Kwenye kazi yoyote ya sanaa, iwe ni uandishi wa vitabu, nyimbo, maigizo, uandishi wa habari na hata biashara na ujasiriamali, kuna mambo mawili yanayoweza kutokea kazi inapotolewa. Kazi hiyo inaweza kusikika kwa siku chache na baada ya hapo kupotea kabisa au kazi hiyo inaweza kudumu kwa muda mrefu, miaka na miaka ikaendelea kudumu.

Kila mtu anayejihusisha na kazi yoyote ya ubunifu, kuanzia uandishi, muziki, maigizo, vichekesho, biashara na ujasiriamali, anapenda kazi yake idumu vizazi na vizazi. Lakini ni kazi chache sana ambazo zinaweza kudumu kwa vizazi. Kazi nyingi zinazozalishwa, hasa kwenye zama tunazoishi sasa, zinasikika kwa muda mfupi na kupotea.

Kwenye zama tunazoishi sasa, zama za mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii, ambapo yeyote anaweza kujiita chochote anachotaka na kufanya chochote, kazi nyingi zimekuwa hazidumu hata dakika kumi, achilia mbali mwaka ambao wengi wangefurahi kazi zao zidumu.

Mwandishi Ryan Holiday, amefanya utafiti kwenye zile kazi ambazo zimeweza kudumu miaka na miaka, kutoka vizazi na vizazi, na kugundua kuna namna kazi hizi zinatengenezwa na hata kutangazwa na kusambazwa ambapo kunatofautiana na zile kazi ambazo hazidumu.

Perrenial-Seller-by-Ryan-Holiday

Kwenye kitabu chake cha PERENNIAL SELLER, Ryan anatushirikisha mbinu hizi, ili kama tukizijua na kuzitumia, tutengeneze vitu ambavyo vitadumu vizazi na vizazi.

Kabla hujaanza kusema mimi siyo msanii hivyo mbinu hizo hazinihusu, naomba nikukumbushe kila kitu kwenye maisha kina pande mbili, upande wa kwanza ni sayansi ya kitu hicho na upande wa pili ni sanaa ya kitu hicho. Hivyo kama unafanya biashara, kuna sayansi ya biashara na pia kuna sanaa ya biashara. Na kama unafanya chochote ambacho kinawahusisha watu, ambapo unataka watu wanunue au walipie, PERENNIAL SELLER kitakupa mbinu za kutengeneza kitu kitakachodumu na kuwa sehemu ya maisha ya wengi.

Kwenye kitabu hichi, Ryan anatuambia kazi yoyote inayodumu vizazi na vizazi imegawanyika kwenye maeneo makuu manne. Eneo la kwanza ni hatua za ubunifu, eneo la pili ni hatua ya ukamilishaji, eneo la tatu ni kutafuta masoko na kutangaza na eneo la nne ni kuwa na jukwaa.

Kwenye uchambuzi huu wa kitabu tutaangalia maeneo haya manne muhimu na jinsi ya kuifanya kazi yako kudumu vizazi na vizazi kwa kuzingatia maeneo haya manne.

ENEO LA KWANZA; HATUA YA UBUNIFU.

Hatua ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza kazi inayodumu ni kuanza na ubunifu. Hapa unakuja na kitu ambacho kinahitajika na watu, kinatatua matatizo na changamoto zao na wanakielewa na jinsi kinavyoweza kuwasaidia. Watu wengi wamekuwa wakikazana kutangaza vitu ambavyo ni vya kawaida, na wanashangaa kwa nini hawauzi kama walivyotegemea. Kama kazi ni mbovu, hata uitangaze kiasi gani, haitakuwa nzuri. Hivyo kabla hujakimbilia kutangaza kazi yako na mengine, kwanza hakikisha ni kazi bora na ya kipekee kabisa.

 1. Kazi ndiyo kitu muhimu zaidi.

Mtu yeyote anayetaka kutengeneza kitu kitakachodumu kwa muda mrefu, basi anapaswa kujua kwamba kazi haikwepeki. Hatua ya kwanza kabisa ya mtu huyo kuchukua ni kuweka kazi, kazi kubwa na kazi ya kipekee kabisa. habari njema ni kwamba kuweka kazi kuko ndani yako, hakuna anayeweza kukuzuia, lakini habari mbaya ni kwamba kazi itauwa ngumu. kutengeneza kitu cha tofauti na cha kipekee, unahitaji kufanya vitu ambavyo wengine hawapo tayari kufanya, na vitu hivyo ni vigumu, ndiyo maana wengine hawapendi kufanya.

 1. Huwezi kumwajiri mtu afanye kazi yako.

Kuna mambo mengi kwenye maisha yako ambayo unaweza kuwaajiri wengine wakufanyie, lakini inapokuja kwenye kazi ambayo unataka idumu, kazi ya kipekee kabisa, basi hiyo huwezi kumwajiri mtu mwingine akufanyie. Hata kama kuna mtu ni mzuri kabisa kwenye ufanyaji, wewe pekee ndiye mwenye ndoto na maono makubwa kwenye kazi hiyo, hivyo ni jukumu lako kufanya kazi hiyo. Hata kama utashirikiana na wengine, au wengine watakusaidia, lakini ile kazi hasa lazima iwe chini yako. Kama unataka kutengeneza kazi inayodumu, au kuanzisha biashara inayodumu, hakuna namna utaweza kujitenganisha na kazi ngumu iliyopo mbele yako.

 1. Watu wengi wanapenda kujiita, ila hawapendi kuwa.

Ni rahisi sana kujiita mjasiriamali, mwandishi, msanii na majina mengine kama hayo. Na dunia ya sasa, dunia ya mitandao ya kijamii, tembelea kila ukurasa wa mtu na utakutwa umepambwa na maneno kama mjasiriamali, ‘self-employed’, ‘hardworker’ na kadhalika. Lakini ukienda kwenye uhalisia wa maisha ya watu hao, unagundua hawaishi yale wanayojiita. Mwandishi anafanya kitu kimoja, kuandika, lakini utakuta wanaojiita waandishi hawajakaa chini na kuandika kitu chenye maana, badala yake wanaahirisha kila mara.

Ni rahisi kujiita chochote unachotaka, lakini ni ngumu kuishi kile unachojiita. Katika kutengeneza kazi itakayodumu kwa vizazi, usikazane na kujiita chochote, wewe fanya kile unachopaswa kufanya, weka kazi na matokeo yatasema kama wewe ni mwandishi kweli, kama ni mchapa kazi kweli au kama ni mjasiriamali kweli.

 1. Kwa nini unataka kufanya kazi unayotaka kufanya?

Hatua muhimu kabisa kwenye kutengeneza kazi inayodumu, ni kujiuliza kwa nini unataka kutengeneza kazi hiyo. Kutengeneza tu kwa sababu umeona wengine wanafanya, ni msukumo usio na nguvu. Unahitaji KWA NINI yenye nguvu, ambayo itakusukuma pale utakapokwama, ambayo itakuamsha pale unapolala.

Baadhi ya KWA NINI zinazoweza kukusukuma ni kama ifuatavyo;

Kwa sababu kuna ukweli ambao haujasemwa kwa muda mrefu.

Kwa sababu dunia itakuwa bora kupitia kazi hiyo.

Kwa sababu umeshachoma moto madaraja yote yaliyokuwa nyuma yako na huna namna nyingine.

Kwa sababu familia yako inakutegemea wewe kupitia hicho unachotaka kufanya.

Kwa sababu njia za zamani hazifanyi tena kazi.

Kwa sababu ndiyo fursa ya kipekee sasa na haitarudi tena.

Kwa sababu itawasaidia watu wengi.

Kwa sababu unataka kufanya na kuonesha kitu fulani muhimu.

Kwa sababu hamasa uliyonayo ndani yako haiwezi kutulizwa.

Hizi ni baadhi ya KWA NINI ambazo zinaweza kukusukuma kufanya kazi ngumu ambayo baadaye itadumu vizazi kwa vizazi. Kwa sababu unataka kuonekana, au kwa sababu unataka kupata fedha za haraka siyo KWA NINI nzuri kwako kutumia.

 1. Upo tayari kutoa nini?

Kitu kingine muhimu kwenye kutoa kazi itakayodumu kwa vizazi ni kile ambacho upo tayari kutoa. Hakuna kitu kinachopatikana bure, na kadiri unavyotaka makubwa, ndivyo unavyohitajika kutoa makubwa zaidi. Kadhalika kwenye kuzalisha kazi itakayodumu kwa vizazi, lazima uwe tayari kutoa vitu vikubwa zaidi.

Utahitajika kufanya kazi siku saba za wiki, na kwa muda mrefu kuliko wanavyofanya wengine. Utahitaji kuwa mbali na familia yako, utahitaji kufanya kazi wakati wengine wamepumzika na kustarehe. Utahitaji kukataa fedha za muda mfupi ili kujiandaa kupata fedha za muda mrefu.

Je upo tayari kujitoa kiasi hicho? Kwa sababu bila ya kujitoa, ni vigumu kufanya kazi inayoweza kudumu.

 1. Kama unataka hela za haraka, sahau kazi inayodumu.

Kitu kimoja kuhusu kutengeneza kazi inayodumu, kuanzia sanaa mpaka kwenye biashara, kama unachoangalia ni kupata fedha za haraka, upo kwenye njia mbaya kwako. Huwezi kutengeneza kazi itakayodumu kama kitu pekee unachoangalia ni kupata hela za haraka.

Zipo njia sahihi za wewe kupata fedha za haraka, kuajiriwa, kuuza vitu vya wengine kwa kamisheni, au kufanya biashara za msimu. Lakini kama unataka kuanzisha biashara itakayodumu miaka kumi mpaka mia moja ijayo, kama unataka kuandika kitabu kitakachosomwa kwa miaka mingi, basi swala la kupata fedha za haraka linapaswa kuwa kwenye mwisho wa orodha kabisa.

 1. Angalia vitu visivyobadilika.

Kama unataka kutia kazi itakayodumu, basi kaa mbali sana na vyombo vya habari au mtindo wa kisasa. Kuna vitu ambavyo huwa vinavuma sana, lakini huwa havidumu. Kuweka nguvu zako kutoa kitu kitakachodumu kwenye mambo yanayovuma ni kujidanganya.

Unapotaka kuzalisha kazi itakayodumu, angalia vitu ambavyo havibadiliki, angalia vitu ambavyo siyo vya msimu. Hata unapoanzisha biashara, anzisha biashara ambayo watu wana uhitaji wakati wote, na siyo biashara ya msimu, au watu wana uhitaji kwa sababu ni kitu kinachovuma, ambacho baadaye kitapita.

Usitekwe na uharaka wa kukimbizana na fursa kwa sababu umeambiwa inapita na haitarudi tena. Ili kuwa na uhakika zaidi, mtu akishakuambia fursa hii inapita na haiji tena, basi ndiyo sababu nzuri kwako kwa nini unapaswa kukaa nayo mbali. Hili ni muhimu sana kwenye biashara, tumekuwa tunaona watu wanakimbizana na vitu vinavyovuma, lakini vimekuwa havidumu. Mfano tumekuwa tunaona watu wanakimbizana na vitu kama ufugaji wa kware au sungura kama fursa mpya, lakini zimekuwa zinakuja na kupita. Wakati tangu miaka na miaka, watu wanakula nyama ya ng’ombe na kuku, na kutumia maziwa ya ng’ombe na mayai ya kuku. Hivyo kama unataka kufanya biashara inayohusiana na ufugaji, maeneo hayo mawili ni mazuri na ya uhakika, ambayo yatadumu vizazi na vizazi.

 1. Sheria ya Lindy kwenye kutabiri kudumu kwa kitu.

Ipo sheria moja ambayo imekuwa inatumika kupima kama kitu kitadumu kwa muda gani. Sheria hii inaitwa LINDY EFFECT. Sheria hii inasema kwamba kama kitu kimedumu miaka 10, basi kina uwezekano mkubwa wa kudumu miaka mingine kumi ijayo. Na kama kitu kimedumu kwa mwaka mmoja, basi kuna uwezekano wa kudumu mwaka mwingine mmoja. Kadiri kitu kinavyokuwa kimedumu kwa muda mrefu, ndivyo kina uwezekano wa kudumu muda mrefu zaidi.

Sheria hii inaweza kukusaidia sana kuepuka kuingizwa kwenye fursa zisizodumu, kwa kuangalia kitu hicho kimedumu kwa muda gani. Na kama unataka kufanya kitu kinachodumu, basi hakikisha unapoangalia, kiwe kimedumu zaidi ya miaka kumi.

 1. Njia mbili za kuifanya kazi ya uandishi kufanikiwa.

Kuna njia mbili za kuifanya kazi ya uandishi kuwa na mafanikio makubwa, hasa kwa vitabu ambavyo siyo vya usanii.

Njia ya kwanza ni kukifanya kitabu kuwa cha burudani sana, yaani mtu asukumwe kusoma zaidi kwa sababu kinamburudisha, kinamfanya afurahi sana kupitia yale anayojifunza.

Njia ya pili ni kukifanya kitabu kuwa cha vitendo, yaani mtu akisoma basi atoke na vitu anavyoweza kufanyia kazi moja kwa moja na akapata matokeo bora kabisa.

 1. Jipe muda wa kutosha.

Kitu muhimu kabisa cha kuzingatia kwenye kutoa kazi itakayodumu ni kujipa muda wa kutosha. Usiharakishe, jipe muda wa kuhakikisha kila unachofanya umekifanya kwa usahihi. Jipe muda wa kurudia kila ulichofanya, kusahihisha makosa na kuboresha zaidi yale maeneo ambayo hayajakaa vizuri.

Hakuna kazi bora ambayo imewahi kuzalishwa kwa haraka, hivyo jipe muda na jua kwamba unazalisha kazi bora hivyo haraka haitakiwi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

ENEO LA PILI; HATUA YA UKAMILISHAJI.

Baada ya kuzalisha kazi yako bora, ambayo umeweka kila ambacho umeweza kuweka, umeteseka na kujitoa sana, kazi yako bado inakuwa haijakamilika. Hapa ni sawa na mama anayebeba mimba miezi tisa, anajifungua, lakini mtoto bado ni mchanga na hivyo kuna kazi ya malezi. Hatua ya pili kwenye kutengeneza kazi inayodumu ni kukamilisha ile kazi ambayo umeweka muda na nguvu zako nyingi. Unahitaji kuhariri na kupitia kazi yako, unahitaji kuizalisha kwa namna inavyoweza kuwafikia wengi na unahitaji kujua watu muhimu unaowahitaji ili kazi yako ifike kwa wale wanaoihitaji.

 1. Zama zimebadilika, sasa unahitaji kufanya kila kitu mwenyewe.

Siku za nyuma, msanii au mtu mwenye wazo na anayefanya kitu, aliishia kuwa mtu wa kufanya tu, kazi nyingine zilikuwa za watu wengine. Hivyo msanii angeandika kitabu kisha wachapishaji ndiyo wangekihariri, kukichapa na kisha kukisambaza. Mtu mwenye wazo la biashara angeeleza wazo lake kisha wengine wangempa mtaji na mengine anayohitaji ili kuanza.

Zama hizo zilishapita, sasa unahitajika kufanya kila kitu mwenyewe. Kuandika tu kitabu hakutoshi kukufanya wewe kuwa msanii. Kuwa na wazo bora la biashara hakukufanyi kuwa mfanyabiashara. Unahitaji kufanya kila kinachofuata mpaka kazi yako ifike kwa wale unaowalenga. Na kazi zitakuwa nyingi, nyingine ambazo zipo nje ya uwezo wako, lakini lazima uzifanye, kwa sababu unataka kazi yako iwafikie wengi.

 1. Wewe ndiye mkurugenzi mtendaji.

Hatua ya kwanza ya kuzalisha kazi inayodumu ni kujua kwamba hakuna anayekuja kukuokoa, hakuna atakayekuja kuondoa kazi kubwa iliyopo kwenye mikono yako, wewe ndiye mkurugenzi mtendaji wa kile unachofanya na hakuna mwingine wa kumwangalia pale mambo yanapokwenda tofauti.

Unahitaji kuwa mtu mzima, kwa maana kwamba unahitaji kufanya maamuzi, ambayo yanaweza kushindwa na ukabeba mzigo wa maamuzi yako. Huwezi kuzalisha kazi inayodumu kama utakuwa na akili na tabia za kitoto, tabia za kuwaachia wengine wafanye maamuzi, halafu mambo yakienda tofauti unawalaumu, na kusema lakini wao ndiyo walisema tufanye hivi. Unahitaji kufanya mwenyewe, na kuwa tayari kubeba jukumu la matokeo utakayopata.

 1. Sentensi moja, aya moja, ukurasa mmoja.

Ili kuweza kuelewa vizuri kile unachofanya, na kuweza kuwaelewesha wengine nao waelewe, hasa wale unaoshirikiana nao au watakaokuwa wateja na watumiaji wa unachofanya, unahitaji kuweza kueleza hicho unachofanya kwa sentensi moja, kwa aya moja na kwa ukurasa mmoja.

Mfumo wa kueleza hicho unachofanya unahitaji kueleza vitu vitabu;

Moja; hichi ni…… hapa unaeleza nini unafanya.

Mbili; ambacho kinafanya …. hapa unaeleza kile unachofanya kina matumizi gani.

Tatu; Hichi kinawasaidia watu ….. hapa unaeleza jinsi kitu hicho kinawasaidia watu kwenye maisha yao.

Hakikisha kwa chochote unachofanya, unaweza kukielezea kwenye maeneo hayo matatu, ndani ya sentensi moja na mtu akaelewa, ndani ya aya moja na mtu akashawishika na ndani ya ukurasa mmoja na mtu akasukumwa kuchukua hatua. Kama huwezi kueleza kile unachofanya kwa namna hiyo, bado hujajiandaa vya kutosha.

 1. Vitu vitatu vya kuzingatia ili kuwateka watu kwenye kile unachofanya.

Watu hawanunui kwa sababu unauza, watu wananunua kwa sababu wameshawishika kununua. Na kwenye kazi yoyote ya sanaa, na hata biashara yoyote, unahitaji vitu vitatu ili kuwashawishi watu kununua.

Cha kwanza; mpangilio wa kitu, hapa ni uelewa wa watu kuhusu kitu hicho na kinafanya kazi gani.

Cha pili; jinsi kilivyoandaliwa, hapa watu wanavutiwa na kitu kilivyo kwa nje na hata jina lake.

Cha tatu; maelezo ya mauzo, hapa ni jinsi kitu kinavyoelezwa kwa wateja wake na wakaona kinawahusu.

Chochote unachofanya, hakikisha kinaowahusu wanakielewa, pia kina mwonekano mzuri na jina linalovutia, na maelezo ya kuwashawishi watu kununua, yanawasukuma watu kuchukua hatua.

 1. Weka nguvu zako kwenye kitu kimoja kwanza.

Watu wengi wanaotamani kufanya kazi zinazodumu wamekuwa wanashindwa kwa sababu wanakuwa kwenye usumbufu mkubwa sana. Wanataka kufanya kazi inayodumu, lakini kila kitu kinachopita mbele yao wanakimbia nacho. Kila wanapoona wengine wanafanya vitu vipya na wao wanataka kuvijaribu. Unapotaka kufanya kazi inayodumu, weka nguvu zako kwenye kazi hiyo kwanza mpaka ikamilike, kisha ndiyo unaweza kuhamia kwenye vitu vingine.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; A Gift To My Children (Zawadi Ya Baba Kwa Watoto Wake, Masomo Ya Maisha Na Uwekezaji).

ENEO LA TATU; MASOKO NA UTANGAZAJI.

Tayari umeandaa kazi yako na kuikamilisha, umeshajua inawahusu watu gani na kwa namna gani unaweza kuwashawishi kuipata. Sasa hapa ndipo wengi wanapopotea, huwa wanafikiri kwa sababu kazi ni bora basi itajiuza yenyewe. Na tena upo usemi wa kiswahili kwamba KIZURI CHAJIUZA NA KIBAYA CHAJITEMBEZA, ukimaanisha kwamba kama kitu ni kizuri basi hakina haja ya kutangazwa. Naomba nikuambie kwamba inapokuja kwenye kufanya kazi ambayo itadumu, basi KIZURI KINAJITEMBEZA, na kinajitembeza hasa. Utahitaji kuitangaza kazi yako mno mno mno. Siyo kwa sababu kazi yako ni mbaya, bali kwa sababu watu unaowalenga sasa hivi wanasumbuliwa na vitu vingine. Wapo kwenye mitandao ya kijamii na wanasumbuliwa na picha za uchi wanazoweka wengine. Hivyo kama hutaweka nguvu ya kuwafikia, hutaweza kuwapata.

Lakini kumbuka hili muhimu, usikimbilie kutangaza kama kazi yako ni mbovu. Kwanza kazi yako iwe bora sana, kazi ambayo unajivunia nayo, halafu hakikisha kila inayemhusu basi anajua uwepo wa kazi hiyo.

 1. Wewe ndiye muuzaji wa kwanza wa kazi yako.

Hata kama kuna watu ambao wanakusaidia kuuza kile ulichotengeneza, kumbuka hili wakati wote, wewe ndiye muuzaji wa kwanza. Na wewe ndiye utakayefanya kazi kubwa kwenye uuzaji kuliko mtu mwingine yeyote. Unahitaji kuwekeza nguvu nyingi kwenye utangazaji na uuzaji wa kazi yako kuliko mtu mwingine yeyote.

Kama unaamini kweli kwenye kazi uliyoifanya kwa nguvu kubwa, basi ifanyie haki kwa kuweka nguvu kubwa kuitangaza na kuisambaza, kuhakikisha kila inayemhusu anaijua.

 1. Watu wapo ‘BIZE’.

Hata kama umekuja na uvumbuzi wa kipekee kabisa ambao unaweza kuwasaidia watu wa aina fulani, kumbuka hili, watu wapo bize, na wapo bize kweli kweli. Siyo kwamba walikuwa wamekaa hawana cha kufanya na wanasubiri wewe uje na cha kuwaambia. Watu wametingwa, hivyo unahitaji kuwa na mbinu za kuwafikia kule walipo, pamoja na kutingwa kwao.

Hivyo unahitaji kuwa na mbinu bora za masoko, mbinu ambazo zitakuwezesha kuwafikia wale wanaohusika na unachofanya, na siyo kukazana kufikia kila mtu. Kuna wakati utahitajika kusambaza kazi yako mwenyewe mtu kwa mtu, nyumba kwa nyumba, ili kuhakikisha unawafikia kweli wale inaowahusu.

 1. Njia bora ya kutangaza na isiyo na gharama.

Watu wamekuwa wanaingia gharama kubwa kutangaza kazi zao, na mauzo yamekuwa siyo makubwa kama wanavyotegemea. Lakini ipo njia moja ya kutangaza ambayo haina gharama na ni muhimu sana. Njia hiyo ni NENO LA MDOMO. Pale watu wanapoanza kuongelea kile unachouza, pale watu wanapowaambia wengine wanunue kile unachouza, hiyo ndiyo njia bora kabisa ya kutangaza biashara yako. Fikiria vitu vingi ulivyowahi kununua kwenye maisha yako, je ulinunua kwa sababu uliona tangazo au kwa sababu mtu alikuambia ni vizuri?

Hivyo unahitaji kuiweka kazi yako kwa njia ambayo mtu anayeijaribu au kuitumia, basi anasukumwa kuwaambia wengine nao wajaribu au kutumia. Kama ni mgahawa, toa huduma ambayo mtu akiipata basi anawaambia wengine nao waje. Kama ni kitabu kinapaswa kuwa kwa namna ambayo mtu akikisoma anawaambia wengine nao wakisome.

 1. Mtandao wako ndiyo sehemu ya kwanza kuuza.

Wale wote ambao unawafahamu na wanakufahamu, ndiyo wanapaswa kuwa wateja wako wa kwanza kwenye kazi yako uliyozalisha. Unahitaji kukaa chini na kuorodhesha wale wote ambao unawajua na wanakujua, na wenye ushawishi kwa wengine, na kuwatumia watu hao kuwafikia watu wengi zaidi. Lakini unapotumia mtandao wako huo wa watu, kuwa makini kuhakikisha unachofanya kinawanufaisha wao na wewe pia.

Mitandao ya kijamii pia ni njia nzuri unayoweza kutumia kuwaambia watu kuhusu kile unachofanya, na kupata wanunuaji na hata wasambazaji zaidi wa kile unachofanya.

 1. Jinsi ya kutumia vyombo vya habari bure na kwa gharama.

Watu wengi hufikiri wakipata nafasi ya kutangaza kwenye TV, redio au magazeti basi watauza sana. Ni kweli vyombo hivyo vinawafikia watu wengi, lakini hilo halimaanishi utawauzia wote unaowafikia.

Manufaa makubwa utakayoyapata kupitia vyombo vya habari ni watu kujua uwepo wako na kile unachofanya, lakini baada ya hapo unahitaji kuwashawishi zaidi mpaka wawe wateja kweli.

Unaweza kutumia vyombo vya habari kutangaza kazi yako bure kama utajiweka kama mtu unayeshauri na kuelimisha kupitia kile unachofanya. vyombo vya habari vitapenda kukuita kwa mahojiano au kuchapa makala na maoni yako. Unapopata nafasi kama hizo, unapaswa kueleza kile ulichotengeneza.

Pia unaweza kulipia matangazo kwenye vyombo vya habari na watu wakajua kuhusu uwepo wako.

Unapofikiria kutumia vyombo vya habari kuwafikia wengi zaidi, hakikisha unatumia gharama ndogo uwezavyo, na hupotezi muda wako mwingi.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; Winning The Loser’s Game (Mbinu Zisizopitwa Na Wakati Za Kufanikiwa Kwenye Uwekezaji).

ENEO LA NNE; KUWA NA JUKWAA.

Umeweka juhudi kubwa kuja na kazi yako ya ubunifu, umekazana kuikamilisha na umeweka nguvu kubwa kuitangaza na kwa siku chache baada ya kuitoa umeona mauzo ni makubwa. Hapo unayaona mafanikio, unaona kwamba kuna dalili za kuwa kazi itakayouza vizazi na vizazi. Lakini hapo ndipo wengi wanapokosea, kumbuka kuuza vizazi na vizazi hatuangalii leo au mwaka huu, tunaangalia miaka 10, 50 na 100 ijayo. Unajua kabisa kwamba huwezi kuendelea kutangaza kazi yako kwa nguvu unazotumia sasa kwa miaka kumi, unahitaji kufanya kazi nyingine pia.

Unahitaji kuwa na njia itakayokuwezesha kuwakumbusha watu kwamba kazi zako zipo na zinaweza kuwasaidia, hasa wale wanaokuja kukujua baadaye, ukiwa tayari umetoa kazi zako unazotaka zidumu. Hapa ndipo unapohitaji KUWA NA JUKWAA, kuwa na njia ya kuwafikia wapenzi na mashabiki wa kazi yako bila ya kuzuiwa na mtu mwingine yeyote.

 1. Kila mtu anahitaji kuwa na jukwaa lake, analomiliki yeye.

Lipo kosa moja ambalo wasanii na hata watu wengine wamekuwa wanafanya kwenye kazi zao. Wanategemea baraka za watu wengine ili maisha yao yaende. Mfano msanii anakuwa anategemea vyombo vya habari kupiga nyimbo zake ndiyo awafikie watu. Inapotokea vyombo hivyo vinakataa kupiga nyimbo zake, anakuwa ameondolewa kabisa kwenye sanaa.

Siku za hivi karibuni pia wafanyabiashara wamekuwa wanafanya kosa kubwa sana. Wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kama majukwaa yao, ambayo wanayatumia kuwafikia wateja wao. Kiasi kwamba kama mitandao ya kijamii inafungwa yote leo, wafanyabiashara wengi wataondoka kwenye biashara kabisa, kwa sababu hawana njia nyingine ya kuwafikia wateja wao.

Usifanye kosa hili kwenye kazi yako unayotaka idumu kwa muda mrefu, unahitaji kuwa na jukwaa unalomiliki wewe mwenyewe. Unahitaji kuwajua mashabiki wa kweli wa kazi zako, ambao unaweza kuwafikia hata kama dunia nzima itakuwa imekususia na kila unayemtegemea amekutenga.

 1. Unahitaji mashabiki wa kweli 1,000 ili kuendesha maisha yako.

Mwandishi Kevin Kelly anasema kwa chochote unachofanya kwenye maisha yako, unahitaji kuwa na mashabiki wa kweli elfu moja ili kuweza kuendesha maisha yako. Tunaposema mashabiki wa kweli, ni wale ambao wanakuamini kweli, wale ambao wapo tayari kufanya chochote kupata kazi zako. Wale ambao wapo tayari kuwaambia wengine kuhusu wewe, wapo tayari kulipa gharama yoyote kupata kazi zako.

Unahitaji mashabiki hao elfu moja ili uweze kuendesha maisha yako kwa upande wa kipato. Kwa mfano kama una mashabiki hao elfu moja, na kila mmoja anakuingizia faida ya elfu moja kwa mwezi, una zaidi ya milioni moja kwa mwezi, kitu ambacho kitayawezesha maisha yako kwenda.

Lakini pia mashabiki hao elfu moja ndiyo wataitangaza kazi yako kwa wengine.

 1. Jukwaa muhimu unalohitaji zama hizi.

Kwenye zama tunazoishi sasa, lipo jukwaa moja muhimu sana unalohitaji ili kazi yako iweze kuwafikia wengi na pia kutengeneza mashabiki wa kweli wa kazi yako.

Jukwaa unalohitaji ni mawasiliano ya wateja na wafuasi wako. Unahitaji kujua wanapatikana wapi, namba zao za simu, na muhimu zaidi email wanazotumia. Kwa dunia ya sasa, email ndiyo mawasiliano rahisi kabisa na yasiyo na usumbufu. Lakini pia mawasiliano ya email yamedumu kwa muda mrefu kuliko hata mitandao ya kijamii, hivyo kwa sheria ya LINDY, email zitaendelea kuwa mawasiliano muhimu zaidi.

Kwa chochote unachofanya, hakikisha una taarifa za wale wateja wako wa kweli, wale ambao wanaamini kwenye kile unachofanya. Kusanya mawasiliano yao kwa njia ya mtandao na hata njia ya kawaida, kisha tumia mawasiliano hayo kujenga nao mahusiano bora.

 1. Tengeneza mahusiano mazuri na mashabiki wako wa kweli.

Ukishakuwa na orodha ya mawasiliano ya mashabiki wako wa kweli, unahitaji kutengeneza nao mahusiano mazuri. Unahitaji kuwasiliana nao mara kwa mara, kwa kuwatumia jumbe nzuri kwa simu kama unafanya biashara ya kawaida. Na kama unafanya kazi ya sanaa, kama uandishi, basi tumia email za wasomaji na wateja wako kuwatumia mafunzo mazuri pia. Kadiri unavyowatumia vitu vizuri, ndivyo wanavyokukumbuka na kuwa rahisi kununua chochote unachotoa.

 1. Ukubwa wa mtandao wako ndiyo ukubwa wa utajiri wako.

Upo usemi wa kiswahili kwamba haijalishi unajua nini, bali unamjua nani na nani anakujua. Kitu kikubwa unachotakiwa kufanya kwenye kazi yako, ni kutengeneza mtandao wako. Na hapa sizungumzii mtandao wa kijamii, kwamba una marafiki wangapi au ‘followers’ wangapi, bali namaanisha mtandao halisi, wa wale watu wanaokujua wewe na kazi unayofanya, ambao mmewahi kukutana ana kwa ana.

Kadiri mtandao huu unavyokuwa mkubwa, na kadiri mtandao huo unavyokuwa na watu wenye ushawishi, ndivyo unavyoweza kukusaidia kufanikiwa zaidi.

Weka kazi kwenye kutengeneza mtandao wa aina hii. Na njia bora ya kukuza mtandao wako ni kuangalia unawezaje kuwasaidia wale ambao wana ushawishi mkubwa kwenye kile unachofanya au eneo ulilopo. Kadiri unavyowasaidia wengi, ndivyo wanavyokuwa na deni kwako, na baadaye wanaweza kukusaidia na wewe pia.

Wasaidie pia wale ambao hawana ushawishi sasa, lakini unaona wana kitu ndani yao, ambacho kitawafanya wafike mbali. Watakapofika juu zaidi, hawatakusahau kamwe na wataweza kukusaidia zaidi.

Hizo ndizo hatua nne za kutengeneza kazi itakayouza vizazi na vizazi.

Mwisho kabisa Ryan anatuambia pamoja na juhudi hizi tunazoweza kuweka, kuna kitu kimoja ambacho hatuwezi kukiathiri, kitu hicho ni BAHATI. Wakati mwingine kuna vitu vinatokea, ambavyo vinakusaidia kusonga mbele zaidi, ambavyo hukuvifanya wewe vitokee. Kwa mfano mtu mwenye ushawishi mkubwa anakutana na kazi yako, na kuipenda kisha kuwaambia wale ambao ana ushawishi kwao na ghafla unakuwa mtu maarufu. Lakini tunapaswa kugundua jambo moja muhimu kuhusu bahati, hutapata bahati kwa kuomba ukutane na bahati, badala yake unahitaji kuwa na maandalizi ya kutosha, ili nafasi inapotokea basi uwe kwenye eneo sahihi.

Hivyo japo huwezi kulazimisha bahati, kadiri unavyokuwa umefanya kazi bora, na kuitangaza vizuri kwa wale wanaohusika, kisha ukawa na jukwaa la mashabiki wa kweli, unaongeza nafasi za wewe kukutana na fursa ambayo utaweza kuitumia na wengine wataona ni bahati.

Kwa chochote unachofanya, usikubali kufanya kitu kitakachodumu kwa muda mchache, kwa msimu tu kisha kikapotea. Tengeneza kitu ambacho kitaishi kwa muda mrefu kuliko muda utakaoishi wewe, na hivyo ndivyo dhana ya wewe kuishi milele.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji