Ni ndoto ya kila mtu kuingia kwenye biashara.

Kwa sababu biashara ndiyo njia ya kuingiza kipato ambayo inakupa uhuru mkubwa wa kuamua uingize kiasi gani.

Ukiwa umeajiriwa, mwajiri ndiyo anaamua ulipwe kiasi gani. Unaweza kuweka juhudi kubwa, lakini bado kipato kikabaki vile vile.

Ukiwa kwenye biashara yako mwenyewe, juhudi zako ndiyo zinaamua upate faida kiasi gani. Ukiweka juhudi kwenye masoko kupata wateja wengi na kwenye mauzo kwa kuwahudumia vizuri wateja, faida yako inaongezeka pia.

Pamoja na umuhimu huu wa biashara, bado wengi wamekuwa wanashindwa kuanza biashara wanazotaka. Zipo sababu nyingi ambazo watu huwa wanazitaja, lakini kubwa kabisa ni ya mtaji.

Wengi hueleza jinsi wanavyokosa mtaji wa kuanza biashara wanazopanga kuanza. Katika hao wanaotumia mtaji kama sababu, sehemu kubwa siyo kwamba hawana fedha kabisa, ila wanachokosa ni nidhamu ya kukusanya mtaji wa kuanza biashara zao.

Hebu fikiria mtu ambaye kwa miaka mitano amekuwa anasema anataka kuanza biashara ila hana mtaji. Lakini kwenye miaka hiyo mitano anakula, anavaa, anastarehe, ana simu ambayo anaweka vocha na mahitaji mengine ya maisha yanaendelea.

Ni kwenye kuanza biashara tu ndiyo anakuwa hana mtaji, lakini mengine ya maisha yanaendelea.

Hii ndiyo sababu imekuwa inafanya msimamo wangu kwenye hilo kuwa huu; watu wanatumia sababu ya kukosa mtaji kuficha hofu yao ya kuingia kwenye biashara. Kwani mtu mwenye ujasiri, anaweza kuingia kwenye biashara wakati wowote, iwe ana mtaji au la na akafanya vizuri tu.

Lakini pia wapo ambao wana nia kabisa ya kukusanya mtaji wa biashara, lakini kukosa nidhamu ya fedha kunakuwa kikwazo kwao. Hawa ndiyo wanakwenda kupata ushauri leo wa namna ya kujijengea nidhamu hiyo na kukusanya mtaji wa kuwawezesha kuingia kwenye biashara.

Kabla hatujapata ushauri wa hatua za kuchukua, hapa ni maoni ya wale walioomba ushauri kwenye hili;

Nahitaji kufungua biashara ya stationary lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa mtaji,  pia nafanya kazi ya kujitolea sehemu ili kupata mtaji huo na kila nikijitahidi kuweka akiba inayotosheleza biashara hiyo nashindwa.  Msaada tafadhali. – Grishen M.

Kila nikipata milioni moja mawazo yanagongana, nataka kufanya kila biashara hivyo hujikuta hela yote imeisha bila kujua. Hali hii inanitesa sana. – Dick M. K.

Mimi Nina shida kwenye eneo la fedha jambo linalonifanya kutokufikia malengo. Ninapopata fedha najikuta naitumia nje ya malengo yangu naomba ushauri nifanyeje ili niweze kutoka kwenye eneo hili? – Lucas S. K.

Changamoto yangu inalenga sana kwenye msukumo wa kuchukua hatua, muda mwingine nakuwa na hamasa kubwa kwamba mshahala wangu wa mwezi ujao lazima niutumie kwa kuanzisha biashara lakini muda na wakati ukifika ambao nilipanga kuanzisha biashara najikuta pesa yote imekuwa na matumizi mengi kiasi kwamba naishiwa pesa na kubaki Sina kitu. – Magafu M. P.

Kutoka kwenye maoni ya wasomaji wenzetu, tunaona jinsi hiyo ilivyo changamoto kubwa, kukusanya mtaji na hata ukishaukusanya kuutumia vizuri.

Nidhamu ya fedha imekuwa changamoto kubwa kwa wengi, na inapoingia kwenye biashara inakuwa na madhara makubwa zaidi.

Hapa kuna hatua tano za kufuata katika kujijengea nidhamu itakayokuwezesha kukusanya mtaji na kuingia kwenye biashara.

Hatua ya kwanza; jua ni biashara gani unataka kufanya.

Usianze kukusanya mtaji halafu ndiyo uje utafute biashara gani ya kufanya. Ukianza hivyo unakuwa umeshakosea na hutakusanya mtaji na hata ukifanikiwa kuukusanya, utajikuta unautumia kwenye mambo mengine.

Anza kwa kuchagua ni biashara gani unayotaka kufanya, biashara inayotoka kweli ndani yako na siyo ile ya kuiga kwa wengine kwa sababu umeona wanafanya au umesikia inalipa sana.

Umuhimu wa kuanza kwa kujua biashara gani na biashara hiyo kuwa kitu unachopenda ni inakupa msukumo mkubwa wa kuendelea kukusanya mtaji.

Sisi binadamu huwa tupo tayari kuteseka pale tunapojua kwa nini tuteseke. Unapochagua biashara unayoipenda kweli na inatoka ndani yako, kukusanya mtaji hakutakuwa tabu kwako. Hata unaposhawishika kutumia fedha hizo kwa mambo mengine, ukikumbuka biashara unayoipenda, hutafanya hivyo.

SOMA; Usisingizie Mtaji Tena; Kama Hujaingia Kwenye Biashara Tatizo Siyo Mtaji, Bali Tatizo Ni Wewe.

Hatua ya pili; angalia ngazi ndogo kabisa unayoweza kuanzia.

Ukisema usubiri mpaka upate mtaji wa kuingia kwenye biashara unayotaka kwa viwango vya juu hutaweza, itakuchukua muda mrefu.

Hivyo unapaswa kuigawa biashara hiyo mpaka ufike ngazi ya chini kabisa unayoweza kuanza biashara hiyo. Katika ngazi hiyo ya chini, hata ukiwa na mtaji kidogo unaweza kuingia na kufanya.

Lengo ni uingie kwenye biashara hiyo mapema na kujifunza wakati umewekeza mtaji kidogo. Kwa njia hiyo utajifunza na kukua vizuri kwenye biashara bila kupoteza mtaji wako mwingi.

Kila biashara unaweza kuanza na hatua ya chini kabisa na ukakua kadiri muda unakwenda. Kama unataka kuwa na kampuni ya usafirishaji, kabla hujafika kwenye magari unaweza kuanza na bodaboda. Kama unataka kuwa na hospitali unaweza kuanza na maabara. Kama unataka kuwa na shule unaweza kuanza na kituo cha watoto. Kabla hujapanga eneo la kuweka biashara yako unaweza kufanya kwa kutembeza au kutumia mtandao.

Angalia wapi unaweza kuanzia na kisha hilo liwe ndiyo lengo unalopigania.

Hatua ya tatu; jua mtaji unaohitaji kuanzia ngazi ya chini.

Baada ya kujua ngazi ya chini kabisa unayoweza kuanzia biashara unayotaka, sasa unapaswa kujua kiasi cha mtaji kitakachokutosha kuanza.

Hii ndiyo namba muhimu ambayo utaanza kuifanyia kazi mara moja ili uweze kuingia kwenye biashara uliyopanga.

Lazima ujue ni kiasi gani cha mtaji unakihitaji na pia upange utakusanya mtaji huo ndani ya muda gani ili uweze kuingia kwenye biashara.

Hatua ya nne; chagua mahali unatunza mtaji unaokusanya.

Umeshajua kiasi gani unahitaji ili biashara iweze kuanza, sasa unapaswa kuchagua wapi utatunza mtaji huo.

Unachopaswa kujua ni kwamba fedha ukiwa nayo karibu huwa haikosi matumizi, mahitaji mbalimbali yanayoonekana muhimu yatajitokeza na kukushawishi utumie fedha hiyo.

Hapa ndipo nidhamu ya hali ya juu sana inapohitajika ili uweze kufikia lengo lako la kuingia kwenye biashara.

Kwanza kabisa jua biashara ndiyo kitu muhimu na kipaumbele cha kwanza kabla ya vitu vingine vyovyote. Hata kama unalala njaa, usione kula kwa siku moja ni muhimu kuliko biashara. Lazima uweke kipaumbele cha kwanza kabisa kwenye kukusanya mtaji wa biashara yako.

Pili weka mtaji huo sehemu ambayo siyo rahisi kuutoa na kuutumia. Kama unaweka fedha ndani au kwenye akaunti yako ya kawaida benki unajidanganya, ni rahisi kutoa na kujidanganya utarudisha. Badala yake tengeneza gereza ambalo huwezi kufikia. Benki nyingi wana aina za akaunti ambazo unaweza kuweka fedha ila kutoa wanakuwekea ukomo kwa kipindi fulani. Fungua akaunti za aina hii na kusanya mtaji wako huko.

Usiruhusu chochote kiingilie zoezi la kukusanya mtaji.

Fanya kila shughuli unayoweza, kama umeajiriwa fanya na kazi za ziada, kama huna ajira tafuta kila aina ya kibarua na sehemu kubwa ya kipato chako weka kwenye akiba yako ya kukusanya mtaji. Kila fedha unayoipata ambayo hukuitarajia, moja kwa moja ipeleke kwenye akiba ya mtaji.

Ukiwa umejitoa kweli na ukawa na nidhamu ya uhakika, mwaka mmoja unakutosha kukusanya mtaji wa kukuwezesha kuanza biashara unayotaka kuanza.

SOMA; USHAURI; Njia Tano Za Kupata Mtaji Wa Biashara Bila Ya Kuchukua Mkopo.

Hatua ya tano; mtaji unapokamilika ingia kwenye biashara uliyopanga na siyo nyingine.

Unaweza kujijengea nidhamu kubwa na ukakusanya mtaji wako, lakini kuna kitu kitatokea pale ambapo tayari una mtaji, utaziona fursa nyingine nzuri zaidi za biashara, ambazo ukiweka mtaji wako utapata faida kubwa na ya haraka.

Ulikuwa unakusanya mtaji wako wa milioni mbili ili upate bodaboda ya kuanzia biashara kwa lengo la kukua na ufike kwenye biashara ya usafirishaji. Umepata milioni yako mbili na unasikia watu wanasema ukienda kulima tikiti, ukiweka milioni mbili kwenye heka moja, unavuna milioni 10.

Kwa kusikia hivyo masikio yanakusimama, unaona mambo si ndiyo hayo, badala ya kununua pikipiki moja utanunua tano kabisa. Au utaachana kabisa na kununua pikipiki na utaenda moja kwa moja kununua teksi au kirikuu na hivyo utakuwa umevuka hatua kubwa.

Unaweka mtaji wako wa milioni 2 kwenye kilimo cha matikiti na unakuja kuvuna laki 5. Umepoteza kila kitu.

Ukishakamilisha mtaji uliokusanya, utumie kwenye mpango ulioweka tangu awali. Usishawishike na mpango mwingine wowote, hata kama unauona ni mzuri kiasi gani. Mpango unaoukusanyia mtaji umeshaufikiria muda mrefu, unaujua vizuri na huo ndiyo unapaswa kuingia.

Hapo panahitaji nidhamu kubwa sana maana ukiwa na fedha, kila wazo litakuja kwako na kuonekana ni zuri. Wewe komaa na wazo uliloanza nalo mwanzo, mengine achana nayo kwa sasa.

Muhimu zaidi; jifunze tangu siku ya kwanza na bila ukomo.

Tangu ulipochagua aina ya biashara unayotaka kuingia, hapo umeanza darasa la maisha yako. Kila siku jifunze kuhusu biashara hiyo na biashara kwa ujumla. Tafuta mafunzo mbalimbali mitandaoni, soma vitabu vya biashara na tembelea maeneo ambayo biashara hiyo inafanywa na jifunze kwa kuangalia watu wanavyofanya au kwa kuwauliza.

Kama una nafasi, omba kufanya kazi hata kwa muda wa ziada kwenye biashara inayoendana na ile unayotaka kufungua. Ukiwa ndani utajifunza mengi ambayo huwezi kuyaona kwa nje.

Kadiri unavyojifunza kwa karibu, ndivyo unavyoielewa biashara zaidi na kupata hamasa ya kuingia.

Zingatia hatua hizi tulizojifunza hapa na utaweza kukusanya mtaji na kuingia kwenye biashara ya ndoto zako bila ya kuwa na kikwazo chochote.

Hakikisha pia unasoma vitabu hivi viwili, ambavyo vitakusaidia mno. Kwenye nidhamu ya fedha soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA FEDHA. Na kwenye nidhamu ya biashara, kuanzia kujua wazo sahihi kwako na njia mbalimbali za kupata mtaji soma kitabu cha ELIMU YA MSINGI YA BIASHARA. Kupata vitabu hivyo wasiliana na 0752 977 170 na utatumiwa au kuletewa kitabu ulipo.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania

Rafiki, karibu upate na kusoma vitabu vizuri vya maendeleo binafsi na mafanikio kwa lugha ya Kiswahili. Pakua na weka app ya SOMA VITABU na upate maarifa sahihi. Kwa maelezo zaidi fungua; https://amkamtanzania.com/somavitabuapp