Binadamu huwa tunapenda kuwepo na usawa kwenye mambo ambayo tunafanya. Iwe ni mahusiano tunayokuwa nayo na wengine, au makubaliano ambayo tunafanya, huwa tunategemea kuwepo na usawa. Kwamba juhudi ambazo kila mtu anaweka na matokeo ambayo yanapatikana yawe sawa kwa wote wanaohusika.

Lakini sivyo uhalisia ulivyo. Kwenye mambo mengi yanayohusisha zaidi ya mtu mmoja, japo kwa nje yanaonekana kuwa na usawa, kwa ndani kuna hali ya kutokuwa na usawa ambayo imejificha. Kwenye mahusiano na makubaliano mengi, wapo ambao faida ikipatikana wananufaika, lakini hasara ikipatikana haiwagusi wao.

Hali hii ya kukosekana kwa usawa ambako kumejificha, ndiyo imekuwa inamfanya mwandishi Nassim Nicholas Taleb kuchunguza kila aina ya mahusiano na makubaliano na kuona ni kwa kiasi gani hali ya kutokuwa na usawa inatumiwa.

Katika vitabu vyake vingi, Nassim amekuwa akiangalia kule ambapo wengi hawaangalii. Amekuwa akionesha jinsi ambavyo watu wanajidanganya wanajua kumbe hawajui, jinsi ambavyo wachache wanaonufaika wanawanyonya wengi wasionufaika.

Katika kitabu chake cha SKIN IN THE GAME, anafanya kazi kubwa ya kuonesha mahusiano na makubaliano kwenye kila eneo la maisha yetu, jinsi ambavyo kuna hali ya kutokuwa na usawa imejificha ndani yake.

skin in the game

SKIN IN THE GAME ni kitabu kinachojadili mada kuu nne kwa pamoja;

MOJA; kukosekana uhakika na kutokutegemeka kwa elimu, elimu ya vitendo na hata elimu ya kisayansi. Hapa mtu anahitaji kujua kuhusu elimu ya nadharia na elimu ya vitendo. Kwamba vile ambavyo wengi wanajifunza kwa nadharia, huwa haviwezekani kwa vitendo. Na wale ambao wamebobea kwenye elimu ya nadharia (wanataaluma) huwa ni wabovu kwenye maisha ya kawaida.

MBILI; usawa kwenye mambo yanayohusu watu, yaani haki, wajibu na ulinganifu kwenye majukumu na matokeo. Usawa unahitajika kwenye kila aina ya mahusiano na makubaliano, kwamba kama mtu ananufaika faida ikipatikana, basi hasara inapopatikana imhusu pia.

TATU; ushirikishwaji wa maarifa na taarifa katika miamala. Kwenye miamala mbalimbali ya kibiashara inayofanyika, upande mmoja unaweza kuwa na taarifa nyingi kuliko upande mwingine, je ni taarifa kiasi gani zinapaswa kushirikishwa kwenye miamala ya kibiashara?

NNE; mantiki kwenye mifumo migumu na dunia halisia. Mantiki kwenye maisha siyo kile ambacho watu wanaelewa na kuandika, bali ni kile ambacho kinafanya maisha yaendelee kuwepo hapa duniani. Kuna vitu watu huwa hawavielewi, lakini ndiyo vitu vinafanya maisha yaende.

KITABU CHA KWANZA; HUWEZI KUKIMBIA ASILI YA KITU.

 1. Huwezi kuielewa dunia bila uhalisia.

Kuielewa dunia, tunahitaji kuwa na uhalisia na kile kinachoendelea. Hii ndiyo Taleb anaita SKIN IN THE GAME, kuwa kwenye eneo husika na kulipa gharama halisi ya kile unachotaka kuelewa. Tangu enzi za zamani imekuwa ikijulikana kwamba watu hujifunza kupitia maumivu, yale tunayojifunza kwa kujaribu na kushindwa, ndiyo tunayoyaelewa zaidi kuliko yale tunayojifunza darasani kwa nadharia.

 1. Kama hasara haikugusi basi hupaswi kunufaika na faida.

Mahusiano na makubaliano mengi baina ya watu yapo kwenye hali kwamba inapopatikana faida basi pande zote zinanufaika, lakini ikipatikana hasara upande mmoja hauhusiki kabisa na hasara hiyo.

Tangu enzi za zamani, watawala na wababe wa kivita, walikuwa wakishiriki wenyewe kwenye vita. Kwenye historia ya Roma, watawala wake wengi walifia kwenye vita. Tawala zilikuwa zinaongozwa na watu wanaochukua hatari kwenye mikono yao.

Lakini kwa zama tunazoishi, tawala zimekuwa zinaongozwa na watu wanaohamisha hatari kutoka kwao kwenda kwa wananchi. Viongozi wa nchi watakubaliana kuingia kwenye vita, lakini wao hawatakuwa popote pale karibu na vita, ila watakaoumia ni wananchi.

 1. Kama usawa hautatengenezwa, mfumo utatengeneza usawa wenyewe.

Taleb anatuambia kila mfumo una njia ya kujitengenezea usawa wake wenyewe. Watu wanaweza kutengeneza njia isiyo ya usawa ua kujinufaisha, lakini haitadumu, mfumo utashindwa na utajirudisha kwenye usawa wenyewe. Kwa mfano anguko la uchumi la mwaka 2008, lilitokana na ukosefu wa usawa kwenye mfumo wa fedha, ambapo mabenki yalikuwa yakinufaika huku wananchi wa kawaida wakibeba hasara inayopatikana.

 1. Kanuni ya fedha inayoshinda kanuni ya dhahabu.

Kwa kipindi kirefu, kanuni ya dhahabu imekuwa inaonekana ndiyo kanuni bora kabisa katika kuongoza mahusiano na ushirikiano wa watu. Kanuni hii inasema wafanyie wengine vile ambavyo ungependa wakufanyie wewe. Ni kanuni ambayo inatengeneza usawa kwenye matendo baina ya watu.

Lakini ipo kanuni ya fedha, kanuni ambayo inaonekana kutengeneza vizuri usawa kuliko kanuni ya dhahabu. Kanuni ya fedha inasema; usiwafanyie wengine kile ambacho usingependa wao wakufanyie. Kanuni hii ya fedha, ni upande hasi wa kanuni ya dhahabu, lakini inafanya kazi vizuri zaidi kuliko kanuni ya dhahabu kwa sababu hasi inafanya kazi ya kuondoa.

 1. Mara nyingi mambo hutokea yenyewe na si kwa sababu yamepangiliwa.

Mambo mengi ambayo yanatokea kwenye maisha ya watu, hutokea yenyewe au kwa bahati tu. Lakini watu huwa hawajui hilo, hivyo huona yametokea kutokana na juhudi zao, na hivyo kujiona wameshajua siri ya kufanya mambo yatokee. Hapo ndipo wanapoweka rasilimali zao nyingi zaidi kwenye kitu na wasipate matokeo kama waliyopata awali.

Taleb anasema watu wamekuwa wamepumbazwa na matokeo ambayo hayana uhusiano na juhudi walizoweka.

 1. Watu wanaotaka kunufaika dhidi ya wengine hufanya mambo kuonekana magumu.

Watu wanapotaka kunufaika dhidi ya wengine, pale wanapotaka kutengeneza mfumo ambao unawanufaisha wao na kuwanyonya wengine, hufanya mambo ambayo hata ni rahisi kabisa kuonekana magumu. Kila kitu kinaweza kurahisishwa kwa namna ambayo kila mtu anaelewa. Ukiona mtu anafanya mambo yaonekane magumu kuliko yalivyo, jua hapo kuna dalili za kuumizwa.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Evolutionary Enlightment (Njia Mpya Ya Uamsho Wa Kiroho).

KITABU CHA PILI; MTAZAMO WA KWANZA KWA MAWAKALA.

Wapo mawakala wengi ambao wananufaika na mahusiano waliyonayo na wengine, ambapo faida ikipatikana wananufaika, ila hasara haiwaumizi wao. Kwenye kitabu cha kwanza tunakwenda kuona jinsi hali ya kukosekana kwa usawa inavyotengenezwa baina ya makubaliano na mahusiano ya watu.

 1. Kila mtu anapaswa kula kile anachotengeneza au kuongelea.

Kuwa makini sana na ushauri unaopokea kwa watu, ambapo matokeo ya ushauri huo hayatawahusu wao. Chochote kile ambacho mtu anakushauri kufanya, hakikisha kwanza na yeye anafanya au matokeo yakija vibaya basi na yeye atahusika.

Wafanyabiashara wengi hupenda kuwahadaa watu na kuwauzia vitu, wakiwaaminisha kwamba ni muhimu kwao, wakati hata wao wenyewe wanajua siyo muhimu.

Hivyo kwenye miamala, baina ya muuzaji na mnunuaji, taarifa zote zinazohusiana na muamala huo zinapaswa kujulikana baina ya pande hizo mbili. Kama upande mmoja utaficha taarifa fulani, ambayo kama upande wa pili ungeijua usingefanya maamuzi ya kununua, ni kinyume na kanuni za maadili.

 1. Ushirikiano wa kikundi unategemea na idadi na ukubwa.

Kumekuwa na ndoto za kuifanya dunia kuishi kijamaa, ambapo watu wanashirikiana kwa pamoja, wanagawana majukumu na kuhusika na matokeo kwa usawa. Kwa mfano pale kijiji kinapokubaliana watu wasivue samaki ambao ni wadogo, au kukata miti kwenye vyanzo vya maji, yote hayo ni mambo muhimu kwa manufaa ya wote.

Hilo linaweza kufanya kazi pale idadi ya watu inapokuwa ndogo na eneo kuwa dogo. Lakini idadi ya watu inapokuwa kubwa na eneo kuwa kubwa, inakuwa vigumu kufuata utaratibu huo, kwa sababu watu wanaanza kuvunja taratibu wakiamini hata wengine wanavunja bila ya kuonekana.

Hivyo ushirikiano baina ya kikundi, unaweza kuwa wa usawa pale idadi inapokuwa ndogo, idadi ikiwa kubwa hali ya kutokuwa na usawa inajitengeneza yenyewe.

 1. Sheria nyingi zinazowekwa kulazimisha usawa, zinaharibu usawa.

Kutokana na hali ya kukosekana kwa usawa kuwa hatari kwa wengine, mamlaka zimekuwa zinaweka sheria mbalimbali za kulazimisha usawa baina ya watu. Lakini sheria hizi zimekuwa zinaharibu zaidi usawa kuliko kutengeneza usawa. Hii ni kwa sababu kitu kikishakuwa sheria, basi kunakuwa na mianya kwenye sheria hiyo ambayo watu wanaweza kuitumia kujinufaisha zaidi.

Hivyo njia pekee ya kufanya mahusiano ya watu kuwa na usawa siyo kwa sheria, bali kuimarisha maadili. Mtu afanye kitu siyo kwa sababu sheria inamlazimisha, bali kanuni za maadili zinamwongoza. Na sheria huja na kuondoka, lakini kanuni za maadili zinadumu mara zote.

KITABU CHA TATU; HALI KUU YA KUKOSEKANA KWA USAWA.

 1. Jamii inaendeshwa na kikundi kidogo cha watu.

Mabadiliko yoyote makubwa kwenye jamii na hata duniani kwa ujumla, yanaanzishwa na kuchochewa na kikundi kidogo cha watu. Ila kikundi hicho kinakuwa na msimamo mkali sana kwenye kile wanachosimamia.

Kwenye kila jambo hapa duniani, kuanzia imani, mpaka maisha ya watu, wapo wachache ambao wapo pande za mwisho, wachache ambao wanakubaliana nacho sana na wachache ambao wanapingana nacho sasa. Ila wapo wengi ambao wapo katikati, kwao kila kitu ni sawa, hawakubaliani wala hawapingi.

Wanaoleta mabadiliko kwenye jamii, wanaoiendesha jamii bila hata ya kujijua, ni wale ambao wana msimamo mkali.

Kwa mfano Waislamu huwa wanakula nyama ambayo ni Halal, na wana msimamo kwenye hilo. Sasa ili waandaaji na wauzaji wa nyama wasipate shida, inabidi nyama wanayoandaa na kuuza iwe Halal, hata kama eneo wanalouza nyama zao lina Waislamu wachache sana. Hivi ndivyo ilivyo kwenye mambo mengi, pale wachache wanapokuwa na msimamo fulani, taratibu nyingi zinaegemea upande wao.

 1. Mapinduzi yanaongozwa na kikundi kidogo cha watu.

Mapinduzi yoyote yale yanayotokea kwenye jamii, yanaongozwa na kikundi kidogo sana cha watu, ambao wamejitoa kweli kusimamia kile wanachoamini. Na siyo kutoka kwenye kundi kubwa la watu ambao muda wowote wanaweza kubadili mawazo yao.

Na hata maendeleo yanayotokea kwenye jamii, yanaongozwa na kikundi kidogo cha watu, ambao wanajua nini wanataka na hawakubali kuzuiliwa na chochote kupata kile wanachotaka.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Seeing Like A State (Jinsi Mipango Ya Kitaifa Ya Kuboresha Maisha Ya Watu Ilivyoshindwa Vibaya).

KITABU CHA NNE; MBWA MWITU BAINA YA MBWA.

 1. Jinsi ya kummiliki mtu mwingine kisheria.

Watu wanaoendesha taasisi mbalimbali wanajua kitu kimoja muhimu sana, kama unataka kuendesha taasisi vizuri, basi unahitaji wale waliopo chini ya taasisi hiyo wasiwe na uhuru usio na mipaka. Watu wakishakuwa na uhuru wa kuweza kufanya chochote wanachotaka, inakuwa vigumu kufanya kile wanachopangiwa kufanywa na hivyo taasisi haiwezi kupiga hatua.

Hii ndiyo sababu kuna mpango wa ajira, ambao kusudi lake kubwa ni kutengeneza watu ambao wataendesha maisha yao kuwategemea wale waliowaajiri. Iwapo mtu atakuwa huru kufanya chochote anachotaka, basi hatakubali kufanyishwa kazi na mtu mwingine.

Hivyo kitu cha mwisho ambacho mwajiri yeyote anataka kitokee, ni waajiriwa wake kua huru, hasa kifedha. Kwa sababu hawatakubali kuajiriwa tena. Ndiyo maana mifumo ya ajira imetengenezwa kwa njia isiyo ya usawa, ili waajiriwa wamtegemee zaidi mwajiri na wawe watiifu kwake.

 1. Umiliki wa watumwa kupitia makampuni.

Utumwa bado upo na kwa zama hizi ni utumwa unaokubalika kisheria. Kwa mfano makampuni mengi makubwa, huwa yana njia ya kutengeneza watumwa, kuwa na wafanyakazi ambao watakuwa watiifu kwa kampuni hiyo hata iweje. Makampuni hayo yanachofanya, ni kumlipa mfanyakazi kiasi kikubwa cha fedha, ambacho hata yeye mwenyewe anajua ni kikubwa na hawezi kupata popote, halafu inampa nyumba, usafiri na zawadi nyingine. Kwa njia hii, mtu hawezi kuthubutu kwenda kinyume na matakwa ya kampuni, hata kama inakosea. Anakuwa ni mtumwa ambaye amekubali utumwa wake kwa maisha yake yote.

 1. Uhuru haujawahi kuwa bure.

Dhana ya uhuru ni dhana ngumu, ambayo wengi hawaielewi. Hakuna uhuru wa bure, na uhuru kamili ni kitu kigumu sana kufikia. Ipo hadithi ya mbwa na mbwa mwitu, walikutana na mbwa akawa anamhadithia mbwa mwitu jinsi maisha yake yalivyo mazuri, anapewa chakula, na kulala sehemu nzuri, mbwa mwitu akamuuliza mbwa, na huo mkanda uliofungwa shingoni ni wa kazi gani? Alipoelewa matumizi yake, mbwa mwitu alimwambia mbwa kwa yote mazuri uliyoniambia, sitaki hata moja kama nitaishia kufungwa mkanda shingoni, akakimbia na mpaka sasa anakimbia.

Kila aina ya uhuru unaotafuta kwenye maisha, ipo gharama ambayo utapaswa kulipa ili kupata uhuru huo. Hakuna uhuru wa bure, na kadiri unavyotaka uhuru mkubwa, ndiyo unahitajika kulipa gharama kubwa.

 1. Njia nyingine zinazotumika kuwaweka watu kwenye utumwa.

Tumeona jinsi ambavyo ajira na makubaliano mbalimbali yanavyowaweka watu kwenye utumwa. Lakini siyo hayo tu, zipo njia nyingi ambazo zinawafanya watu kuendelea kukaa kwenye utumwa, na njia kubwa kuliko zote ni familia. Kuwa na familia, watu wanaokutegemea kunaweza kutumika kama njia ya kukuweka kwenye utumwa. Mfano kama wewe umechagua kuwa huru na kutokufuata vitu fulani ambavyo watu wanataka ufuate, wanaweza kutumia familia yako kukufanya wewe ufuate.

Tumekuwa tunaona jinsi ndugu wa familia wanavyoweza kuteseka na hata kuteswa kwa sababu mtu wa familia hiyo ameenda kinyume na matakwa ya watu fulani. Ni kwa sababu hii, watu wengi ambao walikuwa wanajitoa kupigania uhuru wa wengine, hawakuwa na familia, hawakuwa na watoto wanaowategemea wala kuwa na wake au waume. Walikuwa wanakwepa kuziweka familia zao kwenye hatari inayotokana na uhuru wao.

KITABU CHA TANO; KUWA HAI INAMAANISHA KUCHUKUA HATARI FULANI.

Maisha ni hatari, kila tunachofanya kwenye maisha kina hatari fulani, hivyo kuwa hai, ni kiashiria kwamba kuna hatari umeshachukua na unaendelea kuchukua.

 1. Makovu yanaonesha umejitoa.

Watu waliokosea na ambao makosa yao yapo wazi wanakubalika kwa wengine kuliko wale ambao wanaonekana hawana makosa kabisa. Hii ni kwa sababu makosa yanaonesha kwamba mtu aliyekosea ni mtu wa kujaribu, ni mtu wa kufanya na siyo wa kuigiza.

Hili linaweza kuwa moja ya mambo yaliyochangia Donald Trump kushinda uraisi wa marekani licha ya wapinzani wake kuonesha madhaifu yao yake mengi mno ukilinganisha na washindani wenzake. Kitendo cha wao kuonesha madhaifu yake, kiliwafanya watu kuona huyo ndiye mtu anayewafaa, kwa sababu ni mtu halisi na siyo mtu wa kuigiza.

 1. Wasomi lakini wajinga.

Mwandishi Taleb anasema matatizo mengi ya dunia yanatengenezwa na kikundi kidogo cha watu ambao ni wasomi lakini wajinga (INTELLECTUAL YET IDIOT – IYI). Hawa ni watu ambao wanayo elimu kubwa sana ya nadharia, lakini hawana elimu ya vitendo, hawana uelewa kamili wa kile kinachoendelea kwenye maisha ya uhalisia.

Hawa ndiyo hubishana kuhusu sera na mipango mikubwa ambayo mataifa yanapaswa kuchukua, huku mahitaji ya kawaida ya watu ni kuweza kula, kulala na kufanya yale ya muhimu kwao.

Hawa ndiyo wanaojadili faida na umuhimu wa vita, huku wakiwa hawafiki hata eneo ambalo vita inapiganwa.

Mwandishi anatuambia hawa ndiyo watu wanaotengeneza hali ya kutokuwa na usawa kwenye maisha ya kila siku, kwa sababu hawana uhalisia wa yale wanayopinga au kuunga mkono.

 1. Nani mtaalamu wa kweli?

Muda ndiyo mwalimu wa kweli, kwa sababu kupitia muda ndiyo tunajua kipi ni kweli na kipi kinalazimishwa kuwa kweli. Kuna njia mbili za jinsi vitu vinakwenda na muda. Njia ya kwanza ni kuzeeka na kuharibika kwa vitu kutokana na muda unavyokwenda, yaani muda wa kitu kuendelea kuwepo unakuwa umeisha. Njia ya pili ni kasi ya ajali na hatari zinazoweza kukabili kitu na kikafika mwisho wake.

Ukweli umekuwa unadumu kadiri muda unavyokwenda. Hii ikiwa na maana kwamba, kama kitu kimedumu muda mrefu, basi ni kweli au ni kitu sahihi. Kwa sababu kama kisingekuwa sahihi, basi muda usingekiacha.

Alfonso X wa Spain alikuwa akiishi kwa msimamo huu; unguza magogo ya zamani, kunywa mvinyo wa zamani, soma vitabu vya zamani na tunza marafiki wa zamani. Vitu ambavyo vimedumu kwa muda ni sahihi kuliko ambavyo havijadumu kwa muda.

 1. Ushauri wa bibi dhidi ya ushauri wa watafiti.

Kama ukisikiliza ushauri a bibi yako ambaye ameishi kwa miaka mingi, atakuwa sahihi kwa asilimia 90 na kama utasikiliza ushauri wa watafiti utakuwa sahihi kwa asilimia 10.

Hii ni kwa sababu bibi yako atakuambia vitu ambavyo ameviona vikijirudia mara kwa mara kwa muda mrefu, ambavyo ameona kwa uhalisia, wakati watafiti watakuambia vile ambavyo wamejaribu na kuona vinafanya kazi. Na mara nyingi, vitu watu wanasema, hasa kwenye tafiti, ni tofauti kabisa na wanavyofanya.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; TAO TE CHING (Falsafa Ya Uchina Ya Kukuwezesha Kuwa Na Maisha Bora Na Yenye Mafanikio).

KITABU CHA SITA; MTAZAMO WA NDANI WA WAKALA.

Tunapoingia ndani zaidi na kuangalia wakala wa hali ya kutokuwa na usawa kwenye makubaliano na mahusiano mbalimbali, tunakuja kuona kwamba mwonekano wa nje hauendani kabisa na yaliyopo ndani. Kwamba vitu vingi kwa nje vimekuwa vinawekwa kwa njia ya kushawishi watu waamini ni vitu halisi, wakati ndani siyo vitu halisi.

 1. Kuwa makini na mwonekano wa nje.

Vitu vingi ambavyo kwa nje vimetengenezwa kuwa na mwonekano fulani, ndani ni tofauti. Na mara nyingi mwonekano wa nje hutengenezwa makusudi ili kuwapumbaza watu wachukue hatua fulani ambazo siyo sahihi kwao.

Kwa mfano wapo watu ambao kwa nje wanaonekana ni matajiri, kwa kuvaa na kutumia vitu vya gharama kubwa, lakini kwa ndani hawana utajiri unaoendana na kile wanachoonesha nje. Kile wanachoonesha nje ni njia ya kuwarubuni wengine kuchukua hatua fulani.

 1. Matajiri ni rahisi kurubuniwa kuliko masikini.

Njia nyingi za kuwarubuni watu fedha zao, huwa zinawalenga matajiri kuliko masikini. Hii ni kwa sababu wengi wanapokuwa matajiri, huwa wanaacha kujiangalia zaidi wao na kuanza kuwaangalia wengine wanawachukuliaje. Hivyo hujikuta wanaenda maeneo ambayo matajiri wengine wanaenda, ambayo gharama zake huwa ni kubwa hata kama wanachopata siyo bora.

Matajiri pia wanajikuta hawawezi kufanya chochote bila ya kupata ushauri wa wataalamu na washauri, hivyo unakuta wana washauri wa fedha, washauri wa vyakula, washauri wa mazoezi, mpaka washauri wa kulala. Yote hayo ni kufanya maisha yaonekane magumu kuliko yalivyo, na watu wamejipanga kuwanyonya matajiri kwa njia hizo zisizo sahihi.

Ukiwa tajiri, wala usitake kuonekana kwa nje, badala yake endelea kufurahia yale maisha uliyokuwa nayo kabla hata hujawa tajiri, utajiepusha na watu wengi ambao kazi zao ni kurubuni matajiri.

 1. Kama unataka kuimarisha urafiki, ficha vya ziada ulivyonavyo.

Hebu fikiria una rafiki yako, ambaye kila mkikutana yeye anachoongelea ni fedha kiasi gani anazo, amepata au amepoteza. Na ukiangalia fedha anazozungumzia ni fedha ambazo hujawahi kuota hata kuwa nazo. Au mkikutana anajadili mambo ya elimu kubwa, ambapo wewe huna elimu kubwa kama yeye. Je utapenda kukutana na rafiki wa aina hiyo mara kwa mara?

Katika mahusiano ya urafiki na mahusiano mengine, unahitaji kuficha vingi ambavyo unavyo, ili kuweza kuwa sawa na wengine. Kama utatumia muda mwingi kueleza kwa nini wewe ni bora zaidi, hutaweza kuwa na marafiki.

Sababu nyingine kubwa kwa nini kama una elimu kubwa au fedha nyingi inapaswa kuwa siri yako mwenyewe na mwingine yeyote asijue, kwa sababu kadiri wengi wanavyojua kila ulichonacho, ndivyo unatengeneza watu wengi wa kukurubuni na hata maadui pia.

 1. Matendo kabla ya maneno.

Adui mzuri ni yule ambaye unamiliki. Tangu enzi na enzi, panapokuwa na hali ya kutokuelewana baina ya pande mbili, maneno yamekuwa hayasaidii watu kukubaliana kwenda kwa hali gani, bali matendo. Kwa mfano kiongozi fulani amekosana na kikundi cha watu, kisha akaamka asubuhi na kukuta upanga umechomekwa pembeni ya godoro lake, wenye ujumbe ni sisi tunakuonya tu kwamba kama hutafanya tunavyosema tunaweza kuondoa maisha yako, atasikiliza kuliko kuambiwa kwa maneno tu, vitendo vinadhihirisha.

Japo zama hizi ubabe wa aina hiyo umeondoka, umekuja ubabe mpya wa vitendo ambao ni picha. Watu wamekuwa wanawapiga watu picha kwenye maeneo fulani ya kudhalilisha, kisha wanawalazimisha wafanye kile wanachotaka wao, na kama watakataa basi wataweka picha zao mtandaoni. Njia hii imetengeneza watumwa wengi mno, na imepelekea hata wengine kuondoa maisha yao.

 1. Uhalisia ni ukweli, habari ni feki.

Ukweli na habari ni vitu ambavyo haviendi kwa pamoja, kama unatafuta ukweli, sehemu ya mwisho kabisa kuupata ni kwenye habari. Waandishi wa habari wamekuwa wakilaumiwa kwa kuandika habari ambazo siyo kweli au zimewekwa chumvi sana, lakini kwa sehemu lawama hizi hawastahili.

Waandishi wa habari nao wana maisha, na habari zinazopendwa ni zile ambazo ni hasi au mbaya. Hivyo kama vyombo vya habari vitaripoti mazuri tu, watu hawatakuwa na hamasa ya kununua au kuangalia.

Kwa upande mwingine, waandishi wa habari wanahukumiwa na waandishi wenzao, hivyo mwandishi anapokwenda kinyume na wenzake, ni rahisi kutengwa. Hii ndiyo sababu makampuni makubwa yanaweza kuteka vyombo vya habari na habari mbaya kuhusu wao zisiandikwe bali habari nzuri tu.

Uhuru wa waandishi wa habari ni mdogo sana.

 1. Chukua hatari.

Njia pekee ya kuiokoa dunia, njia pekee ya kuisaidia dunia ni kuchukua hatari, kuweka maisha yako hatarini kwa kuanzisha kitu ambacho huna uhakika nacho, lakini kikifanikiwa kinawasaidia wengine. Hivyo kuwa mjasiriamali na kuanzisha biashara ndiyo njia bora kabisa ya kuchukua hatari ambayo itaiwezesha dunia kuwa sehemu bora ya kuishi.

Rafiki, kuna vitabu viwili vimebaki kwenye kitabu hichi, ambavyo sijavigusia hapa kwenye uchambuzi huu, vitabu hivyo ni HALI YA KUTOKUWA NA USAWA KWENYE DINI NA IMANI na HATARI NA UHALISIA. Hivi ni vitabu viwili vya mwisho kwenye kitabu hichi cha SKIN IN THE GAME, ambavyo vinaonesha kukosekana kwa usawa kwenye dini na imani, na pia kutuonesha uhalisia uliopo kwenye kuchukua hatua.

Nakuachia vitabu hivi viwili ujisomee mwenyewe kwa kutafuta na kusoma kitabu hichi.

Kwa kumaliza uchambuzi huu niseme mambo mengi tunayofikiri yana usawa, hayana usawa, kuna watu wametengeneza hali zisizo na usawa ambazo zinawanufaisha wao zaidi. Hivyo unahitaji kuwa makini na kila unachofanya.

Pia muhimu zaidi, kama unataka mafanikio kwenye chochote unachotaka, kuwa tayari kulipa gharama, kuwa tayari kuchukua hatua ambazo ni hatari.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji