Tangu uwekezaji kwenye masoko ya mitaji umeanza kufanywa kitaalamu, yaani kuwepo kwa taasisi zinazoajiri watu wenye uelewa mkubwa kwenye uwekezaji, uwekezaji umekuwa mgumu sana. Uwekezaji kwenye masoko ya mitaji umekuwa mchezo wa kushindwa kwa sababu watu wanaoshiriki mchezo huu wote wana uwezo mkubwa na ili mmoja afanikiwe, lazima mwingine ashindwe.

Na hii yote imetokana na kitu kimoja ambacho wawekezaji wengi wamekuwa wanajidanganya, kwamba wanazo mbinu za kupata mafanikio makubwa kwenye uwekezaji kuliko wengine. Na kweli wakipata mbinu hizo, haiwachukui muda wawekezaji wengine kuzijua, na sehemu kubwa ya mbinu hizo ni kutegemea wengine wakosee.

Uwekezaji pia umekuwa mgumu kwa sababu ya watu kufanya maamuzi ya kuwekeza kwa hisia. Na hisia mbili ambazo zimewagharimu watu kwenye uwekezaji ni hofu na tamaa. Pale ambapo hisa zinapanda bei, watu huhamasika kununua, na hivyo kununua kwa wingi, na hivyo bei kuongezeka. Hapa wengi wananunua hisa kwa bei juu. Hisa zikianza kushuka bei hofu inawaingia watu na kuanza kuuza wakiepuka kupata hasara, kadiri wanavyouza bei inashuka zaidi na hivyo wengi kuuza kwa bei ndogo. Hivyo mtu ananunua hisa kwa bei juu na kuuza kwa bei chini, haihitaji shahada ya uchumi au biashara kujua kwamba ukinunua kitu kwa bei kubwa na ukauza kwa bei ndogo unapata hasara.

Mwandishi na mwekezaji Charley Ellis amekuwa akiandika miongozo ya uwekezaji kwa muda mrefu na kupitia ufuatiliaji wake wa masoko ya mitaji, ameona makosa ambayo wengi wanafanya kwenye uwekezaji.

Kupitia kitabu chake hichi cha WINNING THE LOSER’S GAME, Charley anatuonesha ni namna gani tunaweza kushinda na kufanikiwa kupitia uwekezaji, kwa kutushirikisha misingi isiyopitwa na wakati ya mafanikio kwenye uwekezaji.

winning losers game

Tatizo kubwa la uwekezaji ni watu kulaghaiwa na vitu vinavyoonekana ni vipya. Na kwa upya huo wa vitu, watu wanafikiri misingi ya zamani haifanyi kazi tena. Hapo ndipo wanafanya makosa ambayo yanawagharimu sana. Hayo yalitokea kuanzia mdororo wa uchumi wa mwaka 1929, kuanguka kwa hisa za teknolojia miaka ya 2000 na hata mdororo wa uchumi wa mwaka 2008 uliosumbua sana nchini Marekani.

Karibu kwenye uchambuzi wa kitabu hichi cha WINNING THE LOSER’S GAME, tujifunze mbinu za kushinda kwenye mchezo huu unaozidi kuwa mgumu na wa kushindwa kadiri siku zinavyokwenda.

MCHEZO WA KUSHINDWA.

Uwekezaji umekuwa unachukuliwa kama mchezo wa kushindwa kwa sababu watu wengi wanaoshiriki ni wataalamu na njia pekee ya kushinda ni kutegemea wawekezaji wengine washindwe.

 1. Changamoto kubwa inayokumba uwekezaji kwa sasa ni kwamba uwekezaji nafanya na taasisi zenye wataalamu wa uwekezaji. Zamani wakati soko la hisa linaanzishwa nchini marekani, asilimia 95 ya wawekezaji walikuwa watu binafsi yaani mtu mmoja mmoja na asilimia 5 ilikuwa ni taasisi za uwekezaji. Lakini sasa hivi asilimia 95 ya uwekezaji inafanywa na taasisi za uwekezaji, na asilimia tano tu ndiyo unafanya na mtu mmoja mmoja. Kitu ambacho kimefanya uwekezaji kuwa mgumu baina ya taasisi na kuwa mgumu zaidi kwa mtu mmoja mmoja.
 2. Wawekezaji wengi wamekuwa wakiamini kwamba wanaweza kulizidi soko la uwekezaji. Kwamba kwa mbinu zao wanaweza kupata faida kubwa kuliko wawekezaji wengine wanavyoweza kupata. Kwa mfano kama wastani wa ukuaji wa thamani ya hisa kwa mwaka ni asilimia 10, basi wapo wawekezaji ambao wamekuwa wanawaaminisha watu kwamba wana uwezo wa kupata zaidi ya asilimia 10 kwa mwaka. Kitu ambacho kwa kuangalia taarifa za miaka mingi siyo kweli. Wapo wawekezaji ambao wameweza kupata zaidi ya wastani wa soko mara moja moja, lakini siyo mara zote. Kibaya zaidi, mwekezaji anayepata zaidi ya soko mara moja au mara chache, kipindi kinachofuata anapata faida ya chini kuliko soko, hivyo ukitafuta wastani unakuta anarudi kwenye wastani wa soko au mara nyingi chini ya wastani wa soko.
 3. Ni vigumu kwa mwekezaji kupata faida zaidi ya wastani wa soko kwa muda mrefu kwa sababu ili apate faida hiyo anahitaji kutumia mwanya wa makosa ya wawekezaji wengine. Kitu ambacho siyo rahisi kwenye zama hizi ambazo uwekezaji mkubwa unafanya na taasisi zenye watu wenye elimu na uwezo mkubwa kwenye uwekezaji. Hivyo kinachotokea ni kila mtu kutumia uwezo wake kujaribu kumpiku mwenzake na mwishowe wote kupata hasara na hivyo kuwa mchezo wa kushindwa.
 4. Sababu kubwa inayopelekea uwekezaji kuwa mchezo wa kushindwa kwa wawekezaji ni wao kuwa tatizo kwenye mchezo huo. Pale kila mtu anapotafuta mbinu za kupata faida kubwa kuliko wastani wa faida wa soko, wanajikuta wakifanya vitu vingi ambavyo havizalishi. Kwa mfano kuuza na kununua hisa mara kwa mara wakilenga kupata hisa zinazofanya vizuri, kunawaingiza kwenye gharama za kodi wakati wa kuuza, hivyo hata kama watapata faida, inaishia kwenye gharama za kuuza na kununua.
 5. Suluhisho kubwa la wawekezaji kuondoka kwenye mchezo huu wa kushindwa ni kuwa na sera ya uwekezaji ambayo wataenda nayo wakati wote wa uwekezaji. Tatizo kubwa halipo kwenye kuwa na sera, bali tatizo lipo kwenye kuishi na sera hiyo pale ambapo mabadiliko ya soko yanavutia kuuza au kununua. Hapa ndipo wengi hufanya maamuzi ambayo huishia kuwagharimu.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; The Warreb Buffett Way (Misingi Ya Uwekezaji Ya Mwekezaji Mwenye Mafanikio Makubwa Warren Buffett)

MCHEZO WA KUSHINDA.

Tumeona jinsi ambavyo juhudi za wawekezaji, hasa taasisi zinavyofanya uwekezaji kuwa mchezo wa kushindwa. Kwa kuwa tumeshajua wapi kunapelekea watu kushindwa, ni rahisi sasa kufanya uwekezaji kuwa mchezo wa kushinda.

 1. Njia ya uhakika ya kufanikiwa kwenye uwekezaji siyo kukazana kulishinda soko, bali kuwekeza kwa muda mrefu, ukiamini kwamba ndani ya muda mrefu, soko litakuwa na kuzalisha thamani. Data zimekuwa zinaonesha kwamba kwa miaka mingi, licha ya kupanda na kushuka kwa soko la hisa, kwa wastani soko limekuwa linapanda kwa silimia 10. Hivyo kama mtu atawekeza kwa muda mrefu, ataibuka mshindi na hatakuwa na tatizo la kuhangaika na mabadiliko ya muda mfupi kwenye soko.
 2. Kabla ya mtu kuwekeza anapaswa kuelewa hatari iliyopo kwenye uwekezaji, kuweka mipango ambayo inaendana na hali ya uwekezaji, kuchagua aina ya uwekezaji ambao unamfaa kulingana na hali yake na kuwa na sera ya uwekezaji ambayo ataifuata na kuepuka kuendeshwa na hisia kwenye maamuzi ya uwekezaji. Hii ni hatua muhimu sana ya mtu kuchukua kabla hajaingia kwenye uwekezaji ili asiwe mtu wa kupoteza.
 3. Pia mtu anapaswa kujijua yeye mwenyewe, hasa kwa kiwango cha hatari ambacho anaweza kumudu kuchukua hatua. Kiwango cha hatari ambacho mtu anaweza kuvumilia kinatofautiana baina ya watu. Hivyo kwa mtu kujijua vizuri, kisha kuchagua uwekezaji unaoendana naye kutampa amani ya moyo na utulivu pia.
 4. Kwa kuwa soko la hisa, hasa kwa nchi kama marekani lina hisa nyingi sana za kununua, ni vigumu mtu kujua hisa zipi anaweza kuchagua za kununua. Na kwa mtu mmoja mmoja haishauriwi kuanza kuchagua hisa za kununua, badala yake imekuwa inashauriwa mtu kuwekeza kwenye mfuko unaofuata soko. Kwa nchi za wenzetu mifuko hii inaitwa INDEX FUND, ambapo inajumuisha zile hisa zinazofanya vizuri kwenye soko. Hivyo wewe mwekezaji huhitaji kuchagua hisa zipi ununue, kwa kuwekeza kwenye mfuko huo, unakuwa unaenda sawa na soko, kwa sababu unakuwa unanunua moja kwa moja zile hisa ambazo zinafanya vizuri kwenye soko.
 5. Uzuri wa mfuko wa uwekezaji kwenye soko ni kwamba hauingii gharama kubwa za kuendesha uwekezaji kama ungekuwa unanunua na kuuza kila hisa wewe mwenyewe. Na pia huwezi kupata hasara kabisa, kwa sababu ndani ya mfuko huo, siyo rahisi hisa zote kushuka kwa wakati mmoja. Hivyo hisa chache zikishuka, nyingine zinapanda, hivyo kwa wastani unabaki kuwa na faida.

DHANA YA KULISHINDA SOKO KWENYE UWEKEZAJI.

Kumekuwa na dhana kwamba baadhi ya wawekezaji wanaweza kulishinda soko, kwa kupata faida kubwa kuliko wastani wa soko. Dhana hii ni uongo na imewapelekea wengi kupata hasara kuliko wale wanaotulia na uwekezaji mmoja.

 1. Njia pekee ya mwekezaji kulishinda soko, ni kutafuta makosa ya wengine na kunufaika nayo. Sasa hii siyo mbinu ya kudumu kwa sababu mwisho wa siku wale wanaofanya makosa wanagundua. Pia ili kulizidi soko, inawabidi wawekezaji kuuza na kununua hisa mara nyingi, kitu ambacho kinafanya gharama kuwa kubwa sana.
 2. Wawekezaji wanaojaribu kulizidi soko wamekuwa wanatumia njia hizi nne, ambazo zote huwa zinashindwa;

Njia ya kwanza ni kutabiri na kuotea soko, hapa wawekezaji wanajaribu kununua hisa kabla hazijapanda bei na kuuza kabla hazijashuka bei. Njia huu hushindwa kwa sababu hakuna mwenye uwezo wa kutabiri soko kwa uhakika.

Njia ya pili ni kuchagua hisa chache ambazo wanajua zitafanya vizuri, hii pia hushindwa kwa sababu hakuna hisa chache zinazofanya vizuri nyakati zote.

Njia ya tatu ni kufanya mabadiliko kwenye mpango wa uwekezaji kwa muda, kitu ambacho siyo rahisi kufanya kwa wakati.

Njia ya nne ni kuwa na sera thabiti ya uwekezaji ambayo mtu anaifuata wakati wote. Hii ndiyo njia ya uhakika, lakini wengi huwa hawawezi kuitekeleza kwa sababu inalenga mafanikio ya muda mrefu na siyo muda mfupi.

 1. Njia moja ya kuongeza uwezekano wa kufanikiwa kupitia uwekezaji ni kupunguza makosa ambayo mtu unaweza kufanya. Na wengi hufanya makosa kwa njia mbili, njia ya kwanza ni kukazana sana, kufanya vitu vingi ili kupata faida, na kuishia kupata hasara. Njia ya pili ni kutokuchukua hatua kwa wakati na hivyo kupata hasara, hawa wawekezaji wanakazana kutokufanya makosa na hilo linawagharimu.
 2. Wawekezaji wenye mafanikio wanaijua na kuiishi misingi hii minne ya uwekezaji;

Moja; maamuzi sahihi kwenye uwekezaji ni kuchagua kuwekeza kwa muda mrefu na kuwa na mchanganyiko kwenye uwekezaji wa hisa, hatifungani na uwekezaji kwenye mali.

Mbili; mchanganyiko wa uwekezaji unapaswa kufanywa kwa kuzingatia ukuaji, usalama na kipato kinachotokana na uwekezaji huo.

Tatu; kuhakikisha mchanganyiko huo wa uwekezaji unasambaa kwenye maeneo mbalimbali, ili eneo moja likipata shida uwekezaji wako wote usiwe hasara.

Nne; kuwa mtulivu na king’ang’anizi, mambo mazuri huwa hayahitaji haraka na hasa kwenye uwekezaji.

SOMA; Kama Haupo Tayari Kuwekeza Kwenye Mambo Haya Matatu, Sahau Kuhusu Mafanikio.

SOKO NA THAMANI.

Kuna nguvu kuu mbili zinazoendesha soko la hisa, nguvu hizo ni SOKO na THAMANI. Nguvu ya soko ni kupanda na kushuka kwa bei ya hisa kunakotokea mata kwa mara na kwa muda mfupi, na nguvu ya  thamani ni ile thamani inayoongezeka kwenye uwekezaji ambao mtu anafanya.

 1. Nguvu ya soko ni ya muda mfupi na imekuwa inawaingiza watu kwenye matatizo. Kupanda na kushuka kwa hisa kumewaingiza watu wengi kwenye matatizo ya uwekezaji, hasa pale wanapokimbilia kununua bei inapopanda na kuuza pale bei inaposhuka. Unapaswa kukaa mbali na nguvu hii ya soko kwa sababu ukienda nayo itakuletea hasara.
 2. Nguvu ya thamani ni ya muda mrefu na inachukua muda kuonekana. Pamoja na kupanda na kushuka kwa bei za hisa, ndani ya muda mrefu, thamani ya hisa inaongezeka. Hivyo kama ukinunua hisa na kukaa nazo kwa muda mrefu, bei yake inakuwa kubwa na hivyo ukiuza unapata faida ya uhakika.
 3. Changamoto kubwa kwenye uwekezaji hailetwi na nguvu ya soko bali inatokana na hisia ambazo watu wanakuwa nazo. Pale soko linapopanda na kushuka, ni vigumu sana mtu kutulia na kusubiri thamani ikue. Wengi huona wasipochukua hatua watapata hasara, na hivyo wanakimbilia kuchukua hatua, kitu ambacho kinawaingiza kwenye hasara kubwa.

Ili kushinda hisia, ni muhimu sana wewe kama mwekezaji kujijua mwenyewe kisha kujijengea mazingira ambayo hisia hazitakuwa kikwazo kwako.

SOMA; Zifahamu Hatua Muhimu Za Uwekezaji Wa Ardhi Na Majengo, Je Upo Hatua Gani Kuelekea Mafanikio Yako?

TIMU BORA KWA KILA MWEKEZAJI.

Taasisi za uwekezaji zina faida ya kuwa na timu kubwa za uwekezaji, watu ambao wana uelewa mkubwa kwenye uwekezaji. Je kama ungeweza kuwa na timu bora ya washauri kwenye uwekezaji si ungenufaika sana!

 1. Njia pekee ya wewe kama mwekezaji kuwa na timu nzuri ya kukusaidia kwenye uwekezaji ni kuwekeza kwenye mfuko wa soko (index fund). Kwa kuwekeza kwenye mfuko huo, unanufaika na kazi za wengine ambao wanachagua hisa zipi za kununua au kuuza. Wewe unaenda na jinsi soko linavyoenda hata kama huna uelewa mkubwa kwenye uwekezaji.
 2. Zipo faida nyingi za kuwekeza kwenye mfuko wa soko la hisa. Na hizi ni baadhi ya faida hizo;

Moja; kodi inayokatwa kwenye uwekezaji wa mfuko wa soko ni ndogo.

Mbili; unaepuka gharama za kununua na kuuza hisa moja moja.

Tatu; utulivu wa akili, wakati wengine wanahangaika pale soko linapopanda au kushuka, wewe kwa wastani unakuwa unapata faida.

 1. Zipo hatari kuu mbili kwenye uwekezaji;

Hatari ya kwanza ni hatari ya uwekezaji wenyewe, hii ni ile hatari ambayo inatokana na uwekezaji ambao mtu anafanya. Kwa mfano kununua hisa halafu zikashuka thamani au kampuni ikafilisika.

Hatari ya pili ni hatari ya MWEKEZAJI MWENYWE, hii ni ile hatari inayotokana na maamuzi anayochukua mwekezaji. Kwa mfano kununua kwa kuwa bei inapanda na kuuza kwa kuwa bei inashuka, kitu kinachopelekea mtu kupata hasara.

Hatari ya kwanza ndiyo wengi huhangaika nayo, lakini kusahau hatari ya pili, ambayo watu wanakuwa nayo na inawazuia sana kufanikiwa kwenye uwekezaji.

 1. Bila ya kujijua wewe mwenyewe, soko la hisa ni sehemu hatari sana ya kuwepo. Hii ni kwa sababu sisi binadamu ni viumbe tunaoongozwa kwa hisia na hisia siyo nzuri kwenye uwekezaji. Hivyo jijue kwanza wewe mwenyewe kabla hujajihusisha na uwekezaji.
 2. Muda ndiyo nguvu kubwa ya kufanikiwa kwenye uwekezaji. Unapochagua uwekezaji wako vizuri, mfano kuwekeza kwenye mfuko wa soko au mifuko mingine ya uwekezaji, kisha ukajipa muda kwa uwekezaji wako kukua, unanufaika sana. Na kama uwekezaji unakua kwa riba mkusanyiko (compound interest) basi kadiri muda unavyokwenda unanufaika maradufu.
 3. Marejesho kwenye uwekezaji huja kwa njia mbili. Njia ya kwanza ni inayotabirika ambapo ni kupata gawio au riba kutokana na uwekezaji uliofanya. Njia ya pili ni isiyotabirika ambayo ni kupanda na kushuka kwa thamani ya uwekezaji kwenye soko. Kama mwekezaji unahitaji kuangalia zaidi njia ya kwanza ambayo ni ya uhakika na unayoweza kuipata kwa muda mrefu. Usisukumwe kuchukua hatua kutokana na njia ya pili ambayo siyo ya uhakika na haidumu.
 4. Uwekezaji wenye marejesho ya uhakika kama hatifungani huwa unakuwa na riba ndogo ukilinganisha na uwekezaji usiokuwa na marejesho ya uhakika kama hisa huwa na riba kubwa lakini pia unaweza kuwa na hasara kubwa pia. Hivyo unapopanga uwekezaji wako, hakikisha unachanganya aina hizo za uwekezaji ili usiwe kwenye hatari kubwa, lakini pia usiishie kupata faida kidogo pekee.
 5. Njia bora ya kufanya uwekezaji kuwa mchezo wa ushindi ni kuwa na sera ya uwekezaji ambayo mtu unaifuata wakati wote. Na katika kutengeneza sera hiyo hakikisha inakidhi vigezo vifuatavyo;

Moja; je sera yako ya uwekezaji inaendana na hali yako na mahitaji yako kama mwekezaji? Hapa unaangalia mgao wa uwekezaji, usalama na kipato.

Mbili; je sera hiyo umeiandika na kuieleza vizuri kiasi kwamba mtu yeyote anaweza kuielewa na kuifuata? Kama haieleweki kwa wengine, ni vigumu hata wewe kuielewa.

Tatu; je sera yako inaweza kupita nyakati ngumu kiuchumi na ukavuka salama? Hapa fikiria nyakati ambazo ni za msukosuko kwenye uwekezaji na kuona kama sera hiyo ingekuacha salama.

Nne; je kwa kufuata sera hiyo utafikia malengo yako ya muda mrefu?

Sera yoyote ya uwekezaji ambayo inakidhi vigezo hivyo inakufaa na itakuwezesha kufanikiwa kwenye uwekezaji.

Yapo mengi ya kujifunza kwenye uwekezaji kupitia kitabu hichi, haya ni machache ambayo kwa kuyatekeleza, utaweza kufanikiwa kupitia uwekezaji.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz