Kupata matokeo bora kwako na kwa wanaokuzunguka kwanza unatakiwa kuboresha mategemeo yako. Unatakiwa kuboresha kile unachokitegemea, ni kitu gani ambacho unachokitegemea kwenye maisha yako, ndicho kitakupa matokeo ya aina fulani.

Unapokuwa na mategemeo bora, mategemeo hayo yanakupa matokeo bora pia. Kuwa na mategemeo bora, yanakufanya hata kazi zako uzifanye kwa mtazamo chanya sana, tofauti na ukiwa na mategemeo hasi ambayo kitu hicho hakiwezi kutokea.

Tegemea kuboresha hali yoyote mbovu kwako na kuwa bora na hilo linawezekana. Tegemea kila siku unayoanza, itakuwa ni siku ya ushindi na mafanikio makubwa kwako. Tegemea kukutana na fursa na tegemea mambo yako yataenda vizuri.

chura na ng'e

Mategemeo chanya kwenye maisha yako, yanaleta matokeo chanya pia. Hakuna mategemeo hasi ambayo yatakupa matokeo chanya. Kila anayetegemea chanya, anatengeneza uwezekano wa kuvuta chanya maishani mwake.

Unavuna ulichopanda, hakuna kinyume cha hili na hauwezi kuvunja sheria hii. Halikadhalika, unavuna matokeo ya mategemeo yako. Kitu gani unakitegemea kwenye maisha yako, utakipata tu kitu hicho hata kama si leo.

Ukiwaangalia watu wengi walioshindwa kwenye maisha ni watu ambao mara zote wana mategemeo hasi sana. Kama unafikiri natania,mtafute mtu mmoja aliyeshindwa kisha muulize anategemea nini kwenye maisha yake? Utasikia tu atakachokwambia.

Sina shaka badala ya kusikia kile anachotegemea utaanza kusikia kwanza malalamiko na mwisho wa siku utasikia kwa sababu sina mtaji basi na ndio siwezi kuanzisha biashara. Najua mpaka hapo utaelewa mategemeo yapo chini au hakuna kabisa.

Unatakiwa kuacha kuishi kwa mazoea kwa kutegemea mambo yako yawe hasi. Hautapungukiwa na kitu, ikiwa utakuwa na mategemeo chanya lakini yasitokee kwa asilimia kubwa kama ambavyo unataka, hautapungukiwa na kitu wala kula hasara.

Wewe weka mategemeo unayoyataka halafu endelea kuchapa kazi kisawasawa. Unapofanya kazi wakati una mategemeo chanya inakusaidia sana kuweza kuzifikia ndoto zako kuliko ungekuwa na mategemeo hasi.

Anza sasa kuweka mategemeo chanya kwenye kazi unayoifanya. Usiangalie kazi unaifanya ni kidogo au ni duni. Weka mategemeo chanya kwenye kazi hiyo kwa kuamini kabisa kwamba ina uwezo wa kukupa matokeo makubwa.

Hakuna kazi yenye ‘gerentii’ ambayo unaweza ukasema inaweza ikakupa mafanikio makubwa kama usipoweka juhudi na kufanya kwa ufanisi. Hata kazi hiyo uliyonayo, ifanye kwa usahihi na ukiwa na mategemeo bora na itakuletea mafanikio makubwa pia.

Ni wangapi ambao wanaonekana wanafanya kazi nzuri sana, lakini kutokana na mategemo yao kuwa hasi kazi hizo haziwapi mafanikio, na inabaki wengi kushangaa mbona yule kazi yake nzuri lakini hafanikiwi? Tatizo hapo ni mategemeo.

Ni wangapi ambao wanaonekana kazi zao ni duni, lakini watu hao unashangaa wamepiga hatua na kujiuliza mtu huyu vipi ameenda kutambika hadi akawa na mafanikio haya? Hakuna lolote hapo zaidi ya mategemeo bora kwenye maisha yao.

Ndio maana ili kupata mafanikio bora kwenye maisha yako, hutakiwi kukosea kwa kuendelea kujibebesha mategemeo hasi ambayo mategemeo hayo yanakurudisha sana nyuma pasipo hata wewe kutarajia.

Kuendelea kujibebebesha mategemeo hasi ni sawa na wewe kusema mimi mafanikio siyataki tena. Hutaweza kufanikiwa kama mtazamo wako uko hasi. Kazi peke yake haitoshi, unatakwa pia na kujenga na mtazamo chanya wa kukuvusha.

Zingatia mtazamo chanya, unakupa matokeo chanya kwenye maisha yako na mtazamo hasi unakupa pia matokeo hasi kwenye maisha yako. Uchaguzi ni wako kipi unataka, lakini ukumbuke ukikosea kwenye mtazamo maisha ya mafanikio sahau.

Fanyia kazi haya na chukua hatua kuhakikisha ndoto zako zinatumia.

Tunakutakia kila la kheri na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kujifunza maisha na mafanikio.

DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,

Ni wako rafiki katika mafanikio,

Imani Ngwangwalu,

Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,

Tovuti; www.amkamtanzania.com

Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,

Email; dirayamafanikio@gmail.com