Kuna watu wanafanya kazi ili waonekane wanafanya kazi. Watu wa aina hii kazi zao huwa ni za juu juu na hazina thamani kubwa. Kwa sababu pale ambapo hakuna anayewaona, basi hawana msukumo wa kufanya kazi. Na mara nyingi kazi inakuhitaji uifanye wakati hakuna anayekuona.
Wapo watu wanaofanya kazi ili wasifiwe, kwamba wanafanya kazi nzuri na ya maana. Hawa pia wanasukumwa kufanya kile ambacho watu wanaweza kukisifia. Lakini vitu vingi kwenye kazi zetu, huwa havianzi kwa mambo yanayoweza kusifiwa. Inakuhitaji muda wa kuweka juhudi ambazo hata hazionekani mpaka kufikia hatua ya kitu kinachoonekana.
Wapo pia wanaofanya kazi kwa sababu wanalipwa au kuna kitu wanapewa, hawa ni wale wa nipe nikupe, hunipi sikupi. Hawa wakilipwa kidogo wanafanya kidogo, na wakilipwa kikubwa wanafanya kikubwa. Sasa tatizo la hawa, huwa wanaishia kulipwa kidogo kwa sababu malipo makubwa huwa yanakuja baada ya kazi kubwa na siyo kabla.
Sababu zote tulizoainisha hapo juu za kufanya kazi, na nyingine zinazoendana na hizo, siyo sababu sahihi. Ni sababu ambazo haziwezi kukufikisha kwenye mafanikio makubwa, kukufanya wewe kuwa wa kipekee duniani. Ni sababu ambazo zinakuweka vizuri katikati ya kundi la watu, ambapo hakuna atakayekuona kwa upekee wowote.

Sababu kuu ya kufanya kazi yako inapaswa kuwa kufanya kazi yako. Yaani ifanye kazi kwa sababu umeamua kuifanya kazi hiyo, kwa sababu ni njia yako ya kuifanya dunia kuwa bora. Huangalii nani anaona au haoni, huangalii nani anakusifia au hakusifii na huangalii unalipwa kiasi gani. Wewe unafanya kazi, kwa sababu ni kitu ambacho umechagua kukifanya.
SOMA; UKURASA WA 1086; Kazi Na Biashara Ambayo Itaendelea Kulipa Zaidi Na Zaidi…
Na unafanya kwa ubora wa kipekee sana, ubora wa hali ya juu sana. hujaribu kutafuta njia za mkato wala kurahisisha kazi hizo. Badala yake unafanya kwa viwango vya juu, na kila siku unakazana kuwa bora sana. Kama ambavyo ng’ombe wanatoa maziwa, na miembe inatoa maembe bila ya kuangalia nani anasifia au anaona, hivyo pia ndivyo unapaswa kufanya kazi yako.
Cha kushangaza sasa, unapoanza kuifanya kazi yako kwa sababu ndiyo kazi umechagua kufanya, watu wanaona, watu wanakusifia na watu wanakulipa zaidi na zaidi. Kile ambacho hukipiganii, kinakuja chenyewe. Sasa kwa nini usiweke juhudi kubwa kwenye kufanya kazi yako?
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog