Huenda unaifanya kwa kawaida sana, kwa namna ambayo kila mtu anafanya, na hivyo hakuna yeyote anayeshangazwa na jinsi unavyoifanya kazi yako. Sasa unaweza kufikiria hilo ni jambo bora, lakini sasa, ni hasara na hatari kubwa, kwa sababu ni kiashiria kwamba hufanyi makubwa na pia hutafika mbali.
Kama kazi yako haijawahi kukosolewa na yeyote, ina maana siyo kazi yenye hadhi ya kuwafanya watu waiangalie kwa jicho la tofauti, siyo kazi ya kipekee na ya tofauti ambayo watu wamezoea. Na hivyo basi, siyo kazi ambayo itaweza kukufikisha kwenye mafanikio makubwa.

Kazi yoyote iliyofanywa kwa mipango mikubwa, kazi iliyofanya kwa ubunifu wa hali ya juu, kazi ambayo haijazoeleka kwa wengi, itakaribisha ukosoaji wa kila aina. Itamfanya kila mtu awe na maoni yake ya kutoa kuhusiana na unachofanya, na wengi kwa sababu hawajazoea, hawatakuwa na maoni mazuri.
Ukiona unachofanya kinakubalika na kila mtu, basi kuna dalili kwamba unachofanya ni cha kawaida sana, hakina tofauti yoyote ile na wanachofanya wengine.
SOMA; UKURASA WA 985; Njia Pekee Ya Kwenda Salama Hapa Duniani…
Na kama kusudi lako kwenye maisha ni kukubalika na kila mtu, na hivyo kujaribu kufanya kile ambacho kila mtu atakikubali, basi jua umechagua njia ambayo siyo ya mafanikio. Huwezi kukubalika na kila mtu na bado ukaweza kufanya makubwa kwenye haya maisha.
Hii ni kwa sababu wengi hawapo tayari kufanya makubwa, kwa sababu yanahitaji muda, kujitoa na hata nguvu. Hivyo hawawezi kuvumilia wanapoona wengine wameweza kufanya kile ambacho wao hawawezi kufanya, na watatumia kila njia kuhakikisha wengine nao wanashindwa.
Chochote unachofanya, usikubali kukifanya kwa ukawaida, kifanye kwa utofauti wa hali ya juu sana, kifanye kwa ubunifu wa kipekee na mara zote, angalia jinsi unavyoweza kwenda hatua ya ziada kila mara. Watu watakukosoa na kukupinga, lakini huwa siyo watu muhimu sana, na wakiwa muhimu, ukosoaji wao utakuwa kitu cha kukusaidia zaidi.
Usiogope kupingwa au kukosolewa, ni sehemu ya safari ya mafanikio, tena pale unapokuwa umepanga kufanya makubwa.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog