Umewahi kuona mtu ambaye ana tatizo au anakosea na kila mtu anaona hivyo lakini yeye haoni kabisa? Hata akiambiwa anakataa kabisa, kwa kuamini yupo sahihi?

Au wewe mwenyewe, umeshawahi kuwa unafanya kitu ukiona upo sahihi kabisa na watu wanakuonesha mambo yaliyo wazi lakini huoni. Ila baadaye unakuja kugundua kwamba hukuwa sahihi na kuona wazi kwamba ulikuwa unakosea?

Hapa ndipo wengi wanasema walilogwa, au kupumbazwa au kufanyiwa mambo wasiyoyaelewa.

Hata matapeli wanatumia sana njia hii, kuhakikisha mtu haoni ukweli ambao upo wazi mbele yao, badala yake wanaona kile wanachotaka kuona.

Masikini

Kinachotokea ni kwamba, akili yako inashindwa kuona tatizo na ni kwa sababu akili yako inakuwa ni sehemu kuu ya tatizo. Sasa kwa kuwa akili yenyewe ni tatizo, ni vigumu sana kuliona tatizo.

Hebu chukua mfano wa polisi ambaye amepewa jukumu la kumkamata mwizi, wakati mwizi huyo ni yeye mwenyewe, je unafikiri polisi huyo atakamata mwizi?

Hivyo ndivyo ilivyo kwa akili zetu, pale zinapokuwa sehemu ya tatizo, hatuwezi kuona tatizo, hata kama kila mtu anaona tatizo. Akili zetu haziwezi kuturuhusu tuone kwamba zinakosea.

SOMA; UKURASA WA 1035; Maamuzi Yanapokuwa Magumu, Tunafanya Vitu Rahisi…

Hivyo njia sahihi kabisa ya kuweza kuona tatizo lolote na kuweza kulitatua, ni kuweza kudhibiti akili yako. Kuhakikisha unaiona akili kama ilivyo, na siyo kuifanya akili yako kuwa wewe.

Ukiweza kuiona akili kama ilivyo, utaona udhaifu wako uko wapi na wapi unapokosea.

Njia rahisi ya kuiona akili kama ilivyo, ni kwa kufanya tahajudi. Hapa unayatuliza mawazo yote uliyonayo na pia unaweza kuchukua wazo moja moja na kulichunguza kwa kina, kulifuata mpaka kujua ukweli na uhalisia wake.

Njia nyingine ni kujihoji na kudadisi zaidi kwenye jambo lolote. Kuacha kuchukulia vitu kama vilivyo na kuviamini haraka, badala yake kuwa na nafasi ya kuhoji na kudadisi zaidi. Kwa njia hii akili itaacha kuingia kwenye mapenzi na kitu chochote, na kukupa nafasi ya kufikiri.

Usikubali akili yako ianguke kwenye mapenzi na kitu chochote kabla hujakifikiri na kukidadisi kwa kina. Kwani mapenzi yakishakuwa makali, hutaweza kuona tatizo ambalo lipo wazi kabisa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog