Tunapopanga kuongeza ufanisi na uzalishaji, huwa tunaangalia muda. Tunaangalia ni muda kiasi gani tunao, kisha tunaupangilia na kuusimamia vizuri. Lakini licha ya kupangilia na kusimamia muda vizuri, kuna wakati tunashindwa kufanya yale tuliyopanga, licha ya kuwa na muda wa kutosha.

Kwa mfano kama lipo jukumu gumu kufanya, ambalo linahitaji utulivu wa akili yako kulikamilisha na juhudi pia, ukilifanya ukiwa tayari umeshachoka, utakuwa na kila sababu ya kuahirisha au kushindwa kufanya vizuri.

Muda Unaotumia

Hivyo hii inatuonesha kwamba, kilicho muhimu kwenye ufanisi na uzalishaji siyo muda, bali nguvu. Kwani kama ukiwa na muda wowote utakao, lakini ukawa huna nguvu, hutaweza kutumia muda huo kama ulivyopanga.

Hivyo kitu cha kupangilia, kusimamia na kutumia vizuri ni nguvu, na siyo muda. Nguvu ndiyo inayozalisha kile tunachotaka, hivyo ni kitu muhimu sana kufanyia kazi.

Katika kupangilia na kusimamia nguvu zako, kwanza jua ni wakati upo unakuwa vizuri kufanya shughuli zako, hasa zile ambazo ni ngumu na zinahitaji umakini wako. Kwa wengi muda huo ni asubuhi na mapema, na kwa wengine muda huo ni mchana au jioni. Hivyo hatua ya kwanza ni kujua muda unaokufaa wewe, muda ambapo unakuwa na nguvu za kutekeleza yale uliyopanga kufanya.

SOMA; UKURASA WA 1043; Kufanya Kazi Kwa Nguvu, Akili, Kujitoa Na Kuamini Unachofanya.

Ukishajua muda mzuri kwako, basi utenge muda huo kwa majukumu yale ambayo ni muhimu sana, magumu na yenye kuhitaji umakini kuyafanya. Usikubali kabisa kutumia muda huo kwa mambo yasiyo ya msingi.

Kwa mfano ukishajua wewe ni mtu wa asubuhi, yaani asubuhi ndiyo unakuwa na nguvu za kuweza kufanya yale makubwa na magumu, linda asubuhi yako, usikubali kufanya mambo yasiyo ya msingi. Kwa mfano usitumie asubuhi hiyo kufuatilia habari, kutembelea mitandao au kufanya mambo yasiyo na tija.

Kwa sababu kila kitu unachofanya, hata kama ni kidogo kiasi gani, kinapunguza nguvu zako, ndiyo maana ni muhimu kutunza nguvu hizo kwa yale ambayo ni muhimu kwa wakati huo. Yale mengine  ambayo siyo muhimu sana, utaweza kuyafanya wakati wowote, lakini siyo kwa ule wakati ambapo nguvu zako ziko juu na unaweza kufanya makubwa.

Jua muda ambapo nguvu zako zipo juu na unaweza kutekeleza magumu na makubwa na ulinde muda huo kwa mambo hayo. Ukiweza kupata masaa mawili kila siku, ya kuweka kwenye kazi yako kufanya yale magumu na muhimu zaidi, basi utaweza kupiga hatua kubwa sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog