Kuanza jambo lolote jipya, huwa ni kugumu. Hii ni kwa sababu wengi huwa tunafikiria makubwa. Kwamba mtu anapotaka kuanza kitu, anawaangalia wale ambao tayari wameshafanya kwa muda mrefu na kufika juu kabisa.

Kwa mfano kama unataka kuanza biashara, halafu unaowaangalia ni wakina Mengi au Bakhresa, utaona kwamba wako mbali sana, na hivyo itakuumiza unaanzaje mpaka kuweza kufika hatua kama walizofikia wao.

Tatizo kubwa

Inawezekana kabisa kufika hatua kubwa kwenye jambo lolote, lakini hapo siyo unapopaswa kuanzia, na wala hilo halipaswi kukukwamisha wewe kuanza.

Unachopaswa kukazana nacho, anza na mtu mmoja. Chochote unachopanga kuanza, anza na mtu mmoja. Hii ni hatua ya chini kabisa, ambayo kila mtu anaweza kuanza nayo. Ni hatua ambayo haiwezi kumshinda yeyote ambaye anataka kuanza kweli.

Kama unataka kuanza biashara, anza na mteja mmoja, ambaye ana tatizo fulani, ambalo wewe unaweza kulitatua, kisha litatue. Kwa kumpa kile anachotaka au kumpa suluhisho la changamoto anazopitia.

Kadhalika kama unataka kuwa mwandishi au hata msanii, anza kumwandikia mtu mmoja, anza kumchorea mtu mmoja na anza kumwimbia mtu mmoja.

SOMA; UKURASA WA 1096; Kufuata Ramani Na Kutengeneza Ramani…

Sasa unajua maajabu yanaanzia wapi? Dunia haina mtu mmoja pekee, na matatizo au changamoto zozote, huwa zinawaathiri watu wengi pia. Na muhimu zaidi, watu wana ndugu, jamaa na marafiki. Hivyo hizi zote zinawavutia wengi zaidi kuja kwako, kupata kile ambacho umeanza kukitoa kwa mtu mmoja.

Unapotoa huduma bora sana kwa mtu mmoja, unapoweka thamani kubwa kuhakikisha mtu huyo anapata kile anachotaka, haitaishia kwake, atawaambia wengine na pia wengine wataona, halafu na wao watakuja kwako ili kupata kile ambacho wameona wengine wanapata.

Chochote unachotaka kuanza, usikwame kwa sababu unaona ukubwa ambao huwezi kuufikia, badala yake anza na mtu mmoja, kisha kazana kutoa kilicho bora kabisa kwa huyo mmoja na yeye, juhudi zako pamoja na thamani unayotoa, vitawavutia wengi zaidi.

Hakuna anayeshindwa kuanza na mmoja, ila wengi wanakosa uvumilivu. Jenga uvumilivu na kuwa tayari kuanza kidogo na kukua kwa hatua.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog