Wakati nipo chuo kikuu, kuna profesa mmoja nilikuwa nampenda sana kwa mtindo wake wa ufundishaji. Haukuwa mtindo wa kukulisha mwanafunzi vitu, badala yake alitoa maswali ya kukufanya ufikiri na wewe mwenyewe utengeneze majibu yako. Siyo wote waliopenda mtindo huo wa ufundishaji, lakini nilichogundua ni kwamba, kupitia mtindo huo nilikuwa naelewa sana na kwa muda mrefu kuliko kukariri.

Siku moja profesa huyu aliuliza swali moja ambalo lilinifanya nifikiri sana. Alianza kwa kusema ninyi watu hamfikiri wala kudadisi kabisa, mnafanya mambo kwa mazoea tu na hilo linawagharimu. Aliuliza ni wangapi wamewahi kufika eneo la posta dar es salaam, tukanyoosha mikono. Akauliza wangapi wamewahi kuona sanamu ya askari iliyopo posta, tukanyoosha mikono. Mwisho akauliza, wangapi wanajua ile bunduki ambayo askari wa kwenye sanamu ameshika imeelekezwa upande upi, hakuna hata mmoja alikuwa na jibu.

Ni rahisi kuona hicho ni kitu ambacho hakina manufaa yoyote kwenye maisha yako, kujua uelekeo ambao bunduki ya sanamu ipo! Ukishajua tu kuna sanamu inatosha. Ndivyo wengi tunavyofikiri hivi na inatugharimu sana.

Nimekuja kuiona gharama hii baadaye, siku moja nikiwa mitaa hiyo hiyo ya posta, mtaa huo huo wenye sanamu, lakini kwa mbali kidogo, kuna sehemu ambayo nimekuwa nazoea kupaki gari na kuendelea na shughuli zangu. Nimekuwa nafanya hivyo kwa mazoea na haijawahi kuwa shida. Sasa siku moja wakati naingia eneo hilo na gari ili kupaki, nikashangaa askari wawili wa usalama barabarani wanakuja kwa kasi sana. Wakaniambia nimepita barabara ambayo hairuhusiwi kupita na hivyo wakaniandikia kosa, shilingi elfu 30.

Pale ndipo nilipoanza kujiuliza hivi kumbe barabara hii hairuhusiwi kupita wakati wote? Basi siku nyingine nikiwa naelekea eneo hilo hilo, nilipofika pale nilipozoea kukatiza, niliona bango liko pale, tena ni bango la siku zote, likionesha hairuhusiwi kupita njia hiyo. Alama ilikuwa pale, lakini sikuwa naifuata kwa sababu nilikuwa nafanya kwa mazoea, na akili yangu haikuona umuhimu wa kutafuta alama hiyo. Lakini baada ya kuadhibiwa, sasa akili yangu inaona kwa usahihi kabisa.

Huu ni mfano mmoja ambao unaonesha jinsi ambavyo tunaruhusu akili zetu zizurure zitakavyo inavyoweza kutugharimu. Watu huwa hawasemi lakini chunguza kwa umakini, matatizo mengi ambayo watu wanaingia, ni kwa sababu hawakuwa wanafikiri sawasawa wakati wanafanya. Walikuwa wanafanya kwa mazoea, akili zao zikiwa eneo tofauti kabisa na pale ambapo wao wapo.

Ukweli ni kwamba, tunaishi kwenye zama za kelele, zama ambazo kupata nafasi ya kufikiri ni kitu kigumu sana kutokea kwenye maisha ya mtu yeyote yule. Kama hutalazimisha akili yako ifikiri, basi mara zote utakuwa unaenda na mkumbo au kufanya kwa mazoea, kitu ambacho kitakuzalishia matatizo mengi.

kuzurura kwa akili

Zama hizi watu wamekuwa wakijisifu kabisa kwa uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Kwa mfano kuongea na simu huku unaendesha gari, kuangalia tv huku unakula, kusoma huku unafanya kitu kingine. Ni rahisi kuona tunaokoa muda kwa kufanya vitu vingi kwa pamoja, lakini ukweli ni kwamba, tunagharimu akili zetu na tunapoteza ubora na thamani ambayo tungeweza kutoa.

Kwa mfano, kuongea na simu huku unaendesha gari, hakutakuwa na tatizo lolote kama kila kitu kitaenda sawa. Lakini pale linapotokea tatizo, ambalo linakutaka ufikiri na kuchukua hatua haraka, hapo ndipo shida inapoonekana. Kwa mfano unaendesha gari huku unaongea na simu, ghafla mbele yako gari nyingine ikafunga breki za haraka, wewe hutaweza kufunga kwa haraka kama yeye, na utamgonga. Kadhalika akatokea mtu mbele yako, ni rahisi zaidi kumgonga kama akili yako imegawanyika.

Watu wamekuwa wanafikiri tatizo la kuongea na simu wakati wa kuendesha ni kuishika, hivyo kumekuja vifaa ya kuiweka simu sehemu ambayo wewe unaongea tu bila ya kuishika, lakini hilo siyo suluhisho. Tatizo la kuongea na simu wakati unaendesha gari, au hata mashine yoyote, ni kwamba akili yako inakuwa imegawanyika, hivyo unapohitajika kufanya maamuzi sahihi na ya haraka, huwezi.

Kuzurura kwa akili ndiyo shida kubwa ya zama tunazoishi sasa. Akili zetu zimetekwa na kila aina ya kelele. Na kelele kubwa zipo kwenye kifaa tunachotembea nacho kila mahali, na kwenda nacho mpaka kitandani, simu janja au kama inavyojulikana kwa kiingereza smartphone.

Ni vigumu sana kutuliza akili na kufikiri kwa kina, wakati dunia nzima unatembea nayo mkononi. Ni vigumu kukaa na hali ya kujisikia vibaya na kufikiri mpaka upate suluhisho wakati kila dakika unaingia kwenye mitandao ya kijamii.

Ukweli ni kwamba, kama mtu hutachukua hatua, kuzurura kwa akili yako kutakuwa gharama kubwa sana kwenye maisha yako. Utafanya makosa ambayo baadaye unajiuliza ulikuwa unafikiria nini. Utashindwa kutatua changamoto unazokutana nazo kwenye maisha yako ya kila siku.

Je unawezaje kuituliza akili kwenye zama hizi za kelele?

Ipo dhana inaitwa MINDFULLNESS, hii ndiyo dhana ambayo nakwenda kukushirikisha leo, ambayo kama ukiweza kuifanyia kazi, utaweza kuituliza akili yako, kufanya maamuzi sahihi na kuweza kufikiri kwa kina.

Unachofanya kwa dhana hii, ni kuwa na UWEPO KIAKILI, yaani chochote unachofanya basi akili yako yote iwe pale.

Itulize akili yako kwa kuhakikisha mawazo yako yote yapo kwenye kile kitu unachofanya. Hata kama ni kitu kidogo kiasi gani, weka mawazo yako yote pale. Usifanye kitu kimoja huku unafikiria kitu kingine, hapo utakuwa unakosa vitu vyote.

Kwa mfano watu wengi wamekuwa hawafanyi kazi na wala hawapumziki, hii ni kwa sababu wakati wa kazi wanafikiria mapumziko na wakati wa mapumziko wanafikiria kazi. Hivyo wanajikuta kila wakati wamebanwa, siyo na kazi wala mapumziko na hakuna kikubwa wanachoweza kukamilisha.

uwepo kiakili

Sasa zoezi la uwepo kiakili ni rahisi kusema, lakini utekelezaji wake ni mgumu sana, hasa kama umeshazoea usumbufu. Kama umeshazoea kula huku unaangalia tv, au kuendesha huku unawasiliana kwenye simu, ni vigumu kurudi kwenye uwepo kiakili.

Lakini lipo zoezi rahisi sana ambalo linaweza kukusaidia kujijengea uwepo kiakili kwenye jambo lolote unalofanya. Zoezi hilo ukiweza kulifanya, utaanza kuituliza akili yako, kudhibiti mawazo yako na kuiweka akili yako kwenye chochote unachofanya, hata kama ni kidogo kiasi gani.

Zoezi hilo ni TAHAJUDI, hili ni zoezi la kudhibiti mawazo yako na kutuliza akili yako. Katika zoezi hili, unaweza kuanza na kitu kidogo kama pumzi yako, unachofanya ni kuelekeza akili na mawazo yako kwenye pumzi yako tu.

Unaacha kufikiria kitu kingine chochote na unafikiria pumzi yako tu. Unachokifanya ni kuhesabu pumzi yako, unapovuta hewa ndani hesabu moja, ukitoa hewa nje unahesabu mbili, unadendelea hivyo mpaka kumi kisha kuanza tena moja. Wakati ukifanya hivyo unaisikilizia hewa jinsi inavyoingia kwenye pua yako na kwenda mpaka kwenye mapafu yako.

SOMA; Kitabu; Jinsi ya Kufanya Meditation na Faida Zake.

Wakati unafanya hivyo mawazo yako yataanza kutangatanga, utaanza kufikiria mambo mengine, lakini usiruhusu mawazo yako yapotee, badala yake yarudishe kwenye pumzi yako. Endelea kufuatilia pumzi yako, endelea kuhesabu kila pumzi mpaka ufike hatua kwamba hakuna kingine chochote unachofikiria kwa wakati huo bali pumzi yako tu.

Zoezi hili huhitaji kufanya kwa masaa, bali unaweza kuanza na dakina 5, 10 15 au hata nusu saa. Unapoanza, anza na muda mfupi uwezavyo, jipe dakika tano tu za kufuata pumzi yako, kaa eneo tulivu ambalo watu hawatakusumbua, pia funga macho ili kupunguza usumbufu wa macho yanapoona kitu kipya. Pia kaa kitako, usilale, maana ukilala ni rahisi kupotelea usingizini.

Kwa kufanya zoezi hili mara kwa mara, unaanza kushika hatamu ya akili na mawazo yako. Unakuwa umerudisha udhibiti ambao kwa sasa umeshaupoteza, na huu utakusaidia sana.

Sasa kwenye kila unachokuwa unafanya, weka uwepo wako kiakili. Kwa kuhakikisha akili yako na mawazo yako yote yapo kwenye hicho unachofanya. yanapotaka kuponyoka kwa kuanza kufikiria kitu kingine, yarudishe pale.

Anza zoezi hili kwa mambo madogo madogo kama kula chakula. Unajua siku hizi watu hata hawafurahii tena hata ladha za vyakula kwa sababu akili zao hazipo kwenye chakula wanachokula. Mtu anakula huku yupo kwenye mitandao ya kijamii, hivyo zoezi zima la kula linakuwa kama kitu cha kupita tu. Hivyo anza kuweka uwepo wako kiakili kwenye zoezi kama la kula, na fikiria kile chakula unachokula, tafuna vizuri, sikia kila ladha ya kilichopo kwenye chakula. Na hapa siyo lazima kiwe chakula cha kipekee sana, hata kama ni ugali maharage, ukila kwa uwepo wa kiakili, utafurahia kuliko hata anayekula chakula kinachoonekana ni cha maana zaidi lakini hali kwa uwepo kiakili.

Uwepo kiakili ni suluhisho muhimu na hatua ambayo kila mtu anapaswa kuichukua hasa kwa zama ambazo tunaishi. Kwa sababu kelele ndiyo zinazidi, machaguo yanazidi kuwa mengi na maamuzi yanakuwa magumu kufanya. Unapoweka uwepo kiakili kwenye jambo lolote unalofanya, unalielewa vizuri na kuweza kuchukua hatua sahihi.

Usikubali mawazo yako yawe mbali na pale ulipo, popote ulipo sasa, hapo ndipo unapopaswa kuwepo, akili na mawazo yako yote yawe hapo. Mawazo mengine yanapokujia, jiambie wakati wake utafikia na yarudishe hapo ulipo sasa.

Fanya zoezi hili rafiki yangu na utaona jinsi utakavyookoa muda wako, fedha zako na nguvu zako pia. Kwa sababu kuzurura kwa akili yako kunakugharimu muda kwa kuchukua muda mrefu kukamilisha jambo, kunakugharimu nguvu, kwa kujihusisha na mambo mengi kwa wakati mmoja na pia kunakugharimu fedha kwa makosa unayofanya pale akili yako inapokuwa mbali na kile unachofanya.

Uwepo kiakili ni jawabu sahihi kwenye zama hizi za kelele, hakikisha unaishi hili kila siku na kwenye kila unachofanya.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog