Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo. Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana. Hatua ndogo unazochukua leo ndiyo zinatengeneza mafanikio makubwa kwako kwa siku zijazo.

Karibu kwenye makala yetu ya leo ya USHAURI WA CHANGAMOTO zinazotuzuia kufanikiwa kwenye maisha yetu. Kupitia makala hizi, wewe rafiki yangu unanitumia changamoto yako kisha mimi nakushauri kulingana na uelewa, maarifa na uzoefu ambao ninao.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kuangalia mambo mawili kwa pamoja, yote yanahusisha biashara. Jambo la kwanza ni mambo ya kuzingatia pale unapoanza biashara sehemu yenye ushindani. Na jambo la pili ni usimamizi bora wa biashara kwa wale ambao wameajiriwa na hawana muda wa kuwa kwenye biashara zao.

Lakini kabla hatujaingia kwenye kina kwenye mambo hayo, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye mambo hayo mawili.

Changamoto yangu ni nifanyeje ili kuanzisha biashara sehemu ambayo tayari kuna biashara ya aina hiyo? Je, kuajiri mtu kusimamia hiyo biashara hakuwezi kuathiri biashara yangu kwakuwa nami nimeajiriwa na muda mwingi nakuwa kazini? Nifanyeje ili kuendesha biashara hiyo? Ahsante. – Laurent A. S.

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu hapo, wapo wengine pia ambao wamekwama kama yeye, hivyo wote kwa pamoja twende tukajifunze mambo muhimu sana kuzingatia.

KUANZA BIASHARA ENEO LENYE USHINDANI.

Biashara za zama hizi zimekuwa na changamoto moja kubwa ambayo ni ushindani. Hakuna biashara ambayo unaweza kuwa unaifanya wewe mwenyewe tu. Labda utaenda sehemu na kukuta tayari inafanyika, au kama haifanyiki, ukatapo anza kuifanya basi wengine wataona inalipa na kuanza kuifanya.

Hivyo unapoanza biashara eneo ambalo lina ushindani zingatia mambo yafuatayo;

  1. Jitofautishe na wale wanaofanya biashara hiyo.

Kufanya biashara ile ile ambayo inafanywa na wengine, kwa njia ile ile ni kujiandaa kushindwa. Unahitaji kujitofautisha na wengine, kwa namna ambavyo unatoa huduma zako. Mteja anapaswa kuwa na sababu ya kuwaacha wengine wote na kuja kununua kwako. Ataweza kufanya hivyo kama utakuwa na kitu cha kipekee unachotoa ambacho hawezi kukipata kwingine.

  1. Toa huduma bora sana kwa wateja wako.

Unapoingia kwenye biashara yenye ushindani, kitakachokuokoa ni huduma unazotoa kwa wateja wako. Wateja ni watu ambao wanataka kujaliwa na kuthaminiwa, wanataka kuonekana ni wa muhimu na siyo tu watu ambao wamekuja kununua. Hivyo tengeneza mahusiano mazuri na wateja wako, waone biashara yako ni sehemu ya maisha yao, sehemu inayofanya maisha yao yawe bora, na watakuja kila wakati kwenye biashara yako.

  1. Usishindane, bali kuwa bora.

Wengi wanapoingia kwenye biashara zenye ushindani, wanachokimbilia kufanya ni kushindana, na eneo ambalo wengi hupenda kushindana ni kwenye bei, kwa kupunguza bei. Sasa ukishakimbilia kuuza kwa bei ndogo, jua wengine nao wanaweza kushusha na mwisho wa siku wote mtakuwa mnauza kwa bei ndogo na hakuna anayetengeneza faida. Wewe usishindane, badala yake kazana kuwa bora zaidi kila siku, kazana kutoa thamani kubwa zaidi, ka kuangalia changamoto na mahitaji ya wateja wako.

  1. Jua madhaifu ya wengine na yafanyie kazi.

Kila biashara ina madhaifu yake, hivyo kwenye washindani wako kibiashara, jua madhaifu yao na yafanyie kazi kwenye biashara yako. Angalia wateja wanakosa nini kule kwa washindani wako na hakikisha kwako wanakipata. Angalia wateja wanalalamikia nini kwa washindani wako na hakikisha kwako wanakipata vizuri. Kupitia madhaifu na mapungufu ya wengine, unaweza kupata fursa kubwa ya kufanikiwa kibiashara.

  1. Tumia akili, badili biashara au badili eneo.

Pamoja na mbinu nzuri za kupata wateja kwenye ushindani, bado unahitaji kutumia akili yako kwenye kufanya maamuzi sahihi. Kwa mfano kama eneo tayari lina wafanyabiashara wengi wa aina ya biashara unayotaka kufanya, kuweka biashara yako hata kama itakuwa bora itakuhitaji kazi kubwa sana na mwisho wa siku mtakuwa mnagawana wateja wale wale. Hivyo angalia ni namna gani unaweza kuanzisha biashara ya tofauti kwenye eneo hilo, kwa kuangalia kile ambacho watu wanakosa. Na kama huwezi kuanzisha biashara nyingine, basi angalia eneo tofauti unaloweza kupeleka biashara yako.

Zingatia mambo hayo matano na utaweza kuanzisha na kukuza biashara yako licha ya kuwa na ushindani mkali.

USIMAMIZI BORA WA BIASHARA KWA WALIOAJIRIWA.

Kuanza biashara ukiwa bado upo kwenye ajira ni njia bora sana ya kuingia kwenye biashara kwa sababu inakupa usalama wa kipato na wakati huo huo unajenga usalama zaidi wa kipato baadaye.

Lakini kutokana na ajira kukubana, huwezi kuwa kwenye biashara yako muda wote, hivyo utahitaji kuajiri watu wa kukusaidia kwenye biashara yako hiyo. Na hapa ndipo changamoto za biashara nyingi zinapoanzia, kwa sababu watu wanaoachwa kwenye biashara hizo hawajali sana, na wenye biashara wanakosa njia bora ya kusimamia biashara hizo.

Yafuatayo ni mambo muhimu kuzingatia ili kuweza kusimamia biashara vizuri pale unapokuwa upo kwenye ajira.

  1. Ajiri vizuri.

Sehemu ya kwanza na muhimu kwenye uendeshaji wa biashara ukiwa umeajiriwa ni kwenye kuajiri. Hakikisha unaajiri vizuri, kwa kutafuta mfanyakazi ambaye ataweza kuisimamia biashara yako vizuri. Na hapa unahitaji kuangalia sifa muhimu tatu; uadilifu, akili na nguvu. Uadilifu ni sifa ya kwanza na muhimu sana, na kama mtu hana, hata kama ana uwezo kiasi gani, achana naye kwa sababu atakuingiza kwenye matatizo. Sifa hizi ni za kuangalia kwa mtu ambaye tayari yupo, usidanganyike kwamba mtu atabadilika, watu huwa hawabadiliki haraka.

  1. Biashara yako isiwe mbali sana na unapoishi au kufanya kazi.

Pamoja na kwamba umeajiriwa, hakikisha biashara yako inakuwa karibu na unakoishi au unapofanya kazi. Sehemu ambayo kila siku unaweza kupita na kuangalia nini kinaendelea. Usianzishe biashara eneo ambalo ni mbali na huwezi kulifikia kila siku au mara kwa mara, labda kama ni kilimo. Lakini kwa  biashara za kawaida, iwe sehemu ambayo unaweza kuifikia kwa urahisi.

  1. Pita kwenye biashara yako kila siku, na kuwa na vipimo vya kuona kila kinachofanyika.

Hata kama ajira yako imekubana kiasi gani, hakikisha kila siku au mara kwa mara unapita kwenye biashara yako. Na usipite tu pale kushangaa kama mteja, bali kuwa na vipimo vya kujua kila kinachofanyika pale kwenye biashara yako. Kwa mfano unaweza kuwa na mfumo wa kompyuta wa kuorodhesha bidhaa na huduma zilizouzwa, au hata kuwa na daftari ambalo linaorodhesha vitu vilivyouzwa. Pia kila siku piga hesabu za fedha ili kujua mapato na matumizi na kuhakikisha yanaendana kweli na mauzo yaliyofanywa. Nakusisitiza ufanye hili kila siku au mara kwa mara ili kama kuna tatizo ulione haraka.

  1. Chukua hatua haraka unapoanza kuona matatizo.

Katika usimamizi wako wa biashara, unapoona matatizo fulani yanaanza kujitokeza, basi chukua hatua haraka. Usisubiri au kupuuzia, itakugharimu kiasi kikubwa. Ukishaona mpaka wewe unayaona matatizo, basi jua ni makubwa. Iwe ni kwa mfanyakazi wako au mambo mengine, chukua hatua mara moja. Wafanyakazi wengi wakishazoea biashara huanza kuziendesha kwa mazoea, na wakishajua ratiba zako wanaweza kujenga mazingira ya kukudanganya kwa wakati unapokuwepo. Hakikisha unakuwa na njia ya kuvunja mazoea ya aina hiyo, na unapoona mambo yanakwenda tofauti, chukua hatua haraka.

  1. Soma kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA.

Kuna kitabu nimenadika kinaitwa biashara ndani ya ajira, ndani ya kitabu hichi nimeshirikisha maarifa yote muhimu ya kuanza na kufanikiwa kwenye biashara ukiwa bado upo kwenye ajira. Hichi ni kitabu ambacho kila aliyepo kwenye ajira na anafanya au anataka kufanya biashara anapaswa kukisoma.

BIASHARA NDANI YA AJIRA SOFT

Kitabu kinapatikana kwa softcopy na hardcopy. Softcopy inatumwa kwa email na gharama yake ni tsh 10,000/= kukipata tuma fedha kwa namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma email yako na utatumiwa kitabu. Hardcopy inapatikana kwenye duka la vitabu HOUSE OF WISDOM lililopo Dar, posta mtaa wa samora jengo la NHC karibu na makao makuu ya TTCL.

Unaweza kuendesha biashara yako vizuri ukiwa bado upo kwenye ajira na biashara hiyo ikawa njia yako ya kuondoka kwenye ajira na kuwa na uhuru wa kipato. Jifunze njia za kuendesha biashara yako vizuri na chukua hatua ili kuweza kupiga hatua.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog