Kuna watu ambao tukiwaangalia kwa nje tunasema watu hawa ni jasiri, tunatamani tungekuwa na mioyo kama yao, mioyo ambayo haiogopi chochote na inaweza kuchukua hatua hatari bila ya hofu.

Tusichokiona ni kwamba, wale ambao kwa nje tunawaona ni jasiri sana na hawana hofu, ndani yao wana hofu kubwa. Wana hofu kama ambavyo sisi binafsi tuna hofu, wana wasiwasi na mashaka pia. Ila kuna kitu kimoja ambacho wanacho, ambacho wengine huwa wanakosa.

Kitu hicho ni uvumilivu. Kwa hakika, ukiangalia kwa kina, kile ambacho tunaita ni ujasiri siyo kingine bali uvumilivu. Hata panapokuwa na pande mbili zinazoshindana, upande unaoshinda, mara zote ni ule upande ambao unaweza kuvumilia zaidi na kwa muda mrefu zaidi.

wp-image--1475273682

Wale ambao tunawaona wanafanya mambo yasiyowezekana, siyo kwamba wao walikuwa na uhakika yanawezekana, bali walikuwa wavumilivu. Wakati wengine wanakata tamaa na kuona haiwezekani, hakuna cha kufanya tena, wao walisema hebu tuvumilie kidogo tuone tutapata nini.

SOMA; UKURASA WA 922; Kupata Na Kupoteza…

Hata wale ambao tunasema wana bahati, ukiangalia kwa undani, utagundua uvumilivu wao ndiyo umewaweka kwenye mazingira ya kuwa na bahati.

Hivyo  basi mwanamafanikio, unapokutana na changamoto yoyote, unapokumbwa na hofu, unapoona kama kila kitu kinaanguka, kumbuka hili, kuwa mvumilivu, endelea kushikilia, endelea kupambana, na kwa hakika utakutana na ushindi, na watu nje watasema huyu ni shujaa kweli kweli. Wasijue kwamba ndani yako kulikuwa kugumu kuliko kunavyoonekana kwa nje.

Njia pekee ya kuishinda hofu ya kushindwa, hofu ya kukataliwa na hata hofu nyingine yoyote ni uvumilivu, wakati mwingine, dunia ni kama inawashindwa wale watu wavumilivu na kuamua kuwaachilia wapate kile wanachotaka. Unaoneaje wewe ukawa mmoja wa watu hao?

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog