Rafiki yangu mpendwa,

Waswahili wanasema kila zama na kitabu chake, kwamba kila zama huwa zina mambo yake ambayo watu waliopita zama za nyuma, hawawezi kuyaelewa. Na wale wanaosema enzi zetu tungefanya hivi, haisaidii kwa sababu hawakuwahi kuwa na vitu vinavyokuwepo kwenye zama mpya.

Kwa mfano sasa hivi ukamrudisha duniani mtu aliyefariki miaka 50 iliyopita, atashangaa kila kitu kinavyoendelea hapa duniani. Atafurahi sana kuona maendeleo makubwa sana, lakini pia atashangazwa sana na jinsi maendeleo haya yamekuwa utumwa na kikwazo kwa wengi kufanikiwa.

Kitu kimoja cha kushangaza kuhusu sisi wanadamu ni kwamba hatua tunazopiga, ambazo zingepaswa kuyafanya maisha yetu kuwa bora zaidi, zinageuka kuwa kikwazo kwenye maisha ya mafanikio kwetu.

Kwenye makala hii, tutakwenda kuangalia changamoto mbili kubwa, ambazo zinatokana na maendeleo makubwa ambayo tumepiga, lakini changamoto hizo zinakuwa kikwazo kwetu kufanikiwa.

Changamoto ya kwanza; machaguo mengi mno.

Watu walifikiri kwamba uwepo wa machaguo mengi ungeleta uhuru wa watu kuchagua kile wanachotaka na kutokufanya wasichotaka kufanya. Lakini hili limekuwa kinyume, uwepo wa machaguo mengi umefanya kuwa vigumu sana kufikia maamuzi.

Kadiri machaguo yanavyokuwa mengi, ndivyo watu wanavyoshindwa kuchagua kipi hasa wanataka. Kwa sababu kuchagua kufanya kimoja kati ya vingi ambavyo vyote vinaonekana ni vizuri, ni kazi ngumu sana.

Hali hii ya kuwepo kwa machaguo mengi imewafanya wengi kuwa na wasiwasi, wasijue kama wanachotaka kufanya ni sahihi. Na pia imewaondolea wengi furaha kwa sababu hata baada ya kuchagua kitu kimoja, wanafikiria vingi ambavyo wameacha.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Uwepo wa machaguo mengi pia umekuwa kikwazo kwa watu kujitoa na kuwa na uvumilivu. Kile tunachoona kwa watu kwamba wanajaribu kitu fulani, wakiona hakifanyi kazi wanakimbilia kujaribu kingine na kingine, mwisho wa siku wanajikuta wamefanya mambo mengi lakini hawana mafanikio, ni uwepo wa machaguo mengi.

Kama mtu ana nafasi nyingi za kuchukua, anapochukua nafasi moja, akaona haimpi anachota, badala ya kukazana na nafasi hiyo, anakimbilia kwenye nafasi nyingine. Sasa hakuna mafanikio yanayopatikana kwa kujaribu jaribu vitu. Mafanikio yanapatikana kwa kuweka juhudi zako eneo moja kwa muda mrefu.

Kuondokana na changamoto hii ya machaguo mengi, unahitaji kufanya maamuzi na kuishi maamuzi yako. Hata kama machaguo ni mengi kiasi fani, tuliza akili yako, chagua nini unataka kufanya na ukishachagua, sahau kuhusu machaguo mengine na weka nguvu zako zote kwenye kile ulichochagua. Ona kama huna kingine unachoweza kufanya ila hicho, na kwa hakika utafanikiwa.

SOMA; MINDFULNESS; Jinsi Kuzurura Kwa Akili Zetu Kunavyotugharimu Kwenye Maisha Na Jinsi Ya Kuzituliza Akili Zetu.

Changamoto ya pili; usumbufu na kelele.

Hatua nyingine kubwa tuliyopiga kwenye zama hizi, ni uwezo wa kuwasiliana na mtu yeyote, popote alipo duniani ndani ya muda mfupi. Pia uwezo wa kupata taarifa yoyote inayotokea duniani, muda huo huo ambapo imetokea, masaa 24 kwa siku na kila siku ya mwaka.

Simu za mkononi na mitandao ya kijamii imerahisisha sana mawasiliano na kusambaa kwa taarifa. Lakini pia imekuja na changamoto kubwa inayowazuia wengi kupiga hatua. Changamoto hiyo ni usumbufu na kelele.

Kwenye zama hizi, mtu kukaa saa moja bila ya kugusa simu yake, bila ya kuperuzi mitandao ya kijamii inaonekana ni tukio la kishujaa. Mtu kuendelea kufanya shughuli zake huku simu inaita na akaamua kuiacha, au kuna ujumbe umeingia na akaamua asiujibu kwa wakati huo ni jambo linaloweza kuonekana ni la kishujaa na anayeweza kufanya hivyo ni mtu wa tofauti kabisa.

Tupo kwenye zama ambazo usumbufu umekuwa kawaida kiasi kwamba kukaa kimya au kujipa muda wa utulivu ni kitu cha kushangaza kwa wengi. Usumbufu tulionao unawafanya wengi kukosa muda wa kufikiri na kutafakari kwa kina kuhusu kile wanachofanya na hilo linawagharimu sana kwenye maamuzi ambayo wanafanya.

Kuondokana na changamoto hii, unahitaji kujiwekea mipaka mikali sana. kwanza unahitaji kuwa na ukomo kwenye matumizi ya vifaa vyenye usumbufu kwako. Pia unahitaji kuwa na muda wako mwenyewe, muda ambao kutafakari na kufanya yale muhimu kwako bila ya usumbufu wowote.

Na kumbuka, hakuna chochote ambacho kinakupita kama utatenga muda wa kufanya kazi bila ya usumbufu. Pia kumbuka huhitaji kujua kila kinachoendelea, huhitaji kujibu kila ujumbe unaoingia kwa wakati unapoingia na huhitaji kupokea kila simu inayopigwa.

Muhimu zaidi kumbuka huhitaji kutembea na simu yako kila wakati na kukaa nayo karibu kwa masaa 24 kwa siku. Unahitaji muda wa kuwa mbali na simu yako ili angalau uwe na maisha yako.

Rafiki, changamoto hizi mbili zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wengi kufanikiwa. Japo wengi hawazioni kama changamoto, kwa sababu bado wanaamini ni fursa nzuri kwao, lakini jinsi wanavyozitumia, badala ya kuwa fursa, inakuwa changamoto.

Wewe umeshajifunza njia bora ya kuzuia fursa hizi zisiwe changamoto, fanyia kazi haya uliyojifunza na maendeleo tuliyonayo kwenye zama hizi yatakuwa baraka kwako badala ya kuwa kikwazo na changamoto kwako.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha