Kuna wakati unataka kufanya kitu, lakini unakuwa umekwama, ukiwa hujui ufanyeje, au uanzie wapi, au panakuwa na changamoto ambazo hujui utawezaje kuzitatua.
Wengi hapa hujiambia haiwezekani na hawawezi kufanya, na kila kitu kinaishia hapo.
Ukweli ni kwamba, chochote ambacho unafikiria kufanya lakini hujui ufanyeje, mamilioni ya watu walishakifanya. Wapo watu waliokuwa wamekwama kama wewe, lakini wakatafuta njia na wakaweza kufanya.

Uzuri zaidi ni kwamba, hawakuishia tu kufanya, badala yake walielezea mchakato mzima wa jinsi walivyofanya. Walielezea mchakato huo kwenye kitabu, video, sauti au hata makala.
Hivyo basi, unachohitaji wewe, hasa pale unapokuwa umekwama ni kujiuliza nani mwingine ambaye ameshafanya hichi ninachokwama kufanya. Na hapo kuanza kutafuta maarifa sahihi ya jinsi ya kufanya.
SOMA; UKURASA WA 952; Jifunze Kwa Wengine, Lakini Usiige Maisha Yao…
Unapokwama popote, anza kwa kujiuliza nani ambaye alishafanya hicho ambacho wewe umekwama kufanya. Uzuri ni kwamba, ipo njia rahisi sana ya kutafuta ambayo ni mtandao wa intaneti.
Tafuta na utapata maarifa sahihi, wakati mwingine utahitajika kulipia gharama kupata maarifa hayo, kuwa tayari kufanya hivyo. Usikubali kukwama kufanya kitu kwa sababu huwezi, kushindwa wewe haimaanishi kila mtu ameshindwa. Wapo mamilioni ya watu wamefanya, jua wamefanyaje na wewe ufanye pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog