Sheria huwa zinatengenezwaje? Ni baada ya watu kufanya mambo fulani, halafu matokeo yake yakaonekana siyo mazuri hivyo sheria inawekwa kuwazuia watu kufanya kitu hicho.
Kwa mfano, watu kunywa pombe na kisha kuendesha magari au mashine hupelekea kupata ajali zaidi. Hivyo sheria inakuwa hairuhusiwi kunywa pombe na kisha kuendesha mashine au gari.
Kadhalika kwenye maisha yako, unapaswa kujiwekea sheria, sheria ambazo zitakuzuia wewe kurudia yale mambo ambayo umewahi kuyafanya au umezoea kuyafanya lakini hayakuletei matokeo bora kama ulivyotegemea.

Zipo sheria nyingi unazoweza kujiwekea, lakini leo nakwenda kukukumbusha tatu muhimu sana, ambazo zitakuwezesha kupiga hatua kwenye maisha yako.
Moja; fanya mambo magumu mapema.
Iwe ni kwenye siku yako au kwenye maisha yako, anza na yale mambo ambayo ni magumu. Mwanzo wa siku, au mwanzo wa maisha, wakati bado ni kijana, unakuwa na nguvu kubwa ya kuweza kuweka juhudi kubwa. Hizi ndiyo nguvu unapaswa kuzitumia ili kuweza kufanya yale magumu.
Wengi wamekuwa wanafanya kinyume hapo, wamekuwa wakiahirisha kufanya yale magumu mpaka baadaye, wakati wanapokuja kutaka kuyafanya, wanajikuta hawana nguvu wala muda wa kuweza kuyafanya.
SOMA; UKURASA WA 750; Tengeneza Uhalisia Unaoutaka Wewe…
Mbili; maisha siyo sinema, siyo kila kitu kitaishia vizuri.
Kila sinema huwa na mwisho mzuri, na tunapenda kuangalia sinema na kutamani maisha yetu yawe kama kwenye sinema. Lakini huo siyo uhalisia, jua na jiambie ya kwamba maisha siyo sinema, maisha ni uhalisia, ambao hakuna anayejua kesho nini kitakuja. Hivyo jambo muhimu ni kuishi leo, kuweka kila juhudi unazoweza kuweka, na kujua kesho itakuja tofauti.
Tatu; omba msaada, usikazane kufanya kila kitu mwenyewe.
Unahitaji msaada kwenye maisha yako, kwa sababu huwezi kufanya kila kitu, huna muda wala nguvu za kuweza kufanya yote hayo. Unahitaji ushirikiano wa wengine kwenye kila kitu ambacho unakifanya. Hivyo kazana kutengeneza mahusiano mazuri na wengine ili waweze kuwa tayari kukusaidia unapokuwa na uhitaji.
Jikumbushe sheria hizi tatu kila wakati, ongeza nyingine pia kama utaweza. Lakini usikubali kwenda na maisha yako kwa mazoea, utaanguka.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog