Ukisikie neno Msamaria mwema unapata picha gani? Kwa wengi ni mtu ambaye anajitoa kuhakikisha maisha ya wengine yanakuwa bora zaidi, hata kama hakuna anachonufaika nacho moja kwa moja kwa kufanya hivyo.
Sasa zipo zawadi kuu mbili ambazo kila mmoja wetu anazo, lakini namna tunavyozitumia tunatofautiana.
Zawadi ya kwanza ni upendo. Hii ni zawadi ambayo mtu unapaswa kujipa wewe binafsi. Iwapo upendo hautaanzia kwako, hakuna namna upendo huo unaweza kwenda kwa wengine.

Lazima uanze kwa kujipenda wewe mwenyewe kwanza, kisha upendo huo unaweza kuwa na manufaa kwa wengine pia. Ukijipenda hata wengine wananufaika na maisha yako, moja kwa moja au hata kama siyo moja kwa moja.
Zawadi ya pili ni wema, hii ni zawadi ambayo mtu unawapa watu wengine. Ni zawadi ambayo wengine wananufaika nayo kutoka kwako. Unapokuwa mwema kwa wengine, unapochukua hatua ambazo zinafanya maisha ya wengine kuwa bora, hata kama wewe hunufaiki moja kwa moja, ni kitu kikubwa sana kwako na kwa wengine pia.
SOMA; UKURASA WA 1003; Njia Bora Ya Kuwakasirisha Wanaokukasirisha…
Tumia zawadi hizi mbili vizuri, ili kuweza kuwa na maisha bora. Jipe zawadi ya upendo ili maisha yako yawe bora, uweze kupiga hatua na kufanikiwa zaidi. Pia wape wengine zawadi ya wema, kwa kuchukua hatua za kuyafanya maisha yao kuwa bora zaidi.
Bila ya kujipenda wewe mwenyewe, maisha yako hayawezi kukamilika, kila wakati utajiona kuna kitu unakosa na mambo yatakuwa magumu.
Na siyo lazima umpende kila mtu, kwa sababu upendo unahitaji kujuana, angalau kwa kiasi fulani. Unapokutana na mtu kwa mara ya kwanza kunaweza kusiwe na kitu cha kujenga upendo baina yenu. Lakini ni muhimu sana umjali kila mtu, uwe mwema kwa kila mtu. Hata kama mtu anaonekana ni msumbufu na mwenye nia mbaya, kuwa mwema kwake, kutakusaidia sana wewe.
Zingatia zawadi hizi, upendo na wema, na kila siku gawa zawadi hizi kadiri uwezavyo, unazihitaji sana na wengine wanazihitaji pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog