Hongera rafiki yangu kwa juma hili namba saba la mwaka huu 2018.

Ni imani yangu kwamba umekuwa na juma bora sana, yapo makubwa uliyofanya na yapo mengi zaidi uliyojifunza. Nenda kayatumie hayo kwenye juma namba nane tunalokwenda kuanza, ili mwaka huu 2018 ukawe mwaka wa kipekee sana kwako.

Karibu kwenye makala yetu ya TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya juma tunalokuwa tumemaliza. Mambo haya yanajumuisha yale niliyojifunza, niliyokutana nayo au kuyaona na kukukumbusha huduma mbalimbali ninazotoa.

Bila ya kupoteza muda tuingie kwenye tano za juma, lakini kabla hebu tupate #NENO la kumaliza juma letu hili.

#NENO; ISHI WEWE, WENGINE WAMESHACHUKULIWA…

Maisha ni magumu, lakini sisi wenyewe tumekuwa tunayafanya yawe magumu zaidi. Hasa pale tunapokazana kuishi maisha ya kuwafurahisha wengine, na hivyo kulazimika kuishi maisha ya kuigiza, maisha ambayo siyo halisi kwetu. Tunafanya vitu ambavyo hatupendi kufanya, na wala havina maana kwetu, kwa sababu tu tunataka tuonekane na watu fulani kwamba na sisi tupo aina fulani.

Hili linafanya maisha kuwa magumu kwa sababu, wale tunaokazana watuone, wala hawana muda na sisi. Wanahangaika na maisha yao, ambayo nayo ni changamoto kwao, au wanahangaika na kuwaridhisha wengine na hivyo hawakuoni wewe unavyohangaika kuwaridhisha.

Wakati mwingine watu wanalalamika kwamba hawapati watu sahihi kwenye maisha yao, hawapati wenza sahihi, hawapati watu sahihi wa kushirikiana nao. Na hilo ni rahisi kupata sababu, ambayo ni kila mtu kuwa kwenye maigizo wakati wa kuanza. Na kwa kuwa tunajua maigizo huwa hayadumu muda mrefu, basi muda unapokwenda, rangi halisi za watu zinaonekana na watu kufikiri wenzao wamebadilika. Watu huwa hawabadiliki, ila wanajionesha, wanachoka kuigiza na mambo yanabaki wazi.

Acha kuigiza, acha kuishi maisha ya wengine, ishi maisha yako, ishi uhalisia wako, fanya kile chenye maana kwako, kile ambacho unakiamini kweli, kile ambacho upo tayari kukifanya hata kama hakuna anayekuangalia, hakuna anayekusifia, na kwa njia hii utakuwa na maisha yenye furaha, na pia utawavutia watu sahihi kwa kuwa kile unachoonesha ndicho kilicho ndani yako.

Na kwa kumalizia, waigizaji huwa wanavutia waigizaji, ukianza kuwa halisi, waigizaji wote wanakukimbia, kwa sababu hawataweza kuvumilia ule uhalisi wako.

#1 KITABU NINACHOSOMA; THE PATH OF PROSPERITY.

Wiki hii nimeweza kusoma vitabu vitatu, kimoja nitakushirikisha kwenye makala ya uchambuzi wa vitabu kwenye AMKA MTANZANIA, kingine sitakushirikisha popote, na kimoja nakwenda kukushirikisha hapa ambacho ni THE PATH OF PROSPERITY ambacho kimeandikwa na JAMES ALLEN. Kama wewe ni mtu unayependa kujifunza na kuwa na mawazo chanya, nina uhakika umewahi kusikia hilo jina JAMES ALLEN, kama bado hupati picha, niambie kama umewahi kusikia kitabu kinaitwa AS A MAN THINKETH. Hichi ni kijitabu kifupi mno, lakini ambacho kimekuwa na nguvu kubwa sana, nguvu ambayo imewawezesha watu kufanya makubwa sana. Sasa hicho nitakushirikisha siku nyingine, leo nakwenda kukushirikisha kitabu chake kingine cha THE PATH OF PROSPERITY.

Nikianza kwa kumwelezea James Allen mwenyewe, alikuwa mwandishi ambaye alikuwa akiandika sana kuhusu nguvu ya akili na mawazo kwenye maisha yetu. Ni mmoja wa watu ambao wamechangia sana kwenye vuguvugu la fikra na mtazamo chanya kama njia ya kutengeneza mafanikio ambayo mtu anayataka.

Sasa kwenye kitabu hichi cha THE PATH OF PROSPERITY, James Allen anaonesha jinsi ambavyo njia ya utajiri kwenye maisha inavyoanzia ndani yetu. Kila ukurasa wa kitabu hichi ni madini, wakati nasoma kitabu hichi nilikuwa naandika ‘notes’ nikajikuta kuna sehemu naandika ukurasa mzima nikaanza kujiuliza sasa nakopi kitabu kizima na kukihamishia kwenye note book!

Kwenye sura ya kwanza anaanza kwa kutuonesha asili ya ubaya na uovu kwenye maisha yetu iko wapi. Na anaonesha wazi kwamba, ubaya na uovu asili yake ni ndani ya mioyo yetu na unatokana na kutokujua uhusiano wa asili wa vitu. Hisia kama za wivu, chuki, hasira na hata hali kama magonjwa, umasikini na mengine ni matokeo ya kile ambacho kipo ndani yetu. James anatuambia ubaya na uovu tunaweza kuukomesha kabisa kwenye maisha yetu kama tutaelewa uhusiano wa asili wa vitu.

Kwenye sura ya pili, Allen anatuonesha jinsi gani kila kinachotokea kwenye maisha yetu siyo ajali wala bahati mbaya, bali tumepanga wenyewe, kwa kuvutia vitu hivyo. Anatuonesha jinsi mawazo yetu yalivyo na nguvu ya kuumba na kuvuta vitu kwenye maisha yetu. James anaeleza pia kwamba hata mambo yanayotokea kwenye taifa, kama maafa, vita na hata magonjwa, yanatokana na nguvu ya mawazo ya wananchi hao. Kama wananchi wengi wanakuwa na mawazo ya aina fulani, basi nchi nzima inaingia kwenye hali hiyo. Na hili linaeleza wazi kwa nini watu wanapokuwa na hofu mambo mabaya hutokea kwa wengi, ni nguvu ya mawazo ambayo yanatawala akili za wengi.

Kwenye sura ya tatu, Allen anatupa siri ya kuondoka pale tulipo sasa na kufanikiwa zaidi. Na ameeleza kwa kina sana kwamba huwezi kutoka hapo ulipo sasa kama hautakubali hapo ulipo sasa. Lazima upatumie vizuri hapo ulipo kama kweli unataka kupiga hatua. Anatoa mfano kwamba kama unaishi kwenye nyumba ndogo au chumba kimoja na unatamani kuishi kwenye nyumba kubwa, hutaweza kufika kwenye hiyo nyumba kubwa kama hutaishi vizuri kwenye hiyo nyumba ndogo. Anasema ishi kwenye nyumba hiyo ndogo vizuri, ifanye kuwa safi, ifanye kuwa na amani, ifanye eneo ambalo kila mtu anapenda kuwa, halafu hapo utakuwa umejiweka tayari kwa ajili ya nyumba kubwa.

Kuna baadhi ya vitu nimevinakili moja kwa moja kwenye sura hii, na nitaviweka moja kwa moja maana kuna mengi ya kujifunza. James anasema kwamba;

“Kabla hujalalamika kwamba wewe ni mtumwa kwa mtu mwingine, angalia kwanza kama hujajiweka kuwa mtumwa wako mwenyewe”. Na hili nimelielewa sana, kabla hujalalamika kwamba mwajiri wako anakutumikisha, umejaribu kujiangalia kama wewe mwenyewe hujitumikishi na madeni yasiyo ya msingi?

“Usilalamike kwamba watu matajiri wanakunyonya, una uhakika kwamba wewe ungekuwa tajiri usingewanyonya wengine? Na je siku za nyuma hujawahi kuwa kwenye nafasi fulani ambayo uliwanyonya wengine?” Hili nalo nimelielewa sana, maana wapo watu ambao ni mafundi wa kulalamikia walio juu, ila subiri wapate nafasi hizo, mtajiuliza hivi huyu ndiye aliyekuwa analalamika kweli?

“Njia pekee ya kuelekea kwenye utajiri na siyo tu utajiri wa fedha bali utajiri wa kila kitu, ni kujijengea maadili ambayo utayaishi. Bila ya maadili, chochote utakachopata, utakipoteza.” Dah, hakuna ukweli zaidi ya huu, wewe angalia tu namna ambavyo watu wanapata utajiri na mafanikio, lakini hayadumu, chunguza kwa ndani na utakuta watu hao walitumia njia ambazo siyo sahihi, au baada ya kufanikiwa walifikiri wanaweza kufanya chochote wanachotaka wao.

Yapo mengi sana ya kujifunza kwenye kitabu hichi, mengi mno, kuna sura nyingine tatu ambazo sijaziandikia kabisa hapa, kama sura ya tano ambapo anaelezea siri ya afya, mafanikio na mamlaka, Allen anatuonesha jinsi ambavyo sisi wenyewe tumekuwa tunayakaribisha magonjwa ambayo tunayapata kwenye maisha. Yaani ukisoma sura hii na ukaielewa, basi hutaruhusu mwili wako unase magonjwa.

Hichi ni kitabu kizuri sana ambacho nashauri kila mtu akisome, na mwisho wa makala hii nitakitoa kama zawadi, endelea kusoma ujue utakipataje, nitakituma kwa atakayepata zawadi hiyo.

#2 MAKALA YA WIKI; GHARAMA YA KUZURURA KWA AKILI YAKO.

Akili zetu ni kitu cha kushangaza sana, tunaweza kuwa eneo fulani kimwili, lakini kiakili tupo mbali sana. Unaweza kuwa unakula chakula, lakini akili yako ipo kwenye sherehe fulani uliyohudhuria siku za nyuma, au ugomvi ulioingia na mtu mwingine.

Tunaweza kuona hii ni nguvu kubwa ya akili, lakini pia ni hasara kubwa sana. Ipo gharama kubwa sana pale akili zetu zinapozurura zitakavyo bila ya sisi kuwa na udhibiti juu ya hilo.

Wiki hii niliandika makala kuhusiana na hili la kuzurura kwa akili, na wengi wameniandikia kusema jinsi gani makala hiyo imekuwa msaada kwao, hasa kwa zama hizi za kelele. Kama hukupata nafasi ya kusoma makala hiyo, unaweza kuisoma hapa; MINDFULNESS; Jinsi Kuzurura Kwa Akili Zetu Kunavyotugharimu Kwenye Maisha Na Jinsi Ya Kuzituliza Akili Zetu. (https://amkamtanzania.com/2018/02/16/mindfulness-jinsi-kuzurura-kwa-akili-zetu-kunavyotugharimu-kwenye-maisha-na-jinsi-ya-kuzituliza-akili-zetu/ )

#3 NILICHOONA WIKI HII; MOTO UPO HAPA HAPA DUNIANI.

Wahindu na Wabudha wana msingi kwenye imani yao unaitwa KARMA. Msingi huu unaeleza kwamba, chochote ambacho mtu anafanya, basi kinamrudia, hivyo matokeo ambayo mtu anayapata sasa ni kutokana na mambo ambayo alifanya huko nyuma.

Wazungu wanasema ‘what goes around comes around’

Na sisi ‘wabongo’ tunasema moto upo hapa hapa duniani, kwamba lolote unalofanya, unalipwa hapa hapa kabla hata hujaenda kukutana na hukumu yako kulingana na imani uliyonayo.

Nimeliona hilo wiki hii kwenye kujiuzulu kwa Raisi wa Afrika Kusini Jacob Zuma. Kama wewe ni mgeni wa siasa za Afrika Kusini, ukiangalia zoezi hili la kumshinikiza kujiuzulu lilivyokwenda, ukimsikiliza wakati anajieleza, akisema haoni kosa lake kwa nini anashinikizwa ajiuzulu na hata kuomba apewe muda kidogo ili amalizie baadhi ya mambo ambayo anayafanyia kazi, utaweza kumwonea huruma, na kuona hata kama ana makosa, kwa nini asiachwe tu amalizie muda mfupi aliobakiza.

Lakini kama umekuwa mfuatiliaji wa siasa za nchi hiyo, utakumbuka kwamba miaka kumi iliyopita, mwaka 2008, tukio kama linalotokea sasa lilitokea, ambapo raisi wa kipindi hicho, THABO MBEKI alishinikizwa kujiuzulu uraisi na aliyekuwa kinara wa kusukuma hilo alikuwa JACOB ZUMA. Na hata shutuma kwake zilikuwa kama anazopata sasa, nyingi zikiwa za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.

Sheria ya asili inasema kwamba chochote kinachotokea kinasababishwa, na asili huwa haidanganywi au kukopwa, bali huwalipa watu sawasawa na kile walichofanya. Hivyo tunapaswa kujitahidi sana kufanya lililo sahihi wakati wote, kwa sababu kila tunachokifanya, baadaye kitarudi kwetu. Tukifanya kibaya, tutalipwa ubaya na tukifanya mazuri tutalipwa mazuri. Ni sheria, siyo bahati, hivyo ifuate unufaike au ikatae uumie.

#4 HUDUMA NINAZOTOA; PROGRAMU YA KUKUWEZESHA KUSOKA KITABU KIMOJA KILA MWEZI.

Naamini sana kwenye usomaji wa vitabu, kwa sababu nimekuwa naona manufaa yake kwangu na kwa wengine pia. Hivyo nimekuwa nasema wazi, kama unaangalia tv, unatumia simu halafu husomi kitabu, hujui unakopeleka maisha yako. Naenda mbali zaidi na kusema kwamba kama unaweza kutembea na simu yako kila mahali, lakini huwezi kutembea na kitabu, hata kama ni cha mfumo wa kielektronini basi akili yako haifanyi kazi sawa sawa. Na pia huwa naamini kabisa, kama unanunua nguo, lakini hununui vitabu, basi unasitiri mwili lakini unaiacha akili yako uchi, na madhara yake ni kuishia kutumiwa na wengine na usione unafanya nini kikubwa kwenye maisha yako.

Yote hayo ni kwenye kukusisitiza wewe rafiki yangu usome vitabu, kwa sababu vina manufaa. Lakini kilio cha wengi kimekuwa kutopata muda wa kusoma vitabu, au kutokujua vitabu gani wasome, au wapate wapi vitabu vya kusoma. Yote hayo nimeyatatua kwa huduma ya PROGRAM YA KUSOMA KURASA KUMI ZA KITABU KILA SIKU. Hii ni program inayokutaka usome kurasa kumi tu za kitabu kila siku, kitu ambacho kitakuwezesha kusoma angalau kitabu kimoja kila mwezi na kwa mwaka utasoma vitabu siyo chini ya 10. Ukisoma vitabu kumi kila mwaka, ndani ya miaka 5, utakuwa ngazi za juu sana ukilinganisha na hapo ulipo.

Karibu kwenye program hii ya kusoma kurasa kumi kila siku. Kupata maelekezo jinsi ya kujiunga na programu hii, tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 wenye maneno KURASA KUMI. Muhimu ujumbe tuma kwa njia ya wasap pekee.

#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; SHERIA YA KUFANYA NA KUSEMA.

“If it is not right, do not do it, if it is not true, do not say it.” – Marcus Aurelius

Marcus Aurelius alikuwa mwanafalsafa wa ustoa na mtawala wa Dola ya Roma. Kupitia kitabu chake cha Meditations ametushirikisha mbinu mbalimbali za kuweza kuishi maisha yetu kwa mafanikio. Katika kauli yake hiyo hapo juu, anatukumbusha umuhimu wa kufanya na kusema yaliyo sahihi.

Angalia kwenye maisha, ni jambo la kushangaza namna ambavyo watu wanafanya mambo halafu baadaye wanakuja kuyajutia, au wanasema maneno ambayo baadaye wanatamani wasingeyasema. Sasa jiwekee sheria rahisi tu kufuata; KAMA KITU SIYO SAHIHI USIFANYE, KAMA JAMBO SIYO KWELI USISEME. Sheria fupi kama hiyo itakuepusha na matatizo mengi sana kwenye maisha yako.

#ZAWADI YANGU KWAKO; VITABU VIWILI VYA JAMES ALLEN.

Juma lililopita nilienda duka letu pendwa la vitabu, HOUSE OF WISDOM BOOKSHOP ambapo vitabu vingi vizuri vinapatikana. Nilikutana na kitabu kimoja kikubwa sana, chenye kurasa 866, kitabu hichi kina kazi zote ambazo James Allen aliwahi kuziandika kwenye maisha yake. Kitabu hichi kinaitwa MIND IS THE MASTER na kina vitabu 19 vya James Allen, nilipokishika tu mkononi, sikujiuliza mara mbili, bali nilikinunua mara moja. Nimefurahi sana kukipata kitabu hichi, kwa sababu ni hazina kubwa ya kuweza kuijua na kuitumia vizuri akili yako.

Sasa inakuja kwamba, huko nyuma nimewahi kununua vitabu viwili vya James Allen, ambavyo ni AS A MAN THINKETH na THE PATH OF PROSPERITY, ambacho nimekushirikisha leo. Sasa vitabu hivi vipo ndani ya kitabu hicho kikubwa, hivyo ni kama nakuwa navyo mara mbili. Sasa nimefikiria na kuona itakuwa sahihi kama vitabu hivi viwili nitavitoa zawadi kwako rafiki yangu, na hivyo ninafanya hilo.

photo_2018-02-18_17-05-44
Vitabu viwili vya juu ndiyo ninavyotoa zawadi.

Ninatoa zawadi ya vitabu hivi viwili, kimoja kwa kila mtu mmoja ambaye atafanya yafuatayo;

Kama siyo mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA basi ajiunge na KISIMA CHA MAARIFA, hapo nitampa kitabu kimoja kama zawadi, na nitakiandika zawadi kwenda kwake na kukiwekea sahihi kabisa. Kitabu utatumiwa popote ulipo Tanzania.

Kama tayari ni mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, basi atakayelipia COACHING PROGRAM atapata kitabu kimoja cha zawadi, na kama upo dar tutakapokutana kwa ajili ya coaching basi nitakukabidhi kitabu, na tutatumia angalau dakika kumi kujadili yale muhimu ya kufanyia kazi kutoka kwenye kitabu nitakachokupa kama zawadi. Kama upo mkoani nitakutumia kitabu nikiwa nimekiweka sahihi kama zawadi kwako.

Chukua hatua sasa kupata zawadi hiyo ya kitabu, zawadi itatolewa kwa anayewahi kuchukua hatua, hivyo wa kwanza kuchukua hatua anapata zawadi. Vitabu hivyo viwili vikishatoka na zoezi la zawadi linaishia hapo, ila huduma hizo nyingine zinaendelea.

Karibu sana rafiki upate zawadi hizi, zitakusaidia sana katika kutawala akili na mawazo yako ili kuweza kufanya makubwa. Kupata zawadi hiyo tuwasiliane kwa wasap namba 0717396253 ili kuingia kwenye moja ya huduma hizo na kupata zawadi hizo nzuri.

Nakutakia kila la kheri kwenye kulianza juma la nane, likawe juma la mafanikio makubwa kwako, kwa kuishi msingi wetu wa maisha ya mafanikio ambao ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog