Asili, yaani ulimwengu kwa ujumla wake, huwa inawaandaa viumbe hai wote kwenye kuendana na mazingira ambayo viumbe hawa wanajikuta.

Kwa mfano, mmea ambao unaota kwenye eneo la jangwa, huwa na majani madogo na membamba, wakati mwingine miiba kabisa. Hii inapunguza mmea huo kupoteza maji mengi kwenye mazingira hayo ya jangwa. Lakini mimea inayoota kwenye eneo lenye mvua za kutosha, huwa na majani mapana.

Kadhalika kwa wanyama, simba kwa sababu anakula nyama, ana meno makali ya kurarua, lakini swala anayekula majani, ana meno ya kusaga.

Tunachoona ni kwamba, asili haitengenezi matatizo ambayo kiumbe atashindwa kuyatatua. Inatengeneza matatizo ambayo yanaendana na kiumbe husika, au inahakikisha kiumbe huyo ana njia za kupambana na matatizo yanayoweza kujitokeza.

 

FurahaLakini sasa, sisi binadamu, kwa uwezo wetu mkubwa wa kufikiri kuliko viumbe wengine walio chini yetu, huwa tunatengeneza matatizo mbalimbali. Na matatizo haya yamekuwa magumu sana kwetu kutatua, kwa sababu uwezo wetu juu ya kuandaa mazingira ya kutatua matatizo haya ni mgumu sana.

Kwa mfano magonjwa mbalimbali ambayo tunayatengeneza kwa mitindo mibaya ya maisha, yamekuwa magonjwa magumu sana kutatua. Magonjwa kama kisukari na shinikizo kubwa la damu, ni magonjwa ambayo mtu akishayapata hayatibiki moja kwa moja.

SOMA; UKURASA WA 872; Mshumaa Usioisha…

Na hata matatizo yetu ya ufanyaji wa kazi, usimamizi wa muda, yanazidi kuwa magumu kwa sababu tumeyatengeneza sisi wenyewe. Kwa mfano siku za nyuma hakukuwa na mitandao ya kijamii wala simu janja, watu waliweza kutumia muda wao vizuri kwa yale ambayo ni muhimu.

Lakini zama hizi za mitandao ya kijamii na simu janja, kila mtu analia na muda, kila mtu anatamani apate muda zaidi lakini hawezi kuondokana kabisa na mitandao hii.

Tunatengeneza matatizo kisha matatizo haya yanakuwa gereza letu, tunakazana kuyatatua na tunashindwa kabisa.

Hivyo hatua muhimu sana kwetu, ni tuache kutengeneza matatizo. Kwenye kila kitu unachopanga kufanya, subiri na utafakari je ni matatizo gani unayoweza kutengeneza kwako binafsi?

Kila unapotaka kula chakula, kila unapotaka kununua kitu, kila unapotaka kusema kitu, jipe sekunde chache za kufikiri je ni tatizo gani unaweza kuwa unatengeneza?

Hii itakuepusha kuja kuhangaika na matatizo ambayo umejitengenezea lakini huwezi kuyatatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog