Tunapokutana na kitu kigumu kwenye maisha, tunasema ni kazi kweli kweli.
Hii inaonesha ni kwa namna gani tunaitafsiri kazi kwenye akili zetu, kwamba ni kitu chochote ambacho ni kigumu na ambacho hatupo tayari.
Sasa kama chochote unachofanya kwenye maisha yako kinakuwa kazi, unakuwa umeshashindwa kabla hata hujaanza.

Ukiangalia watu wa kawaida, huwa wanafanya kile wanachofanya kama kazi, hivyo wanafanya kwa kiasi, kwa namna ambavyo wengine wanafanya.
Lakini wale ambao wamefanikiwa huwa wanafanya kama mapenzi, hawaoni kama mzigo wala ugumu. Badala yake wanaona kama kitu wanachopenda kufanya, ambacho ni muhimu kwao na wengine pia.
Kwa namna hiyo wanajituma sana, wanaweka juhudi kubwa na wanafanya kwa viwango vikubwa mno.
SOMA; UKURASA WA 888; Raha Leo, Maumivu Kesho…
Acha kuita kile unachokifanya kazi, badala yake kiite sehemu ya maisha yako, ona ndiyo mchango ambao maisha yako yanatoa kwenye dunia hii. Kwa mtazamo huo utaweka juhudi kubwa zaidi ili kuweza kutoa matokeo bora sana.
Usifanye tu kwa kiasi ili uonekane kwamba umefanya, au kama wengine wanavyofanya. Badala yake fanya kwa viwango vya juu sana, fanya kwa namna ambavyo unakuwa umetoa thamani kubwa kwa wale wanaotegemea kile unachofanya.
Ikishakuwa ni kazi kwako, jua kabisa umefika kwenye hatua ya kushindwa. Lakini ikiwa ni mapenzi kwako, ikiwa ni kile ambacho upo tayari kufanya, hata kama kwa wengine kinaonekana ni kigumu kiasi gani, upo kwenye njia nzuri ya mafanikio.
Isiwe kazi, iwe mapenzi, iwe mchango mkubwa unaotoa kwa wengine, iwe thamani unayoongeza kwa wengine na iwe alama unayoacha hapa duniani.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog