Kuna aina kuu mbili za fasihi, fasihi simulizi na fasihi andishi. Kwa asili, sisi binadamu tumeishi kwa kipindi kirefu kwenye fasihi simulizi kuliko fasihi andishi.

Tangu enzi na enzi, watu walikuwa wakifundishana na kurithishana maarifa kwa njia ya hadithi na masimulizi. Kumekuwepo na hadithi nzuri za kufundisha na hata kuburudisha.

Watu wanaelewa sana kitu kinapoelezwa kwa njia ya hadithi kuliko kuelezwa kwa njia ya maelezo ya kawaida. Hata kitu ambacho ni cha kawaida kabisa, kikielezwa kwa njia ya hadithi kinaeleweka vizuri zaidi.

Katika dunia tunayoishi sasa, dunia ambayo kuna kelele za kila aina, ni vigumu sana kusikika kama utakuwa unasema kile ambacho kila mtu anasema.

Hivyo ili kujitofautisha, ili kuweza kusikika kwenye kazi na hata biashara, unahitaji kutumia hadithi. Na siyo tu zile hadithi za sungura na fisi au paka na panya, bali hadithi za mifano yako binafsi, kwa mambo ambayo umeshapitia.

Mwandishi Gabrielle Dolan anatuoa mwongozo sahihi wa kutumia hadithi za mifano yetu binafsi kwenye kazi na biashara zetu ili tuweze kueleweka zaidi na kuwashawishi watu kuchukua hatua.

9780730343295.pdf

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi cha STORIES FOR WORK tujifunze jinsi ya kutumia hadithi za mifano yetu wenyewe kuwashawishi watu kuchukua hatua.

AKILI YETU KWENYE HADITHI.

Akili zetu ndiyo chanzo na kipokezi kikuu cha hadithi mbalimbali. Tunaposimulia au kusikiliza hadithi, yapo mambo yanayotokea kwenye akili zetu ambayo yana maana kubwa kwenye hatua tunazochukua kulingana na hadithi tunayokuwa tumesikia.

  1. Ubongo wa binadamu umegawanyika kwenye sehemu kuu mbili, ubongo wa kulia na ubongo wa kushoto. Ubongo wa kushoto unahusika zaidi na kufikiri kwa kina na mahesabu. Ubongo wa kulia unahusika zaidi na hisia na kumbukumbu. Sasa mtu anaposikia hadithi, ubongo wa kulia unafanya kazi zaidi kuliko ubongo wa kushoto, hivyo hadithi zinaibua hadithi na kutengeneza kumbukumbu.
  2. Ubongo wetu pia una sehemu kuu tatu; sehemu ya kwanza inaitwa ubongo wa mjusi (reptile brain au hind brain) ubongo huu unafanya kazi sawa kwa viumbe wote, ndiyo unaotufanya tuwe hai, tuepuke hatari na kujilinda. Sehemu ya pili ni ubongo wa mnyama (mammal brain au mid brain), hii ni sehemu ya ubongo inayohusika na kujenga mahusiano na hisia. Sehemu ya tatu ni ubongo wa juu (neocortex au fore brain) sehemu hii inahusika na kufikiri na kufanya maamuzi. Tunaposikia hadithi, sehemu hizi zote za ubongo zinafanya kazi kwa pamoja na kushirikiana na ndiyo maana huwa tunaelewa na kukumbuka zaidi hadithi kuliko maelezo ya kawaida.
  3. Homoni ya oksitosini huwa inatolewa kwenye miili yetu pale tunaposikiliza hadithi. Oksitosini huwa inaitwa ni homoni ya kutengeneza mahusiano, ndiyo homoni inayotolewa pale watu wanapofanya mapenzi, mama anapojifungua mtoto na hata mama anaponyonyesha mtoto. Homoni hii ya oksitosini inawezesha watu kuwa pamoja na kuimarisha mahusiano, hivyo unapotumia hadithi kwenye mawasiliano yako, unaimarisha mahusiano yako na wanaokusikiliza.
  4. Tafiti zinaonesha kwamba, sisi binadamu huwa tunafanya maamuzi kwa hisia, kisha kuyadhibitisha kwa kufikiria. Wengi hufikiri kwamba tunafanya maamuzi kwa kufikiria kisha kuyapa hisia, lakini hilo siyo sahihi. Kwa kuwa hadithi zinaibua hisia, ukitaka kuwashawishi watu kuchukua maamuzi, tumia hadithi, zitaibua hisia zao na hizo zitawapelekea kufanya maamuzi, ambayo baadaye watayadhibitisha kwa kufikiri.
  5. Ili hadithi ifanye kazi vizuri kwa watu, inahitaji vitu viwili, kushika umakini wa mtu (attention) na pia kutengeneza mvutano ndani ya mtu (tension). Hadithi inaposhika umakini wa mtu inamfanya asikilize kwa makini na asikubali kusumbuka. Pia inapotengeneza mvutano, inamfanya mtu kuibua hisia ndani yake, za kumweka yeye kama sehemu ya hadithi hiyo. Naamini umewahi kusikia hadithi ya kutisha au kusikitisha, iliyopelekea kujiona wewe kama upo kwenye hali ile, na ukawa na hofu au hata kulia kabisa.

AINA KUU NNE ZA HADITHI UNAZOWEZA KUTUMIA.

Mwandishi anasema zipo aina nyingi sana za hadithi, lakini tunaweza kugawa aina hizi za hadithi kwenye makundi mbalimbali. Wapo ambao wameweza kugawa kwenye makundi kumi, wengine saba, wengine matano. Mwandishi amegawa hadithi zote kwenye makundi makuu manne, na kuonesha namna gani unaweza kutumia kila aina ya hadithi.

  1. Hadithi za ushindi. Aina ya kwanza ya hadithi ni hadithi za ushindi, hizi ni hadithi zinazoonesha mtu kutoka chini mpaka juu, kutoka kwenye mazingira magumu mpaka mazingira mazuri. Kwenye aina hii ya hadithi, unaangalia hatua yoyote ambayo umeweza kupiga kwenye maisha yako, ambayo kwa kuwashirikisha wengine watahamasika kuchukua hatua. Kwa mfano kama ulikuwa kwenye madeni na changamoto za kifedha, ila ukaweza kuondoka kwenye madeni nakufikia uhuru wa kifedha kwa kuchukua hatua fulani, ni hadithi ambayo inaweza kuwahamasisha wengine kuchukua hatua kama ulizochukua wewe.
  2. Hadithi za majanga/maafa. Aina ya pili ya hadithi ni hadithi za majanga. Hizi ni hadithi zinazoonesha changamoto na matatizo ambayo mtu umekutana nayo, ambayo yalikufanya uanguke au ushuke kutoka ulipokuwa. Hadithi za majuto pia zinaingia kwenye eneo hili, kama unajutia kuchukua au kutokuchukua hatua fulani. Hizi ni hadithi unazoweza kutumia kuwatia moyo wengine ambao wanapitia majanga, au wanaoogopa kuchukua hatua kwa kuhofia kuingia kwenye matatizo changamoto.
  3. Hadithi za mvutano. Aina ya tatu ya hadithi ni hadithi za mvutano, hadithi zinazotokana na hali unayopitia, ambayo ni ya mvutano na huwezi kufanya maamuzi sahihi kulingana na hali ya mvutano unayokuwa nayo. Hizi ni hadithi zinazotokana na migogoro ya ndani, pale ambapo unajikuta unalazimika kufanya kinyume na unavyoamini. Pia inaweza kuwa hadithi ya namna ulivyokosea au kwenda kinyume na ulivyoahidi. Hadithi za aina hii zinawafanya watu wakuamini, kwa kukuona kuwa muwazi.
  4. Hadithi za mpito. Aina ya nne ya hadithi ni hadithi za mpito. Hizi ni hadithi za vipindi vya mpito kwenye maisha yako, labda kubadili kazi, kubadili biashara, kuoa/kuolewa, kuacha/kuachwa na mambo mengine makubwa unayopitia kwa kipindi fulani cha maisha yako. Hadithi za aina hii zinaweza kuwashawishi watu kuchukua hatua sahihi kwenye nyakati za mpito.

VITU VIWILI VINAVYOHITAJIKA ILI HADITHI IFANYE KAZI.

Siyo kila hadithi unayoweza kuwaambia watu kwa wakati wowote itafanya kazi. Unaweza kuwapa watu hadithi na badala ya kuwahamasisha ukawa umewakwaza kabisa. Kama ulitegemea watu wakuamini na kununua unachouza, au wakubaliane na mawazo yako, wakakuona kama mtu usiyefaa kabisa na usiyeaminika.

Ili kujua hadithi inayofaa na kwa wakati gani, unahitaji vitu viwili katika kila hadithi unayotaka kutumia.

  1. Kitu cha kwanza na muhimu kabisa kwenye hadithi ni uhalisia. Tumia hadithi ambayo ni kweli na inakuhusisha wewe binafsi, ambayo una uhakika nayo. Hii itakusaidia kuwa sahihi mara zote na watu kukuamini pia. Ukitumia hadithi za wengine, kwanza hutakuwa na uhakika na ukweli wake, na pili, pale watu wanapogundua unatumia hadithi za wengine, wanakosa kukuamini.
  2. Kila hadithi unayotoa kwenye hali fulani, lazima iwe na kusudi ambalo linaendana na maamuzi ambayo unataka watu wachukue. Hadithi lazima iwe inawahamasisha watu kuchukua hatua fulani, ambazo zitatimiza kile unachotaka. Unahitaji kuwa na ujumbe maalumu ambao mtu unataka aondoke nao ili aweze kufanya maamuzi sahihi.

JINSI YA KUPATA NA KUTUMIA HADITHI KWENYE KAZI NA BIASHARA ZAKO.

Watu wengi hufikiri kwamba hawana hadithi wanazoweza kutumia kwenye kazi na biashara zao. Wengi huogopa kutumia hadithi zao binafsi kwa kuona watakuwa wanaweka maisha yao hadharani. Ukweli ni kwamba kila mtu ana hadithi anayoweza kutoa kwa wengine kwa njia ambayo haitakuwa kujiweka wazi, bali kujenga ushawishi na kuaminika zaidi.

  1. Njia rahisi ya kupata hadithi za kutumia ni kufikiria na kuandika kila kitu ambacho umewahi kufanya au kukutana nacho kwenye maisha yako. Chochote ambacho kimewahi kutokea kwenye maisha yako, ambacho unakikumbuka na kuna kitu ulijifunza au kuondoka nacho kiorodheshe. Ukishaorodhesha matukio hayo, yatenge kwenye makundi manne ya hadithi, kisha angalia ni maeneo gani unaweza kutumia kama hadithi, kwenye kazi na biashara zako.
  2. Ukishaanza kuweka matukio ya maisha yako kwenye hadithi, utaanza kuona hadithi kwenye kila eneo la maisha yako. Kila unachokutana nacho kwenye siku yako, utaona namna unavyoweza kukitumia kama hadithi kuwashawishi watu kuchukua hatua zaidi. Watoto, wajomba na mabinamu ni chanzo kizuri sana cha hadithi unazoweza kutumia maeneo mbalimbali.
  3. Ukishakusanya hadithi zako zinazotokana na matukio ya maisha yako, unahitaji kutengeneza hadithi hizo kwenye mfumo mzuri ambao unamwezesha mtu kufuatilia, kuelewa na kuchukua hatua. Mfumo mzuri wa hadithi una maeneo makuu matatu, mwanzo, katikati na mwisho.
  4. Mwanzo mzuri wa hadithi unaanza na kitu ambacho kinamfanya mtu asikilize, awe makini na aache kufikiria kile ambacho anafikiria. Mwanzo mzuri wa hadithi unaanza na muda au eneo. Unakumbuka zile hadithi zinazoanza na ‘hapo zamani za kale…’? Anza hadithi yako kwa kutaja muda, au eneo na watu watakuwa tayari kusikiliza nini kilitokea wakati huo au eneo hilo.
  5. Epuka kuanza hadithi na maelezo ‘wacha nikupe hadithi’ au tujifunze kupitia hadithi hii. Ukianza na kauli kama hizo inamfanya mtu kuona kama umetengeneza hadithi hiyo ili kumshawishi achukue hatua. Unahitaji kuanza na hadithi moja kwa moja, na mtu ataona unamshirikisha uzoefu wako na hivyo kukuamini zaidi.
  6. Katikati ya hadithi ndiyo eneo muhimu sana, kwa sababu wengi huwapoteza watu hapa. Wengi huweka maelezo mengi yasiyo na maana na hata ya kujirudia rudia. Unahitaji nidhamu ya hali ya juu katikati ya hadithi, kueleza machache lakini muhimu na kuhakikisha unaeleweka hasa. Toa maelezo mafupi na yenye kueleweka, kama kitu siyo muhimu usikiweke.
  7. Mwisho wa hadithi ndiyo eneo muhimu sana, hapa unahitaji kuhakikisha mtu amepata ujumbe uliokusudia na kumwezesha kuchukua hatua uliyotaka achukue. Mwisho mzuri wa hadithi una sehemu tatu, daraja la kuunganisha watu na biashara au kazi yako, muunganiko wa kufikisha ujumbe wako na pumziko la kuwafanya watu waelewe ujumbe wako.

MAMBO MENGINE MUHIMU YA KUZINGATIA KWENYE KUTUMIA HADITHI.

Mpaka sasa tumejifunza athari za hadithi kwenye akili, aina za hadithi tunazoweza kutumia na hata namna ya kupata na kutumia hadithi. Yapo mambo mengine muhimu ya kuzingatia ili kuhakikisha tunaweza kutumia hadithi vizuri.

  1. Mazoezi yanakufanya kuwa bora. Hakuna mtu anayekuwa mtumiaji bora wa hadithi kwa mara moja. Bali unahitaji kufanya mazoezi ili kuwa bora. Anza kwa hadithi ndogo ndogo na kwa hadhira ndogo, labda mtu mmoja au watu wachache. Angalia namna gani watu wanachukulia hadithi unayowapa, kisha boresha zaidi. Kadiri unavyofanya, ndivyo unavyozidi kuwa bora.
  2. Unaweza kutumia hadithi kwenye kila eneo la maisha yako, kazi yako na hata biashara yako. Kama unataka kuwashawishi watu kuchukua hatua fulani, hadithi inawasaidia sana kukuelewa. Kama unawataka watu wanunue unachouza, ukiwa na hadithi zinazohusisha hicho unachouza na mafanikio yako na ya wengine, utawashawishi wengi kununua. Kadhalika kama upo kwenye usaili wa kazi, hadithi yako binafsi, ya jinsi ulivyoweza kupiga hatua fulani, itakutofautisha na wengine wanaoomba kazi na wewe.
  3. Hakikisha kila ulipo, kila unachofanya, kuna hadithi unayoweza kuitumia. Kwa kifupi, chochote unachofanya na ambacho kinahusisha wengine, hakikisha una hadithi au mifano halisi ya kuwawezesha watu kukuelewa. Hata kama una data na ukweli kiasi gani, kama utakosa hadithi, utawakosa watu.
  4. Unaweza kutumia hadithi kwa njia mbalimbali, kwenye maongezi ya ana kwa ana na mtu mmoja mmoja, kwenye maongezi mbele ya watu wengi na pia kwenye uandishi wa vitabu, makala, maoni na kadhalika. Popote ulipo na kwa njia yoyote unayoweza kutumia, hakikisha kuna hadithi unayoweza kuwashirikisha watu.

Matumizi ya hadithi ni njia nzuri na rahisi ya kuwashawishi watu na hata kueleweka vizuri. Pata kitabu hichi na tenga muda ukisome, ili uweze kujifunza mengi kuhusiana na matumizi ya hadithi.

Kwenye kitabu, mwandishi ametumia mifano halisi ya hadithi za watu na jinsi zilivyowasaidia kushawishi na hata kueleweka na wengine.

Usomaji

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz