Kuna watu wanaamini dunia ni sehemu ya mateso, sehemu ngumu na yenye kila aina ya shida. Na tangu wanapoamka mpaka wanaporudi kulala, hicho ndiyo wanachoona na kupata kwa siku nzima. Kwa mfano mtu anataka kuwahi mahali, halafu akakutana na foleni kubwa, au chombo alichokuwa anatumia kikaharibika. Hapa moja kwa moja mtu anaona ni ubaya wa dunia unamwandama.

Kuna watu ambao wanaamini dunia ni sehemu nzuri ya kuishi, sehemu yenye kila tunachotaka na tunaweza kupata chochote. Na tangu wanapoamka mpaka wanaporudi kulala, wanachoona ni fursa za uzuri wa dunia zikijionesha kwa njia mbalimbali. Kwa mfano mtu anayetaka kuwahi mahali, halafu akakutana na foleni kubwa, anajua hakuna namna zaidi ya kusubiri foleni hiyo iishe, na hivyo anatumia muda huo wa foleni kwa mambo mengine muhimu, kama kujisomea, au kutafakari mambo mengine.
Unaona hapo, mazingira yale yale, tukio lile lile, lakini mmoja anaona ni kitu kibaya kutokea kwake, huku mwingine akiona ni kitu bora kutokea kwake. Yupi anayefanikiwa zaidi? Jibu lipo wazi, anayeona mazuri.
SOMA; UKURASA WA 957; Ongea Unavyotaka, Lakini Watu Watasikia Wanachotaka Kusikia…
Sasa kitu kikubwa cha kujifunza hapa siyo nani anayefanikiwa au kushindwa, na wala siyo dunia kuwa nzuri au mbaya, bali dhana kwamba, nje pako vile vile, ila ndani ndiyo panapobadilika. Kwa dunia hii hii na maisha hayo hayo unayoishi, unaweza kuona mazuri au kuona mabaya.
Na kikubwa sana, ambacho unapaswa kuondoka nacho hapa ni hichi, unaweza kubadili mtazamo na fikra zako wakati wowote na kuzielekeza kwenye uzuri. Pale unapoanza kufikiria na kuona mabaya, jikamate kisha fikiria na ona mazuri. Jilazimishe kuangalia upande wa mazuri na kuchukua hatua nzuri, na hiyo itakuwezesha kuchukua hatua bora zaidi.
Mawazo na mtazamo ulionao siyo kitu ambacho umezaliwa nacho kama kilema fulani, bali ni kitu ambacho umejijengea, na hivyo una nafasi ya kujenga ambacho ni bora zaidi ya ulichonacho sasa.
Tengeneza na ishi mtazamo ambao utakupa hamasa ya kuwa bora zaidi, hamasa ya kuchukua hatua zaidi. Na usiogope kama utakuwa sahihi au la, kwa sababu kwa mtazamo wowote unaoweza kuwa nao kuhusu maisha na dunia kwa ujumla, siyo mtazamo pekee uliopo.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog
Asante coach kwa makala ya kurasa za maisha
Hakika n lazima tuwe na mtazamo tofauti tunapokabiliana na changamoto yoyote ile mbele yetu tusiangalie mazingira ya kitu chenyewe kilivyotokea tuone fursa
LikeLike
Karibu Hendry
LikeLike