Ukiwa unasikiliza redio, labda kuna kipindi kizuri ulikuwa unasikiliza, halafu kikaisha na kikaja kipindi kingine, ambacho siyo kizuri kwako huwa unafanya nini? Je unakaa na kuanza kulalamika kwa nini redio hiyo imeleta kipindi ambacho siyo kizuri wakati wewe unataka kusikiliza vipindi vizuri? Kama akili yako iko sawa huwezi kufanya hivyo.
Unachofanya ni kubadili stesheni ya redio. Na utabadili mara nyingi uwezavyo mpaka ufike kwenye stesheni ambayo inaendana na kile unachotaka. Labda kwenye kubadili badili unafika kwenye stesheni yenye muziki unaopenda, na ukasikiliza. Labda pia baada ya wimbo mmoja, zinazofuata zikawa siyo nzuri kwako, unaendelea kubadili tena.
Sasa hili tunalofanya kwenye stesheni za redio, tunaweza kulifanya vizuri sana kwenye akili na mawazo yetu.

Mara kwa mara kuna mawazo yanatuingia kwenye akili zetu, mawazo ambayo siyo mazuri kwetu. Yanaweza kuwa mawazo ya hofu, mawazo ya kukata tamaa au mawazo ya kushindwa. Haya ni mawazo ambayo yakishakuingia yanakuondolea kabisa nguvu na hamasa za kuchukua hatua. Yanakufanya unywee kabisa na ukose kujiamini.
Unachohitaji kufanya kwenye hali kama hiyo ni kubadili stesheni ya mawazo. Unapogundua tu mawazo ya hofu na kushindwa yameingia kwenye akili yako, yaondoe haraka kwa kubadili mawazo. Jipeleke kwenye mawazo ya aina nyingine, jikumbushe mambo makubwa na magumu uliyowahi kufanya na kufanikiwa, jikumbushe nyakati za furaha kabisa kwenye maisha yako.
SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FAIL FORWARD (Hatua 15 Za Kufikia Mafanikio Kupitia Kushindwa).
Kwa kufanya hivi, unabadili mawazo yako na unarudisha ile hali ya kujiamini na hamasa ya kuchukua hatua. Mawazo hayo ya kushinda na mafanikio yanakupa nguvu mpya ya kuweza kuchukua hatua.
Usikubali kabisa mawazo yanayoingia kwenye akili yako yawe sehemu ya wewe kurudi nyuma. Na ukishagundua chanzo cha mawazo hayo, kaa nacho mbali. Kama ni watu wanakuletea habari za kushindwa, basi kaa mbali na watu wa aina hiyo. Kama ni habari chanya unazosoma zinakufanya uone mambo ni magumu, achana na habari hizo.
Akili yako inapokea kila aina ya mawazo na kuyafanyia kazi, hivyo hakikisha mawazo yanayoingia kwenye akili yako ni mawazo ambayo ni bora kabisa, yanayokupa hasama ya kuchukua hatua. Kama siyo jua una uhuru wa kubadili stesheni ya mawazo, na hakikisha unazo stesheni nyingi za mawazo mazuri.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog