The world turns aside to let any man pass who knows where he is going. – Epictetus

Hongera mwanamafanikio kwa nafasi hii nzuri na ya kipekee sana ya leo.
Ni fursa nzuri ya kwenda kuweka juhudi kubwa kwa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambaopo tutaweza kupata matokeo bora sana.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu wa mafanikio kwa mwaka huu 2018.

Asubuhi ya leo tutafakari DUNIA ITAKUPISHA…
Kama unajua wapi unataka kufika, au nini unataka kupata, na upo tayari kufanya kila linalowezekana kufika au kupata unachotaka, dunia itakupisha upate hicho unachotaka.

Lakini kama hujui unataka nini, au kama unajua lakini hupo tayari kujitoa hasa kuhakikisha unakipata, dunia itakuwa kikwazo kikubwa sana kwako.
Dunia ina kila kitu ambacho tunakitaka, lakini huwa haitoi kirahisi,
Ina tabia ya kupima kwanza kila anayetaka, je anataka kweli na yupo tayari kulipa gharama? Au anataka tu juu juu?

Ni kwa wale wanaotaka kweli, wale wasiosimamisha na chochote, wale walio tayari kufanya kila kinachohitajika kufanyika ndiyo dunia inawapisha wapate kile wanachotaka.

Lakini wale wanaojaribu, wanaoona wengine wamepata na wakafikiri hata wao wanaweza kupata, wanaokimbilia kulalamika na kuacha pale wanapokutana na changamoto, ndiyo ambao dunia inakuwa ngumu sana kwao.

Hivyo rafiki yangu, jua hasa kile unachotaka, kuwa tayari kufanya kila kinachohitajika kufanyika na kuwa mbishi, king’ang’anizi na mvumilivu na dunia itakuwa haina namna bali kukupisha upate kile unachotaka.

Ukawe na siku bora sana leo rafiki yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha