio kweli umedanganya na umejidanya pia kwa kuamini kwako.

Kama ikiwa mtu ataweza kuuza njia ya mafanikio yake na kuinadi kwamba ni rahisi basi ingekuwa haina haja ya kusema hadharani, angefanya mwenyewe. Wewe fikiria akwambie wewe ni nani na kwa upendo upi kwamba mafanikio yapo rahisi kihivyo.

Kila mtu mwenye mafanikio anajua ili ufanikiwe, inahitaji jitahida za nguvu na si lelemama. Sasa inapotokea mtu akakwambia mafanikio ni rahisi na akaacha kukwambia kwanza kazi inahitajika hata kama pesa utakuwa unatengeneza umelala, mtu huyu ni rahisi kuweza kukupoteza kutokana na mawazo yake hayo.

Mafanikio unatakiwa kujua hayaji kirahisi, kuna kuweka juhudi nyingi, kuna kushindwa kwingi na kuvumilia kila aina ya adha lakini si kitu cha mara moja tu na kufanikiwa. Kama unafikiri hizo zibadilishe haraka, vinginevyo utakuwa umeshindwa mwenyewe kabisa.

Soma; Usiruhusu Maamuzi Haya, Yakuharibie Maisha yako yote.

“Nitafanya kwa maarifa zaidi, lakini si kwa juhudi kubwa”

Pia katika dunia hii ya mwendo kasi najua umesikia sana hadithi za fanya kazi kwa akili tu na maarifa na utafanikiwa hata kama usipoweka juhudi kwa nguvu sana, haya ni maneno ambayo yamekuwa yakisemwa sana.

Kuna wakati huwa nafikiri wenye mawazo hayo na kuanza kuyajadili na ambao wanatafuta hiyo ‘work smart not work hard’ hawa wanawaza nini. Inafika mahali ninakuwa naamini pengine watu hawa wanaota ndoto za mchana kweupe.

Kuna wakati unapaswa kujua kutafuta mafanikio kwa maarifa tu peke yake na kusahau kufanya kazi huo ni uvivu, tena mkubwa. Hiyo tukiwa na maana kwamba hatukatai maarifa ni muhimu lakini kazi ni lazima kazi iwekwe ili kutoa matokeo yanayoeleweka.

Ni wazi tu kusema kwamba kama umekuwa kila siku ukijidanganya kwamba mimi natumia akili na sitaki kufanya kazi sana, unajidanganya na tayari utakuwa umeshaingia kwenye kundi la kuanza kurudi nyuma kimafanikio.

Kubali kutumia maarifa kweli kwenye kazi zako, lakini hata hivyo usisahau kuchapa kazi. Kazi unatakiwa kuifanya haswa na hakuna mbadala wake, zaidi ya wewe kujituma na kufanya kazi kwa nguvu zote na kwa jinsi unavyojua.

Soma; Sababu Kumi Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Biashara Mwaka Huu 2018.

“Kila kitu kinanihusu mimi”

Itakuwa ni ndoto za mchana za kutaka mafanikio makubwa, lakini wakati huohuo wewe ukang’ang’ana na kila kitu kutaka kufanya wewe. Mafanikio hayo hutaweza kuyapata kwa jinsi unavyotaka wewe.

Ili kufikia mafanikio makubwa na hatimaye kuwa tajiri, unahitaji kshirikiana na wengine pia. unahitaji kuwa na timu ambayo itakuwa inakusaidaia kufikia ngazi ya juu ya kimafanikio. Huwezi kuwa tajiri kwa kufanya kila kitu wewe, timu ndio itakusukuma zaidi.

Sasa wengi wanakuwa wanakosea pale wanapokuwa wanamawazo ya kuwa matajiri wakubwa lakini wakati huo huo fikra zao zinakua kila wakati kutaka kufanya wao kutokana na sababu mbali mbali walizonazo.

Hakuna mtu ambaye ni tajiri mkubwa pasipo kuwa na timu ya kuweza kumsaidia. Kila mtu unyemwona ni tajiri mkbwa kuna watu ambao wapo chini yake na watu hao anaendana nao vizuri sana katika kuhakikisha kila kitu kinakaa sawa.

Kwa hiyo kama nia yako ni kuwa tajiri, unachotakiwa kukifanya kuanzia leo ni kufuta hizo fikra ambazo ulikuwa nazo na kutengeneza fikra za kishindi ili kuweza kufikia mafanikio makubwa ambayo unayahitaji kwenye maisha yako.

Soma; Achana Na Hadithi Zote Za Uongo, Njia Halisi Ya Mafanikio Yako Iko Hivi.

“Maarifa niliyonayao yananitosha”

Ni ngumu sana kuweza kupiga hatua za kimafanikio kama unaamini kwamba kwa sasa maarifa uliyonayo yanakutosha. Watu wengi wanaamini sana katika hilo hasa wanapotafuta mafanikio yao.

Utakuta  ni watu ambao kwa sasa, hawawezi tena kufanya kitu kingine zaidi ya kuamua kutumia maarifa yao yale yale. Kila wakitaka kujifunza kwa wengine, hawataki kwa kujiamini wao kila kitu kwa sasa wanakijua na kinawatosha.

Ili kuweza kuwa mtu wa mafanikio unatakiwa kuwa na mwendo wa kujifunza kila siku. Hutakiwi kujifunza mara moja na ukasema leo imetosha. unatakiwa kujifunza kwenye vitabu au semina zinazotolewa ili kujenga mafanikio makubwa.

Tambua huwezi kuwa na mafanikio makubwa sana kama unaamini maarifa uliyonayo hapo ulipo yanakutosha. Maarifa siku zote ni lazima kuyatafuta ili kujenga mafanikio endelevu na yasiyo na kikomo.

Kwa maelezo hayo, hizo ndizo fikra chache kama wewe unazo, na unaendelea kuziendeleza naoamba usahau kabisa swala la kuweza kuwa tajiri maishani mwako. Kama nilivyosema kumbuka mafanikio makubwa ni zaidi ya mipango na mawazo uliyonayo.

Kwa makala nyingine za mafanikio, tembelea dirayamafanikio.blogspot.com kujifunza zaidi kwa kina.

Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatimia.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com