Mpendwa rafiki,

Tabia zetu ndiyo zinaathiri maisha yetu kwa kiasi kikubwa sana. kila kitu ni tabia, hata wewe leo unasoma hapa ni tabia uliyojijengea kuwa niingia mtandao wa Amka Mtanzania nitasoma makala  au huenda ulikuwa una shida ya kitu fulani ukaingia katika mtandao na search engine yako ikakuleta hapa  na hatimaye unafaidika na maarifa.

Kufanya mazoezi kwa mtu ni tabia wala siyo kitu kingine, kuweka akiba kwa mtu ni tabia. Kukopa kwa mtu ni tabia yake haijawahi kutokea eti umeamka tu ukawa na deni kubwa sana hapana bali ni tabia ya mtu ya kukopa kila siku au kila mara na kukosa nidhamu ya fedha hatimaye inakuja kuzaa deni kubwa kama hilo.

Muda tulionao

Mpendwa msomaji, ulishawahi kukaa chini na kujiuliza kwanini tunarudia makosa mengi kila siku katika maisha yetu? nina hakika kuwa makosa mengi  tunayofanya huwa yanajirudia sasa kwanini inakuwa hivyo? Au watu wanakimbia makosa yao ndiyo maana makosa yanajirudia kila siku? Hebu jiulize rafiki ni kwa sababu gani?

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Harmonic Wealth (Siri Ya Kuvuta Maisha Unayoyataka).

Hivyo basi, tunarudia makosa mengi kwa sababu ya kukosa muda wa kutafakari na kupitia  makosa yetu tunayofanya kila siku. Je una desturi ya kutenga muda kila siku wa kupitia yako ilikwendaje? Huenda jawabu ni hapana labda unaishi kienyeji, kimazoea unaishi tu ili mradi siku ziende, unaamka unaenda katika shughuli zako ukirudi unalala tu huna hata habari ya kukaa chini kupitia siku ilikwendaje, je kuna mambo gani mazuri uliyofanya ndani ya siku husika ili kesho uyaboreshe zaidi? Je ni mambo gani ambayo umekwenda mrama na umejifunza nini kupitia hayo makosa uliyofanya siku husika? Je ulichukua hatua chanya za kutatua tatizo au ulikimbia tatizo?

Kila siku tenga muda wa kupitia siku yako kwa kufanya hivyo utayajua mazuri na mabaya hivyo itakuwa ni ngumu tena kuyarudia makosa. Shida ya watu wengi hawapendi kukaa chini hata dakika kumi na tano wakiwa pekee yao, mtu akijiona mpweke tu anatafuta kitu cha kusikiliza, kukimbilia kwenye mitandao ya kijamii ili kuondoa upweke.

Hakika maisha ya binadamu wa karne hii yamekuwa ni maisha ya kujikimbia sisi wenyewe, hatutaki kujisikiliza hata kidogo, tumesahau ya kuwa sauti yako ya ndani ndiyo mafanikio yako. je usipokuwa na muda wa kujisikiliza maana yake nini? Maana yake unakimbiza mafanikio ndani yako, haya yote ya jinsi ya kusikiliza sauti yako ya ndani utaweza kujifunza zaidi kwenye kitabu cha Ongea Lugha yako.

SOMA; Ifahamu Sehemu Pekee Ambayo Huwezi Kudanganya Watu Wote

Rafiki, usifanye makosa tena ya kutotenga muda wa kupitia siku yako, mtu anayesema hana muda na mshangaa sana kwa sababu kama unapata muda wa kuangalia tv, kuingia kwenye mitandao ya kijamii, unapata muda wa kula, muda wa kuoga, kupiga mswaki na mengine mengi utashindwaje kupata muda wa kutafakari na kupitia siku yako ilikwendaje?

Hatua ya kuchukua leo, unarudia makosa kila siku kwa sababu ya kutotenga muda wa kupitia siku yako. hivyo anza zoezi la kuwa na mfumo katika maisha yako, ipangilie siku yako vizuri kuanzia unapotoka kitandani mpaka unaingia tena kitandani. Kila muda wako hakikisha umeupangilia vizuri na usisahau kuweka ratiba ya kuweka ratiba ya kupitia siku yako.

Kwahiyo, unapokimbia makosa yako kumbuka kabisa huwezi kukimbia matokeo yake hivyo njia nzuri ni kuyatatua tu lakini ukikimbia utayapata tu matokeo yake popote pale ulipo. Ni rahisi kukimbia matatizo yako lakini ni ngumu kukimbia matokeo yako.

Ukawe na siku bora rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

Mawasiliano; +255717101505//+255767101504, deokessy.dk@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kutembelea mtandao  wa KESSY DEO(www.mtaalamu.net/kessydeo ) kujifunza zaidi kila siku. Asante sana!