Habari rafiki?

Karibu kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufikia mafanikio makubwa. Hizi ni makala ambazo zinajibu changamoto mbalimbali ambazo tunakutana nazo na zinakuwa kikwazo kwenye safari yetu ya mafanikio.

Kwenye makala ye leo tutakwenda kuangalia njia tano za kupata mtaji wa kuanza au kukuza biashara yako bila ya kutumia mkopo.

Sijui watu tumetoa wapi hii kasumba, lakini kila ambaye anakosa mtaji wa biashara anakuambia hajapata mkopo au hakopesheki. Tumekuwa tunafikiria zaidi mikopo na hili linatuzuia kuziona njia mbadala za kupata mtaji ambazo zinatuzunguka.

Kabla hatujaangalia ni njia zipi mbadala tunaweza kutumia kupata mtaji wa biashara bila ya kuchukua mkopo, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Mahitaji Makubwa ya bidhaa mtaji kuwa mdogo. Taasisi za kutoa mikopo hazitoi mikopo bila dhamana ya kitu kisicho hamishika. Asante kwa ujenzi wa Taifa. – Julius M. N.

Kama alivyotuandikia msomaji mwenzetu Julius, wapo watu wengi ambao wamekwama kwenye hali kama yake. Wanataka kuanzisha au kukuza biashara zao, lakini hawana njia sahihi ya kupata mtaji. Wanafikiria kupata mkopo ambao kwa hali wanayokuwa nayo wanakuwa hawana sifa za kupata mkopo.

Lakini mkopo siyo njia pekee ya kupata mtaji wa biashara, zipo njia nyingine mbadala na za uhakika zaidi za kupata mtaji wa biashara ambazo mtu unaweza kuzitumia na zikakusaidia sana.

Kitu kingine muhimu cha kugusia hapa kabla hatujaingia kwenye njia za kupata mtaji, ni kwamba kwenye kuanza biashara, haishauriwi kuanza na mkopo. Hii ni kwa sababu mwanzo wa biashara una changamoto nyingi na mikopo inakutaka uanze kurejesha mara moja. Hivyo unapoanza biashara kwa mkopo, ni vigumu sana kufanikiwa.

Zifuatazo ni njia tano unazoweza kutumia kupata na kukuza mtaji wa biashara yako bila ya kuchukua mkopo.

  1. Fedha na akiba zako binafsi.

Hii ndiyo sehemu ya kwanza na muhimu sana ambayo kila mmoja wetu anaweza kuanzia. Japo wengi hawapendi kuitumia kwa sababu hawana subira na hawana nidhamu.

Fedha na akiba zako binafsi ni sehemu nzuri ya kuanzia kupata mtaji wa kuanza au kukuza biashara yako. Unachofanya hapa ni kuwa na njia yoyote ya kukuingizia kipato, kisha sehemu kubwa ya kipato hicho kuiweka akiba, ambayo baadaye utaitumia kama mtaji.

Hii ni njia ambayo itakuwezesha kuanza biashara yako kwa amani na bila ya usumbufu wowote.

Lakini pia njia hii ina changamoto kumbwa mbili, changamoto ya kwanza ni inakuchukua muda, hasa pale kipato chako kinapokuwa kidogo. Na hapo huna namna, lazima uwe na subira katika kukuza mtaji wako.

Changamoto ya pili ni kukosa nidhamu ya fedha, na hivyo kushindwa kutunza akiba unayojiwekea, hasa pale vinapotokea vitu vinavyokufanya utumie fedha uliyojiwekea akiba. Kutatua changamoto hii fungua akaunti maalumu ya kukusanya mtaji wako huo, ambayo huwezi kutoa fedha kwa kipindi fulani, kisha kila unapopata kipato, weka kwanza akiba kwenye akaunti hiyo kabla hata hujaanza matumizi.

Hakuna njia nzuri ya kuanza biashara kama kwa kuanza na mtaji ambao umekusanya mwenyewe. Hii itakupa uhuru wa kuweza kuiendesha biashara na kuikuza badala ya kuwa na wasiwasi wa utawezaje kurejesha mkopo hasa mwanzo wa biashara ambapo faida huwa ni ndogo au hakuna kabisa.

SOMA; Sababu Kumi (10) Kwa Nini Unapaswa Kuwa Na Biashara Mwaka Huu 2018.

  1. Michango ya ndugu, jamaa na marafiki.

Jamii zetu zimezoea michango ya sherehe kama harusi, ambapo mtu anaweza kuwasumbua watu mpaka wakatoa michango. Umekuwa ni utaratibu wa watu kudai michango ya harusi kwa nguvu kweli, kukumbusha kila mara kwa ujumbe na kuwafanya watu waahidi kiasi watakachochangia. Lakini inapokuja kwenye michango ya mambo ya maendeleo huwa watu hawapo tayari. Na wengi wamekuwa hawathubutu kuwabana watu kwenye michango ya maendeleo kama wanavyowabana kwenye michango ya harusi.

Unaweza kuwatumia ndugu, jamaa na marafiki kupata mchango wa kuanza au kukuza biashara yako. Unachohitaji hapa ni kuandaa vizuri wazo la biashara yako, na kuonesha ni kiasi gani cha fedha unahitaji. Kisha chagua watu wako wa karibu au unaojuana nao kama 100 hivi. Gawa kile kiwango unachohitaji kwa watu hao, kisha anza kuwasiliana na mmoja mmoja, na itakuwa vizuri kama utaonana nao ana kwa ana. Waeleze mpango wako wa biashara, kisha waombe kile kiasi ambacho ungependa wakuchangie. Kisha watake wakupe ahadi ya lini wanaweza kuwa wamepata na kukupa, kisha wakumbushe.

Kwa mfano kama unahitaji milioni tano, chagua watu 100 ambao unajua wanakujua kwa namna moja au nyingine, kisha gawa milioni 5 kwa 100 na utapata elfu 50, hapa sasa pata nafasi ya kukaa na kila mmoja kumwomba akuchangie hiyo elfu 50 au hata zaidi.

Ukiweza kujieleza vizuri kwa watu hao, na ukawapa muda, huku ukiendelea kuwakumbusha mara kwa mara, utashangaa jinsi ambavyo utapata mtaji wa biashara yako kwa njia ambayo hukutegemea.

  1. Weka wazo lako vizuri kisha tafuta wabia.

Wakati mwingine unaweza kuwa na wazo zuri sana la biashara, ambayo inaweza kuleta mabadiliko makubwa, na upo tayari kuifanyia kazi lakini umekwama kwenye mtaji. Wakati huo pia, kuna watu ambao wana fedha, lakini hawana muda wa kuendesha au kusimamia biashara, hivyo wameziweka tu hizi fedha.

Sasa unaweza kuingia kwenye ubia na watu wa aina hii, wao wakatoa mtaji na wewe ukatoa muda na wazo lako la biashara. Kwa namna hii utapata mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara yako bila ya kuwa na madeni. Wale unaoingia nao bia wanajua kabisa kwamba biashara ikifanikiwa na wao wanafanikiwa.

Kwenye hili unahitaji kuwa makini kwa wabia unaochagua, wawe watu wa kuaminika na ambao wapo tayari kusubiri biashara hiyo ifanye vizuri. Pia wewe binafsi unahitaji kujituma sana kuhakikisha biashara inafanya vizuri ili usije kuwaangusha wale wanaokuamini.

SOMA; Biashara Tano Unazoweza Kuanza Kufanya Mwaka 2017 Kwa Mtaji Kidogo Au Bila Ya Mtaji Kabisa.

  1. Tengeneza uaminifu kwa wateja na unaonunua kwao.

Kwenye biashara ipo dhana inayoitwa mali kauli. Siyo mara zote unapata mali unazotaka kwenye biashara kwa kulipia fedha taslimu, wakati mwingine kauli yako inakuwezesha kupata mali hata kama hujalipia fedha taslimu. Lakini hili linahitaji uaminifu wa hali ya juu sana kwa kila unayejihuisha naye kwenye biashara yako, kuanzia wateja wako na hata wale unaonunua mali kwao au wanaokusambazia.

Kwenye hili una nafasi mbili za kucheza, ya kwanza ni kuwashawishi wateja walipie kabla hawajapata kile wanachotaka, na hivyo kutumia fedha zao kununua au kuandaa kile wanachotaka. Hivyo ni kama wateja wanakukopesha ili uwape kile wanachotaka. Kama unaaminika na wateja wameshawahi kununua kwako na kufurahishwa na huduma zako hilo siyo zoezi gumu.

Nafasi ya pili ni kuwashawishi wale unaonunua mali kwao kukupa bila ya kulipa, kisha wewe kwenda kuuza na kuwalipa baada ya kuwa umeuza. Hili pia linahitaji uaminifu na wauzaji kuwa wameshakuzoea, kwa kuwa mnunuaji mzuri kwao.

Kwa vyovyote vile, iwe unahitaji kupata kitu au la, endesha biashara yako kwa misingi ya uaminifu na mambo mengi yatakuwa rahisi sana kwako.

095a5b996f7db11bfe3b1d93a17b444b.0

  1. Anza na biashara zisizohitaji mtaji mkubwa.

Kuna wakati una wazo la biashara fulani, ambayo unaipenda kweli, lakini kuianza unahitaji kuwa na mtaji mkubwa. Sasa siyo lazima uanze na biashara hiyo moja kwa moja, badala yake unaweza kuanza na biashara nyingine unayoweza kuanza kwa pale ulipo kwa wakati huo, kisha faida unayoipata unaiweka kwa ajili ya kuanza ile biashara ya ndoto yako.

Kwa mfano unaweza kuanza na biashara ambazo hazihitaji mtaji mkubwa kama biashara za kutoa huduma binafsi kama ushauri wa kitaalamu kama una utaalamu au uzoefu wa vitu fulani.

Pia unaweza kuanza na biashara kama ya mtandao (network marketing) na ikawa sehemu ya wewe kukusanya mtaji ili kuanza ile biashara ya ndoto yako.

Chochote unachoweza kutumia kuanza pale ulipo sasa, kitumie na weka akiba kwa ajili ya kuanza ile biashara ya ndoto yako. Hili linahitaji subira na uvumilivu kwa sababu ni njia ndefu, lakini kama huna njia nyingine ya kutumia, basi huna budi kuitumia.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kutatua Changamoto Ya Usimamizi Kwenye Kilimo Na Jinsi Ya Kupata Mtaji.

Tumia njia hizi tano kuweza kupata mtaji wa kuanza na kukuza biashara yako bila ya kuchukua mkopo. Wakati wowote unapohitaji mtaji wa biashara, usianze na kufikiria mikopo, bali anza kwa kufikiria njia zipi bora unazoweza kutumia kupata mtaji wa kuanza biashara. Uzuri ni kwamba, ukiangalia mazingira yako na hali yako vizuri, utaona njia nyingi unazoweza kutumia. Huenda kuna vitu unamiliki, ambavyo huvitumii, na unaweza kuviuza na kupata fedha, unaweza kuchukua hatua kama hiyo na ukapata mtaji.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog