Miujiza hutokea, jambo ambalo halikutegemewa kabisa linatokea, ambaye hakuna anayeweza kuelezea limetokeaje na kwa sababu gani.

Lakini inapokuja kwenye mafanikio, kutegemea miujiza ili kufanikiwa siyo njia sahihi.

Hii ni kwa sababu miujiza ina sifa kuu mbili;

Sifa ya kwanza ni kwamba hutokea mara chache sana, yaani miujiza ni adimu sana. Hivyo kusubiri muujiza utokee ili upate kile unachotaka, ni njia ya kujichelewesha, kwa sababu inatokea mara chache mno.

Sifa ya pili ni kwamba miujiza haitabiriki, huwezi kuitegemea kwa sababu hujui inatokea lini. Sasa hili si zuri kwenye mafanikio, kwa sababu kusubiri kitu ambacho hujui kama kitatokea, na wala hujui kitatokea lini ni kujiandaa kushindwa.

siyo ajali

Hivyo unapofikiria kuhusu mafanikio yako, miujiza isiwe moja ya njia zako za kufika kule unakotaka. Kama itatokea sawa itokee, kama utakuwa na imani kwamba itatokea hakuna shida yoyote.

Kikubwa ni wewe uwe na mpango thabiti wa kuelekea kwenye mafanikio yako, ujue kila hatua ya kupiga ili kufanikiwa. Ujue ni wapi unakwenda na njia ipi unapita ili kufika pale. Na kama utakwama kwa njia yoyote ile, ujue njia mbadala ya kukuwezesha kufika.

SOMA; SIKU YA 9; Siri Ya Utajiri, Mafanikio na Furaha.

Ukishakuwa na mipango hiyo, kinachobaki ni kazi sasa. Weka kazi mpaka upate kile unachotaka, usikubali kwa namna yoyote ile kuishia njiani. Utakutana na vikwazo na changamoto nyingi, lakini usikubali hizo ziwe mwisho wako. Kazana kuendelea mpaka ufike unapotaka.

Usipange na kusema utapata huku ukiwa hujui utapataje, usiseme muujiza utakupa kile unachotaka, hata kama unaamini hivyo, weka kazi kubwa kuhakikisha unapata kile unachotaka.

Na cha kushangaza sana ni kwamba, ukiwa hutegemei muujiza, ukiwa ‘bize’ kuweka juhudi ili kupata unachotaka, ndipo unapokutana na muujiza kwenye mazingira ambayo hukutegemea. Maana halisi huwa inawapendelea wale wanaochukua hatua.

Hivyo nimalize kwa kusema, usisubiri muujiza, badala yake tengeneza muujiza.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog