Happiness is a good flow of life – Zeno of Citium

Hongera rafiki kwa siku hii bora na ya kipekee sana kwetu.
Ni siku mpya ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa msingi wetu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu 2018 tutaweza kupiga hatua kubwa sana.

Asubuhi ya leo tutafakari FURAHA HAINA KANUNI…
Ukishaanza kujiambia nikipata kitu fulani ndiyo nitakuwanna furaha,
Ukajiambia nikifikia kiwango fulani cha elimu au kazi ndiyo nitakuwa na furaha,
Ukasema watu fulani wakishabadilika kwenye maisha yako basi utakuwa na furaha,
Basi jua hapo umetengeneza kanuni moja nzuri sana, kanuni hiyo ni kujihakikishia hutakuwa na furaha maisha yako yote.

Furaha haina kanuni, hivyo kanuni yoyote ya furaha unayojiwekea au kufuata itakwenda kushindwa. Lazima utashindwa. Kwa sababu chochote unachoweka kama kigezo au kipimo, huwa hakitoshelezi.

Furaha ni jinsi unavyoishi maisha yako ya kila siku, jinsi unavyochukulia kila kinachotokea na jinsi unacyochukua hatua kuwa bora zaidi.
Kama huna furaha leo, kuna uwezekano mkubwa hutakuwa na furaha kesho pia.
Kama huna furaha wakati una kipato kidogo, usitegemee ukawa na furaha kipato kitakapoongezeka.

Hakuna kanuni ya furaha kwa sababu furaha siyo kitu kinachojitegemea, bali furaha ni sehemu ya yale maisha unayoyaoshi kila siku.
Achana na kanuni yoyote ya furaha unayoifuata, ni kanuni ya kushindwa, wewe ishi maisha yako na maisha yatakuwa bora na yenye furaha.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha