Kupata chochote unachotaka, unahitajika kutoa kitu fulani, kwa lugha nyingine, ili upate lazima upoteze. Na kadiri unavyotaka vitu vikubwa, ndivyo unavyohitaji kupoteza vitu vikubwa zaidi.
Hii ndiyo sababu wakati mwingine unakiacha kitanda mapema, kabla hata ya usingizi kuisha, ili kuwahi kwenye shughuli zako kwa sababu unahitaji kupiga hatua fulani.
Hivyo hakuna wasiwasi kwamba kuna kitu cha kutoa, kitu cha kupoteza. Swali muhimu sana kujiuliza ni je kipi upo tayari kupoteza?

Kwa sababu siyo kila kitu kinafaa kupoteza ili upate kile unachotaka. Kwa mfano kama unataka kufanikiwa, lakini inakutaka kuchukua hatua ambazo zitakuwa hatari kwa maisha yako, siyo sahihi kupoteza afya ili kupata mafanikio.
Hivyo kila mmoja wetu anahitaji kuwa na njia ya kujua vitu gani yupo tayari kupoteza na vipi hawezi kupoteza hata iweje.
SOMA; UKURASA WA 1021; Watu Watakaa Upande Wanaotaka Kukaa…
Na njia hii ni kujua kwanza vitu gani unavyothamini sana kwenye maisha yako. Weka vipaumbele kwa yale maeneo muhimu ya maisha yako, kama afya, mahusiano na hata uhuru binafsi.
Kisha yafanye maeneo haya kuwa ya kipekee na usikubali kabisa kupoteza kwenye maeneo hayo. Yale mengine ambayo siyo kipaumbele, unaweza kupoteza ili kuweza kufika kule unakotaka kufika.
Kwa mfano kama unahitaji muda zaidi kwenye shughuli zako, na kwa kuwa muda wa siku ni masaa 24 pekee, unahitaji kuondoa muda kwenye maeneo fulani na kuupeleka kwenye shughuli zako. Wengi hukimbilia kuondoa muda kwenye kulala au muda na watu ambao ni wa muhimu kwao. Lakini watu hao hao utawakuta wakizurura kwenye mitandao ya kijamii, wakifuatilia habari na hata kuingia kwenye mabishano na wengine? Hapo ndiyo utaona kwamba watu hawa hawajaweka vipaumbele vyao vizuri. Kama mtu wa aina hii, ataacha kabisa kuzurura kwenye mitandao ya kijamii, akaacha kabisa kufuatilia habari, akaondokana na kila aina ya mabishano yasiyo na msingi, atakuwa na muda mwingi wa kufanya mambo yake na bado akapata muda wa kulala na hata kuwa na wale wa muhimu kwake.
Jua vitu gani vina thamani zaidi kwenye maisha yako, kisha vipe kipaumbele na usivipoteze katika safari yako ya mafanikio.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog