Unapokuwa na uhitaji mkubwa na muhimu sana kwenye maisha yako, hutakubali kujaribu watu wengi kupata uhitaji huo, bali utakachohitaji ni kupata aliye bora katika kukutimizia uhitaji huo.
Kwa mfano unaumwa ugonjwa ambao ni hatari sana, lakini una tiba, na fedha kwako siyo changamoto. Je utaanza kujaribu jaribu kila daktari katika kutibu ugonjwa huo au utaenda kwa daktari bingwa kabisa wa magonjwa ya aina hiyo akutibu?
Unaona jinsi ambavyo ukiwa na uhitaji moja kwa moja unakwenda kwenye ubora?
Hivi sasa ndivyo unavyopaswa kuwafanya wengine kuja kwako.
Tatizo kubwa kwa wengi, kwa kazi wanazofanya, biashara wanazofanya ni kwamba wanafichwa. Wanafichwa kwa sababu wapo wengi wanaofanya na kelele pia ni nyingi.

Kila mtu kuna kitu anaahidi, lakini wengi hawatimizi, hivyo wateja na wale wanaotegemea kile mnachofanya wanakuwa wameshachoka na mwishowe wanaamua tu kuhudumiwa na yeyote, kwa sababu wanaona wote ni wale wale na hakuna tofauti yoyote kubwa.
Sasa hapo ndipo ilipo fursa kubwa sana kwako, fursa ya kuweza kuwafikia wengi, kuwafanya wengi waje kwako na kuweza kuwafanyia makubwa.
Fursa hii inaanza na kuiambia dunia kwamba wewe ni bora kabisa kwenye kile unachofanya. Najua hilo ni gumu kwa wengi, kwa sababu utaonekana kama unajisifia au unaringa. Lakini kwa namna dunia inavyoenda, kukaa kimya ni kujipoteza.
Husemi hili kwa njia ya kujionesha kwamba wewe ni wa muhimu kuliko wengine, au wewe ndiyo wewe na wengine hawafai. Bali unasema hivyo kuwataarifu watu kwamba kama wanahitaji kupata kilicho bora, wasihangaike kupoteza muda wao sehemu nyingine bali waje kwako.
SOMA; #TAFAKARI YA LEO; ZUNGUKWA NA WANAOKUFANYA UWE BORA…
Sasa kutoa kauli kama hii ni mtego mkubwa, kwa sababu watakuja watu kutaka kuona kama madai yako ni ya kweli, watakuja kukujaribu kuona huo ubora unaosema unao.
Na hapo ndipo unapohitaji kufanya kweli. Usiwe kama wengi ambao waahidi mengi lakini hawayatekelezi. Wewe tekeleza kweli, sema wewe ni bora na fanya kwa ubora wa hali ya juu sana.
Weka kila aina ya juhudi unayoweza kuweka, jali zaidi na kazana kutimiza kile ambacho umeahidi. Na kwa njia hii, utakuwa bora kama unavyosema.
Usiogope kwamba utashindwa kutimiza hilo uliloahidi kwamba wewe ni bora, kwa sababu wengi sana wanafanya kwa kawaida, wengi wanafanya kwa mazoea, hivyo kama utapiga hatua kidogo tu kuondoka kwenye mazoea, basi utaweza kuleta matokeo makubwa sana.
Hakuna ubaya wowote kuiambia dunia kwamba wewe ni bora kama unaweza kutekeleza hilo. Wale walioshindwa na kukata tamaa na maisha yao watakuambia siyo vizuri kujisifia, watakuambia ni bora ukae kimya, lakini kumbuka wao wamekaa kimya kwa sababu hawana chochote wanaweza kufanya kwa ubora.
Kama kuna kitu unaweza kukifanya vizuri, kama upo tayari kujitoa na kuwasaidia watu kwenye kile unachofanya. Basi hakikisha kila anayeweza kunufaika na kile unachofanya anajua kuhusu uwepo wako. Na siyo tu anajua kwamba upo, bali anajua kwamba wewe ni bora kabisa, na kwa uhitaji alionao, akifika kwako anapata suluhisho sahihi kwake.
Ni kipi unaweza kufanya kwa ubora wa kipekee kabisa? Ifanye dunia ijue kuhusu hilo ili uondoke mafichoni.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog