Kabla ya kuingia katika maisha ya ndoa, wale walengwa wanakuwa na mitazamo yao tofauti waliyojijengea lakini wanakuwa na picha fulani ya matokeo watakayoyapata baada ya kuingia kwenye maisha ya ndoa. Hivyo, mambo huwa ndivyo sivyo pale watu wanapokutana na mambo tofauti na kile walichotarajia kukikuta.

Kabla ya kuingia katika wito wowote kaa chini na tafakari mwenyewe unafaa kuingia katika maisha gani, kwa sababu siyo kila mtu ameitwa kuwa mwanandoa kuna aina nyingi za maisha ambayo unaweza kujichagulia kuishi. Kabla ya kuingia katika wito au maisha ya ndoa jichunguze kwanza je una fiti katika maisha ya ndoa kwa sababu wewe mwenye unajijua.

Rafiki, usiingie katika mahusiano ya ndoa kwa hisia, ingia katika maisha ya ndoa kwa kuongozwa na akili na ishi na mtu mwenye akili yaani mtu sahihi ndiyo utaweza kufurahia maisha ya ndoa.

4d1bd-maadui2bwa2bmahusiano

Ndugu mmoja alikuwa anashirikisha hadithi zake za mambo ya ndoa yake kwa rafiki yake. Ndugu alikuwa anamwambia rafiki yeye hawezi kukaa na mwezi wake wa ndoa chini hata dakika 30 wakiwa wanaongea. Rafiki akamuuliza kwanini huwezi kukaa na mwezi wako? Ndugu akamjibu wakikaa na mwezi wake huwa lazima wataishia kugombana hivyo kuepuka hili anaamua kumkwepa tu. Akiwa sebuleni yeye anaenda chumbani, au jikoni kujishughulisha na kazi ili mradi tu asipate muda wa kuongea naye.

SOMA; Hizi Ndizo Hazina Saba (07) Muhimu Katika Maisha Ya Ndoa.

Ndugu msomaji, kama ulivyosoma hapo juu umeona rafiki na ndugu wakisimuliana changamoto zao za ndoa. kadiri ya simulizi zao hapo juu wanandoa hao ni ngumu kabisa kujenga ndoa imara lakini pia familia imara. Kama wanandoa wanaishi maisha ya paka na panya yakukwepana hakika hakuna watakachokuwa wanajenga zaidi ya kujiandaa kushindwa na kuanguka.

Huwa napokea email na simu za ushauri kwa kweli ndoa nyingi siyo salama na wanandoa wao wenyewe ndiyo wanajitengenezea gereza. Mwingine anakuambia anaamua kukaa baa ili muda uende ili akirudi akute mwenzake amelala na asubuhi anawahi kuondoa sasa kwa maisha kama haya ? kwa kutumia tu akili au ufahamu wa kawaida yaani common sense, uliingia kwenye maisha ya ndoa kufanya nini? Kwa namna hii ya kukwepana mtawezaje kujenga familia? Watoto watawezaje kujifunza maisha kutoka kwenu, mtawezaje kuwavutia hata na wale wanaotarajia kufunga ndoa na kuwaonesha mfano mzuri?

Mahusiano yoyote yanajengwa na muda sasa kama wewe huwekezi muda katika mahusiano yako ya ndoa unategemea kupata nini? Maji ukiyajengea ukuta unategemea yatafanya nini kama siyo kuruka juu na kutafuta njia ya kutokea. Maamuzi mengi yanayofanywa na watu katika mahusiano mengi ni ya kuongozwa na hisia zaidi kuliko kutumia akili. Usiposhibisha njaa ya mwenzako wako kwa kukimbia matatizo hakika dunia  kwa asili yake itakuadhibu tu na kuyaona maisha yako ni machungu.

SOMA; Huyu Ndiye Mshauri Wa Kwanza Katika Maisha Ya Ndoa.

Hatua ya kuchukua leo,kama unataka kutengeneza ndoa imara usimkimbie mwenzi wako, kaa naye mpange maisha yenu ya ndoa na familia yenu. Hakuna zawadi nzuri unayeweza kumpa mwenzi wako wa ndoa kama kumpa muda na unapomnyima kumpa zawadi hiyo lazima utamwacha katika njaa hivyo na elewa kuwa mtu akiwa na njaa lazima atafuta chakula kwa gharama yoyote ile kiwe kizuri au kibaya ili mradi ashibishe njaa yake. Usikimbie matatizo yako ya ndoa bali yatatue na hakuna kitu kizuri au kibaya bali ubaya au uzuri uko katika mtazamo, picha  uliojenga wewe kwenye akili yako.

Kwahiyo, mpe mwenzako muda, msikilize mwenzako kupitia muda pekee kila mmoja anaweza kumaliza njaa yake na hatimaye mnakuwa na maisha bora kabisa. Chochote ambacho kinachotokea katika maisha yako anayesabisha ni wewe kwa sababu kuna mahali ulikosea au kuna kitu huku fanya ndiyo maana tatizo linajitokeza.

Ukawe na siku bora rafiki yangu.

Rafiki na mwalimu wako,

Deogratius Kessy

Mawasiliano; +255717101505//+255767101504, deokessy@gmail.com , kessydeo@mtaalamu.net

Unaweza kujifunza zaidi kwa kutembelea mtandao wa Kessy Deo(www.mtaalamu.net/kessydeo )

Asante sana!