Whoever does not regard what he has as most ample wealth, is unhappy, though he be master of the world. – Epictetus

Hongera mwanamafanikio kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
TATUA, AMUA NA ONGOZA ndiyo mwongozo wetu kwa mwaka huu 2018, ambapo utatuwezesha kufanya makubwa.

Asubuhi ya leo tutafakari MTUMWA WA DUNIA…
Kuna watu ambao hata wapate kitu gani, wanaishia kuwa watumwa wa dunia.
Hata kama kwa nje wanaonekana wana mafanikio kiasi gani, ndani yao ni watumwa ambao wamejiweka kweye gereza kubwa na linalowazuia kuishi maisha ya uhuru.

Watu hawa ni wale ambao hawakubali na kuridhika na chochote wanachopata, au popote wanapofika.
Kila hatua wanayopiga, wanaona mbele zaidi na kusahau pale walipo. Wakifikia ile waliyokuwa wanaona wanazidi kuona mbele zaidi.

Hakuna ubaya wowote wa kutaka zaidi, au kupenda kupiga hatua zaidi, ni kitu kizuri kwa sababu ndiyo kinaleta maendeleo.
Lakini pale mtu anaposhindwa kuthamini pale alipo, anapokosa kuridhika na kile alichonacho, anajinyima kitu muhimu sana kweye maisha yake.
Anajinyima utulivu wa nafsi unaohitajika ili mtu kuweza kufurahia kila hatua na kunufaika nayo.

Kuthamini pale ulipo sasa haimanishi ndiyo umekubali kubaki hapo, bali kunamaanisha unaweza kupatumia vizuri kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako.
Na muhimu zaidi, popote unapotaka kwenda, utaanzia hapo ulipo sasa na siyo sehemu nyingine yoyote.

Kataa kuwa mtumwa wa dunia, kataa kukimbizana na kila hatua inayojitokeza mbele yako kabla hujaithamini ile hatua uliyofikia.
Thamini kila hatua unayopiga, na popote unapotaka kufika, jua utaanzia hapo ulipo sasa.

Ukawe na siku bora sana ya leo.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha