The first and greatest punishment of the sinner is the conscience of sin. – Lucius Annaeus Seneca
Asubuhi njema mwanamafanikio.
Hongera kwa siku hii mpya na ya kipekee sana kwetu.
Ni nafasi nyingine nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Ni kwa msingi wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ni mwongozo wetu kwa mwaka huu 2018.
Asubuhi ya leo tutafakari ADHABU KUBWA YA MKOSAJI…
Kwenye maisha yetu, wapo watu ambao wanatukosea katika mambo mbalimbali.
Ni rahisi kutamani kuwaadhibu watu hawa, kulipa kisasi na kuwaonesha kwamba wamekosea.
Lakini hiyo siyo adhabu kubwa kwa wakosaji hao.
Adhabu kubwa kabisa kwa mkosaji yeyote ni UTAMBUZI WA KOSA LAKE.
Pale mtu anapotambua kwamba amefanya kosa, na hilo likamwingia ndani kabisa, linamuumiza kuliko hata aliyekosewa.
Lakini kama mtu hatatambua kosa alilofanya, hata ukimwadhibu sana sana ataona unamwonea, au wewe ndiye unayekosea.
Hivyo badala ya kukazana kuwaadhibu wakosaji au kutaka kulipa kisasi, hakikisha kwamba wametambua kosa walilofanya na kwa njia hiyo watajiadhibu sana wenyewe.
Umewahi kumwambia mtu kitu ukifikiri ni utani, lakini mtu yule akakuambia hajapendezwa na hilo na hapo ukajisikia vibaya kwa ulichosema?
Hivyo ndivyo utambuzi wa kosa unavyoadhibu.
Wafanye watu watambue makosa yao na kisha waache wajiadhibu wenyewe kwa makosa waliyofanya.
Kwa njia hiyo watajifunza na siyo rahisi kurudia tena kile walichofanya.
Kadhalika kwa upande wako, tambua kila kosa unalofanya, kwako na kwa wengine pia, na hakikisha unajifunza na hurudii tena kosa hilo.
Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha
Asante sana kocha; kwa tafakari hii njema. Nimeipenda, waache watu wajiadhibu wenyewe.
LikeLike
Karibu.
LikeLike