Kwa miaka mingi, serikali za mataifa mbalimbali zimekuwa zinaonekana kama ni adui wa watu. Inavyoonekana ni kama maisha ya watu yalikuwa na uhuru mkubwa kabla ya kuja kwa tawala za kiserikali.

Na changamoto kubwa inayoletwa na tawala za kiserikali ni kwenye usimamizi na utozaji wa kodi. Hizi ni kazi kubwa mbili za kila aina ya serikali, ambazo zimekuwa zikitengeneza changamoto kwa wananchi walio wengi.

Bila ya kusimamia watu wake vizuri, serikali yoyote ile haitaweza kudumu, kwa sababu itakuwa rahisi kwa machafuko kutokea na hata serikali kupinduliwa.

Pia bila ya kukusanya kodi, serikali haiwezi kujiendesha, kwa sababu serikali haina kazi au biashara ambayo inafanya kwamba inalipwa. Bali fedha za kuendesha serikali zinatoka kwenye kodi za wananchi.

Lakini pia serikali zina jukumu jingine kubwa ambalo ni kuhakikisha maisha ya wananchi wake yanakuwa bora. Na hapa serikali inawajibika kuhakikisha watu wana chakula cha kutosha, wanapata huduma za afya, elimu na miundombinu muhimu kama njia za usafiri, maji na makazi bora.

Katika kutekeleza majukumu yake, serikali nyingi zimekuwa zinajikuta kwenye upinzani na wananchi wake, hata kwa jambo ambalo ni jema kwa wananchi, mara nyingi wananchi hawaelewi na hivyo serikali kulazimika kutumia nguvu.

Mwandishi James Scott amefanya utafiti wa serikali mbalimbali na mipango waliyokuwa nayo ya kuyafanya maisha ya wananchi wake kuwa bora, lakini ikashindwa vibaya sana.

Katika utafiti wake huu, amejumuisha mipango ya makazi ya pamoja kama kwenye jiji la Brasilia nchini Brazil, mapinduzi ya kikomunisti nchini Urusi na hata mpango wa VIJIJI VYA UJAMAA nchini Tanzania. Katika yote haya, mwandishi ameonesha jinsi ambavyo nia ya serikali ilikuwa njema, lakini mipango hiyo ikashindwa vibaya kwa utekelezaji mbovu wa mipango hiyo.

seeing-like-a-state

Karibu sana tujifunze kwenye kitabu hichi cha SEEING LIKE A STATE na tuweze kuona kwa nini mipango mizuri ya serikali inaishia kuwa maumivu kwa wananchi na hata kushindwa vibaya.

SABABU NNE ZA KUSHINDWA KWA MIPANGO YA SERIKALI YA KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI WAKE.

Kila serikali duniani huwa na mipango mbalimbali ya kuboresha maisha ya wananchi wake. Iwe ni utoaji wa huduma bora za afya, elimu au mipango mikubwa ya kiuchumi kama mfumo wa ujamaa na ukomunisti. Mipango yote hii huwa ni kwa nia njema, ya kufanya maisha ya wananchi kuwa bora zaidi. Lakini mipango mingi huwa inashindwa, na kuna sababu nne zinazochangia kushindwa kwa mipango hii.

 1. Kutaka kurahisisha asili na jamii kwa ujumla.

Kuendesha nchi siyo kazi rahisi, kuweza kusimamia kila mwananchi, kujua kila ambacho mtu anafanya, na kuhakikisha watu wanafuta sheria siyo kazi rahisi. Hivyo kila serikali huwa inatafuta njia ya kurahisisha zoezi la kusimamia wananchi wake kwa umakini. Na hapa zipo njia mbalimbali kama kuwataka watu wakae eneo moja, watu kuzungumza lugha moja, watu kufanya kazi au kilimo cha aina moja na kadhalika. Njia hizi za kurahisisha usimamizi zimekuwa zinaenda kinyume na jinsi watu walivyokuwa wamezoea kuishi hapo awali na hii hupelekea mipango mingi kushindwa.

 1. Itikadi kali ya mabadiliko isiyotekelezeka.

Kuna mambo ambayo kwa kupanga ni rahisi sana, lakini utekelezaji wake ni mgumu. Baadhi ya mipango ya serikali, imekuwa mizuri katika kupanga, na kila kitu kinaonekana kinawezekana, lakini katika utekelezaji wake, ndipo ugumu na changamoto zinapoonekana. Viongozi wanakuwa wanaona ni rahisi kufikia yale maono yao, lakini hawaangalii hali ya wananchi na hata asili inavyoweza kuathiri mipango hiyo. Hii imekuwa inapelekea mipango mingi kushindwa kwa sababu kiuhalisia inakuwa haiwezekani. Kwa mfano wazo la vijiji vya ujamaa kwa Tanzania, kwa sehemu kubwa lilikuwa halitekelezeki kama lilivyopangwa, kwa sababu maeneo ambayo watu walikuwa wanapelekwa, hayakuwa na zile huduma muhimu ambazo watu waliahidiwa.

 1. Matumizi ya mabavu.

Pale ambapo serikali inashindwa kutekeleza mipango yake kwa hiari, basi kitu ambacho huwa kinafuata ni matumizi ya nguvu na mabavu. Wananchi wanaokataa kutekeleza mipango ya serikali wanalazimishwa kuifuata hata kama kwao haina manufaa. Tukirudi kwenye mfano wetu wa vijiji vya ujamaa, wale waliokataa kuondoka kwenye makazi yao na kwenda kwenye vijiji vya ujamaa, walilazimishwa kwa nguvu na hata nyumba zao kuchomwa moto. Matumizi ya mabavu yamekuwa yakifanya mipango mingi kushindwa haraka kuliko ingepewa muda zaidi.

 1. Jamii ambayo ni dhaifu, ambayo haiwezi kupinga.

Pale ambapo jamii ambayo inaletewa mipango na serikali ni dhaifu na haiwezi kupinga mipango ambayo haiwafai, imekuwa inachangia mipango hiyo kushindwa. Kwa sababu kwa nje jamii itaonekana kama inapokea, na hivyo viongozi kuona kwamba ni mafanikio. Kumbe kwa ndani watu wanapinga na hivyo mipango kushindwa.

Kwa mfano kwenye vijiji vya ujamaa, licha ya kwamba watu walilazimika kwenda kwenye vijiji hivyo, bado wengi hawakujitoa katika kazi za ujamaa, kitu kilichopelekea mpango wa kulima pamoja kwa ujamaa kushindwa.

NJIA NNE ZA SERIKALI KUWA NA UDHIBITI KWA WATU WAKE.

Ili serikali yoyote iwe salama, lazima iweze kuwa na udhibiti kwa watu wake, iweze kujua kila mtu ambaye yupo chini ya serikali na anafanya nini. Pia hii inarahisisha kujua watu wa nje na kuweza kuhakikisha watu wapo salama. Hili ni zoezi gumu kwa serikali yoyote, hasa serikali za zamani, kwa sababu watu walikuwa wanakaa sehemu mbalimbali na ni vigumu kuwajua.

Ili kurahisisha hili, serikali ziliweza kutumia njia nne muhimu.

 1. Mitaa iliyopangwa vizuri.

Kabla ya kuwepo kwa serikali za nchi, watu walikuwa wakiishi kwa makundi, kwenye nyumba ambazo zimejengwa bila ya utaratibu wa aina yoyote ile. Watu walioishi kwenye jamii fulani waliijua mitaa yao na hakukuwa na tatizo. Lakini serikali inayowaongoza, ambayo ipo nje ya jamii hiyo, ilikuwa vigumu kujua kila mtaa na watu wake. Hivyo kurahisisha hilo, serikali zilileta utaratibu wa kuwa na nyumba zilizojengwa vizuri kwenye mitaa iliyopangwa vizuri. Kwa njia hii inakuwa rahisi kwa maafisa wa serikali kufika kila mahali. Inarahisisha ukusanyaji wa kodi na hata udhibiti pale tatizo linapotokea.

 1. Majina ya ukoo.

Siku za nyuma kabisa, watu walikuwa wanakuwa na jina moja pekee, halafu wanakuwa na jina jingine la utani, ambalo liliendana na maumbo yao au hata kazi zao. Hii ilikuwa inatosha kwa sababu kwenye jamii ndogo, ni rahisi watu kujuana. Lakini serikali inapotaka kuwajua watu wake, kuwa na jina moja kama Amani mtoto wa John haitoshi, hivyo utaratibu wa majina ya ukoo ulianzishwa rasmi. Watu walipaswa kuwa na majina angalau matatu, ambayo yanaweza kuwatofautisha na watu wengine.

 1. Lugha moja.

Kila jamii ina lugha yake, ambayo iliwawezesha kuwasiliana vizuri na kuelewana kwenye shughuli zao na mahitaji yao pia. Lakini nje ya jamii hiyo, lugha ni vigumu kueleweka. Ni vigumu kwa serikali kuongoza watu kama haiwezi kuelewa watu hao wanazungumza nini na kama watu hao hawaelewi serikali inasema nini.

Hii ilifanya kila serikali kutafuta lugha moja ambayo itaweza kueleweka kwa wote na kuifanya hiyo kuwa lugha ya taifa. Hii ilirahisisha utawala na shughuli nyingine za kiserikali, kama utoaji wa elimu, huduma za afya na kadhalika.

 1. Kazi ya aina moja.

Kabla ya kuwepo kwa serikali moja inayounganisha jamii mbalimbali, watu walikuwa huru kufanya kila wanachojisikia kufanya. Na wengi walifanya ili kutimiza mahitaji yao binafsi kama kuwa salama na kupata chakula. Ili kuweza kuwasimamia watu vizuri, serikali zimeweza kutengeneza kazi rasmi za watu na hata kwenye kilimo basi kilimo rasmi. Kwa njia hii watu wanalazimika kufanya kazi ambazo zinakubalika, au kulima mazao ambayo yanakubalika. Hii inahakikisha watu wanapata mahitaji yao, na pia serikali inaweza kukusanya kodi.

KUSHINDWA KWA MAPINDUZI YA KIKOMUNISTI YA URUSI.

Lenin alikuwa kiongozi wa mapinduzi ya kikomunisti nchini  Urusi ya mwaka 1917. Lenin alikuwa na mipango mizuri ya kuhakikisha taifa la Urusi linakuwa lenye nguvu na wananchi wake wanakuwa na maisha bora. Aliona jinsi matumizi ya sayansi na teknolojia yanavyoweza kuboresha maisha ya wananchi wake. Lakini mapinduzi haya yalishindwa, na mpaka kufikia mwisho wa utawala wake, Lenin hakuwa ameona kile alichofikiri kingewezekana.

Zifuatazo ni sababu zilizopelekea mapinduzi ya kikomunisti kushindwa.

 1. Mipango isiyotekelezeka.

Kupitia maandiko yake na misimamo yake, Lenin alikuwa na mipango mingi ambayo kwenye makaratasi inaonekana ni rahisi, lakini utekelezaji wake ulikuwa mgumu kwa uhalisia. Mipango yake wa kila mwananchi wa kijijini kuwa na umeme, na kilimo kufanyika kwa mashine haikuwezekana kutokana na kukosekana kwa utayari wa watu na matumizi ya mabavu.

 1. Kutegemea kikundi kidogo cha watu kuendesha mapinduzi.

Katika mpango wake wa mapinduzi, Lenin alitegemea kikundi kidogo cha watu kuongoza kila kitu, huku kundi kubwa la watu likifuata na kuongozwa. Lenin aliamini ni rahisi kuwasimamia na kuwaongoza watu wachache kuchukua hatua kuliko watu wengi. Lakini kundi hili la watu halikuweza kuleta matokeo aliyotegemea.

 1. Upinzani kutoka kwenye vyama vya wafanyakazi.

Lenin alikuwa na mipango mizuri, lakini utekelezaji wake ulikuwa wa nguvu na mabavu. Mipango hii ilitekelezwa kidikteta kitu ambacho kilifanya wananchi wengi kuteseka na kuumia. Kutokana na hali hii, Lenin alipata upinzani mkali kutoka kwa vyama vya wafanyakazi na makundi mengine ya kijamii yaliyosababisha mipango mingi kutokukamilika.

 1. Kuondoa siasa na kuona kila mtu anaweza kuaminika.

Katika kutekeleza mipango ya mapinduzi, Lenin aliamini siasa ni kikwazo. Kama kila mtu ataweza kusema atakavyo na hata kuweza kupinga basi itachelewesha mambo kutokea. Pia aliamini kwamba kila mtu anaweza kuaminika, akapewa kazi ya uongozi na kuweza kuleta matokeo mazuri. Yote haya yalikuwa ni mawazo mazuri, lakini hayakuwa yanatekelezeka.

 1. Kuamini kwenye kilimo cha mashamba makubwa na kudharau kilimo cha wakulima wadogo wadogo.

Lenin aliamini kwamba, ili nchi iweze kuendelea, basi lazima iondokane na jembe la mkono na kulima kisasa, kuwa na mashamba makubwa ambayo yanaendesha kwa mbinu za kisasa. Lakini tafiti mbalimbali zilionesha kwamba, kilimo cha mashamba makubwa kilikuwa na gharama kubwa kuliko cha wakulima wadogo wadogo. Lenin hakukubaliana na tafiti hizo, aliendelea kusisitiza kilimo cha mashamba makubwa ambacho kilishindwa kuleta matokeo yaliyokuwa yanategemewa.

KUSHINDWA KWA VIJIJI VYA UJAMAA TANZANIA.

Moja ya mipango ya kitaifa ambayo ilikuwa na nia njema ya kuboresha maisha ya watu lakini ikashinda kufanya hivyo ni mpango wa Vijiji vya Ujamaa nchini Tanzania. Wakati wa kuitangaza sera ya UJAMAA NA KUJITEGEMEA mwaka 1967 Mwalimu J. K Nyerere alieleza dhumuni la serikali kuhakikisha maisha ya watu wote yanakuwa bora na siyo maisha ya wachache. Hivyo kuanzishwa kwa vijiji vya ujamaa kungewasaidia watu kupata huduma zote muhimu kwa pamoja, huku wakishirikiana katika uzalishaji. Pamoja na nia hii njema, wazo la vijiji vya ujamaa pamoja na sera ya ujamaa vilishindwa kuleta matokeo yaliyotegemewa. Na hapa ni baadhi ya mambo yaliyosababisha.

 1. Maagizo kutoka juu kwenda chini.

Pamoja na hii kuwa nia njema, mpango wa kuwahamisha wananchi kutoka kwenye makazi yao na kwenda kwenye vijiji vya ujamaa haukuwashirikisha wananchi. Bali wananchi walikuwa wakipokea maagizo kutoka kwa viongozi kwamba wanatakiwa kuondoka pale walipo na kwenda kwenye vijiji vilivyochaguliwa. Hili liliwafanya wananchi kupinga kutokana na kutoshirikisha na kujua umuhimu wa wao kufanya hivyo na hata kupendekeza njia bora zaidi.

 1. Matumizi ya nguvu.

Mwanzoni wakati wa mpango huu, Mwalimu Nyerere alisisitiza kwamba hili litakuwa zoezi la hiari. Akiamini kwamba, wale wachache ambao wataenda kwenye vijiji vya ujamaa, watapata huduma nzuri za afya, elimu, maji n.k. Wengine wakiona huduma hizo nzuri, basi na wao wataamua wenyewe kwenda kwenye vijiji hivyo.

Lakini hilo halikutokea, watu wengi hawakwenda kwenye vijiji vya ujamaa na hivyo ilibidi wapelekwe kwa nguvu. Akilihutubia bunge Mwalimu Nyerere alisema serikali inabidi ichukue jukumu la baba kuhakikisha watoto wanakuwa na hali nzuri.

 1. Viongozi kutekeleza maagizo ili kulinda kazi zao.

Kila mkoa na kila wilaya ilipewa idadi ya vijiji ambavyo inapaswa kutengeneza na kuhakikisha watu wote wanaenda kwenye vijiji hivyo. Ili kulinda kazi zao, maafisa wa serikali walilazimika kuhakikisha watu wanaenda kwenye vijiji hivyo ili kulinda kazi zao. Hii ilipelekea watu kupelekwa kwenye maeneo ambayo hayakuwa mazuri na hivyo maisha kuwa magumu kwao.

 1. Maeneo kutokutafitiwa na kuandaliwa vizuri.

Watu wengi waliondolewa kwenye maeneo ambayo tayari yana uzalishaji kwao na kuelekwa kwenye vijiji ambavyo ardhi haikuwa na uzalishaji, maji hayakupatikana kwa urahisi na maisha kuwa magumu pia. Hili lilipelekea maisha kuwa magumu na tatizo la njaa kuwa kubwa kitu ambacho kiliigharimu serikali kuwapatia vyakula.

 1. Kulazimisha watu kulima mazao ya aina moja na kwa ujamaa.

Moja ya mipango kwenye vijiji vya ujamaa ilikuwa ni eneo liwe na zao moja linalimwa na lilimwe kwa ujamaa. Hivyo kulikuwa na shamba moja la kijiji kizima ambapo kila familia ilipangiwa eneo la kulima. Baadhi ya mazao yaliyochaguliwa hayakuwa yakiendana na mazingira na pia hayakuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi. Changamoto nyingine ilikuwa kulima kwa ujamaa ambapo baadhi ya watu hawakujitoa kama ambavyo walikuwa akijitoa kwenye kazi zao binafsi.

MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA ILI MIPANGO YA SERIKALI IWEZE KUTIMIA.

Kila serikali lazima iwe na mipango ya kuhakikisha maisha ya wananchi wake yanakuwa bora zaidi. Ni kwa maisha ya wananchi kuwa bora ndipo serikali inakusanya mapato mengi, inapata wafanyakazi na hata viongozi bora pia. Ili kuhakikisha mipango hii ya serikali inatimia, mambo yafuatayo ni muhimu yazingatiwe.

 1. Wananchi washirikishwe katika kufikia mipango hiyo.

Serikali kuamini kwamba yenyewe ndiyo inajua kile kilicho bora kwa wananchi na wananchi wanapaswa kupokea tu mipango wanayoletewa ni kujiandaa kushindwa. Mipango yoyote ya kuboresha hali ya wananchi, lazima wananchi washirikishwe katika kufikia maamuzi ya mipango hiyo. Hivyo kupokea maoni ya wananchi kwenye faida na haya utekelezaji wa mipango mbalimbali, inawasukuma wananchi kuitekeleza, kwa sababu wanaona ni kitu ambacho wamechagua wao wenyewe.

 1. Muda unahitajika.

Mipango ya kuboresha maisha ya wananchi inakuja na mabadiliko na mabadiliko yoyote yanahitaji muda. Hivyo kama serikali inataka mipango itimie, lazima iwe na muda na subira pia. Kulazimisha mambo yatokee haraka huja na madhara ya mipango kushindwa. Lakini kama kutakuwa na muda wa kutosha, wananchi wataelewa na kuweza kuchukua hatua za mabadiliko.

 1. Kuruhusu demokrasia.

Sababu kubwa ya kushindwa kwa mipango ya serikali nyingi, imekuwa kukosekana kwa demokrasia. Hasa pale serikali inapoona inaweza kutumia nguvu kuleta mabadiliko yoyote. Watu wanaweza kushindwa kwa nguvu hizo, lakini kwa ndani wakawa na upinzani utakaopelekea mipango kushindwa.

Serikali zimekuwa zinakutana na changamoto mbalimbali katika kuwaongoza na hata kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora. lakini changamoto hizi zinaweza kutatuliwa na maisha ya watu yakawa bora kama misingi ya utawala bora itafuatwa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz