Linapokuja swala la fedha, watu wamekuwa wanajaribu njia nyingi za kupata fedha lakini wamekuwa wanaishia kufa masikini. Hii ni kwa sababu fedha zina msingi yake na wale ambao hawaijui hiyo misingi hawawezi kuzipata, hata wakikazana kiasi gani.

Siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la michezo ya kamari na bahati nasibu ambayo imekuwa inaibuka kila siku. Zilianza kamari za kubashiri matokeo ya michezo mbalimbali, ambapo wengi walifikiri ni ukombozi kwao kifedha.

Baadaye imekuja michezo ya bahati nasibu, ambayo ni kamari ile ile ila tu inakuja kwa njia ambayo inaonekana ni nzuri kwa nje. Michezo hii ambayo inawaaminisha watu wanaweza kupata mamilioni kwa kutumia kiasi kidogo, mfano kutumia shilingi mia tano kupata mamilioni ya fedha, imejizoea umaarufu kwa wale wasioijua misingi ya kifedha.

Kwa kuwa michezo hii inatengeneza faida kubwa, kwa kutumia hali ya watu kutokuelewa, ina nguvu kubwa ya kufanya matangazo mengi na yanayoshawishi wengi. Hivyo hata yule ambaye alikuwa hafikirii kucheza michezo hii, anajikuta anashawishika kwa nguvu ya matangazo na shuhuda zinazotolewa kwenye matangazo mbalimbali.

Kitu kingine ambacho kimekuwa hatari zaidi kwenye michezo hii ya kamari na bahati nasibu, ni namna ambavyo wameweza kuwalaghai viongozi mbalimbali wa serikali, ambao nao wanawashawishi wananchi wacheze michezo hii kujipatia kipato. Yaani kiongozi ambaye amepewa dhamana ya kuwaongoza watu, kuwapeleka kwenye maisha ambayo ni bora, anawaambia njia ni kucheza kamari, na wale wananchi wasioelewa misingi ya fedha, wanasikiliza, kwa kuwa wanaona kama haya viongozi wanasema, basi ni kitu sahihi.

Cha mwisho kwa hapa, kuhusu michezo hii ni utetezi ambao umekuwa unatolewa na wanaoendesha na hata kutangaza michezo hii. Wanakuambia kwamba michezo hii inalipa kodi na hivyo inachangia maendeleo ya nchi. Hii ni sababu ya hovyo kuliko hata zote, kwa sababu kodi inayolipwa na michezo hii siyo kutokana na thamani yoyote iliyotengenezwa, ila ni makusanyo ya fedha za wananchi, wanaoamini wanaweza kuondoka kwenye umasikini kupitia kamari.

michezo ya kubahatisha

Sasa kama unavyonijua rafiki yako, sina shida na wanaoendesha michezo hii, ndiyo biashara yao, pia sina shida na serikali ambayo inawaambia watu wacheze michezo hii, yenyewe inapata kodi. Ila nina shida na wewe, nina shida na wewe kama umewahi kucheza michezo hii au umewahi kufikiri kwenye akili yako kwamba matatizo yako ya fedha yanaweza kuondoka kwa kucheza kamari au bahati nasibu.

Nina shida na wewe kiasi kwamba leo nimekuandalia maneno makali sana, ambayo yanaweza kukuumiza sana, lakini sina namna bali nitakuambia maneno hayo na kama yakikuuma basi badilika, kama yasipokuuma basi endelea na michezo hii, kama umekuwa unashiriki michezo hii.

Maneno makali niliyopanga kukupa ndiyo haya, kama umewahi kucheza kamari au bahati nasibu, kama umewahi kufikiria kucheza michezo hii, basi ninachokuambia ni kwamba AKILI YAKO HAIKO SAWA. Ndiyo nakuambia akili yako haiko sawa, na nitakupa sababu tano kwa nini nakuambia akili yako haiko sawa kama unacheza kamari.

  1. Ni michezo ambayo imeandaliwa maalumu wewe kushindwa.

Kwenye michezo hii ya kubahatisha na kamari, imepangwa kiasi kwamba lazima utashindwa. Ndiyo yaani unashiriki kwenye mchezo ambao tayari umeshapangiwa kushindwa. Yaani ni sawa na kuingia kwenye mchezo wa mpira wa miguu, wewe uko mwenyewe na wenzako wako 11, utashindwa.

Michezo ya kubahatisha imetengenezwa kwamba, wengi washiriki, lakini wachache sana, kama siyo mmoja ndiyo ashinde, ili kuwapa wengine moyo wa kuendelea kucheza.

Hebu fikiria kwenye mchezo ambao washiriki ni elfu 10, halafu watu watatu tu ndiyo wanaoweza kushinda. Hii ina maana kwamba watu 9,997 wameandaliwa kushindwa moja kwa moja. Ni mchezo wa ajabu sana huu.

  1. Hakuna juhudi unazoweza kuweka kuongeza nafasi yako ya kushinda.

Kwenye shughuli mbalimbali za kujiingizia kipato, kadiri unavyoongeza juhudi, ndivyo unavyoongeza kipato chako. Kwa mfano kama unafanya biashara, ukiongeza ubora wa kile unachofanya, ukikazana kuwafikia wengi, moja kwa moja unaongeza kipato chako. Kama umeajiriwa, ukiongeza juhudi kwenye kazi zako, unaongeza thamani yako na hilo linaweza kupelekea kuongezewa kipato, au hata kudai kipato zaidi.

Lakini kwenye michezo ya kubahatisha, ukishacheza, ukishachagua namba, ukishaweka timu zipi zimeshinda, ndiyo imetoka, huna namna unaweza kubadili, wewe unasubiri tu bahati ikuangukie.

Sasa ninachojua kuhusu mafanikio ni kwamba, kama unasubiria bahati, tayari umeshashindwa, unahitaji kutengeneza bahati, kupitia maandalizi bora na kuweka juhudi kubwa kwenye kile unachofanya.

  1. Ni njia ambayo haitabiriki na haina mifano ya waliofanikiwa.

Duniani kuna mifano mingi ya watu waliofanikiwa kwenye kila eneo la maisha, watu hawa huwa tunawatumia kama hamasa ya sisi kufanikiwa pia. Kwa kuona watu ambao wametoka kwenye mazingira magumu na kuweza kufanya makubwa, tunakuwa na imani kwamba hata sisi tunaweza. Na kwa kujifunza kupitia yale waliyofanya, na sisi tunaweza kufanya pia.

Lakini kwenye michezo ya kubahatisha, hakuna mifano ya waliofanikiwa, na kama ipo basi ni michache sana. Na kibaya sana ni kwamba, huna cha kujifunza kutoka kwa aliyeshinda mchezo wa kubahatisha, yeye imemtokea kama bahati, hivyo hana cha kukuambia kwamba ukifanya hivi na hivi basi matokeo yake yatakuwa hivi.

  1. Ni uvivu uliopindukia.

Fedha zingekuwa rahisi kama hivyo, kwamba ubashiri matokeo halafu ukae na kusubiri, au uchague namba tatu halafu ukae na kusubiri mamilioni ya fedha, kusingekuwa na magari, kusingekuwa na mainjinia, kusingekuwa na madaktari wala wataalamu wowote. Kwa sababu kwa nini mtu ajitese kusoma miaka mingi, kufanya kazi usiku na mchana ili apate fedha wakati anaweza kubashiri matokeo au namba na akapata fedha?

Kama umewahi kushiriki michezo hii, au umekuwa unafikiria, basi jua una uvivu wa kupindukia. Kila mtu ana uvivu, ila wako umepindukia na ni dalili kwamba, hutakuja kufanikiwa kwenye maisha yako, kama hutabadili huo mtazamo ulionao kuhusu fedha na mafanikio.

  1. Unajichelewesha kupata fedha.

Tatizo la michezo ya kubahatisha na kamari ni hili, huwezi kucheza mara moja na kushinda au kusema nimeshindwa basi sichezi tena. Na hata hao wanaochezesha wanajua watu wakifanya hivyo basi wao hawana biashara, hivyo jukumu lao la kwanza ni kuhakikisha unacheza kila mara, tena hata siku moja ucheze mara nyingi. Ndiyo maana utawasikia wakiwahoji wanaoshinda wanasema nilikuwa nacheza mara nyingi. Huo ni mpango wa kukufanya na wewe ufikirie kucheza mara nyingi.

Sasa fedha unazoweka kwenye kucheza michezo hii, na nguvu na muda unaoweka kufuatilia michezo hii, inakuchelewesha kufanikiwa. Kama fedha hiyo kidogo, na muda na nguvu hizo ungezielekeza sehemu nyingine, ungeweza kutengeneza mafanikio imara zaidi kuliko hilo unalopoteza kwenye kamari na michezo ya kubahatisha.

Je ufanye nini ili kufanikiwa kifedha na kuondoka kwenye umasikini?

Nimeshakuambia kama unacheza kamari na michezo ya kubahatisha, AKILI YAKO HAIKO SAWA. Sasa je ufanye nini ili kupata fedha na kuondoka kwenye umasikini? Maana hili ndiyo jambo la msingi kabisa.

Na jibu ni moja, ujue msingi mkuu wa fedha, uishi kila siku na kila mahali, na ninakuhakikishia, utafanikiwa kifedha.

Msingi mkuu wa fedha unaopaswa kuujua ni huu; FEDHA NI ZAO LA THAMANI. Kama unataka kupata fedha, basi kuna kitu kimoja tu unapaswa kufanya, toa thamani. Toa thamani kwa wengine, na wao watakuwa tayari kukupa wewe fedha walizonazo.

Iko hivi rafiki, watu wana shida, watu wana matatizo, watu wana mahitaji, angalia wewe kwa ujuzi ulionao, elimu uliyonayo, uzoefu ulionao, muda ulionao na nguvu ulizonazo  ni thamani gani unaweza kuongeza kwa wengine. Angalia ni matatizo yapi ya watu unaweza kuwatatulia, angalia ni mahitaji yapi unaweza kuwatimizia, kisha fanya hivyo kwa juhudi zako zote.

Kwa njia hii, utajiweka kwenye nafasi nzuri ya kutengeneza kipato, kila mtu mwenye shida na uhitaji atakuja kwako ili umtatulie na atakuwa tayari kukulipa.

Haihitaji uwe na elimu kubwa, ujulikane au hata uwe umeajiriwa, unachohitaji ni wewe kuangalia kipi unaweza kufanya na anza kukifanya. Kama huna kazi kabisa anza na chochote unachoweza kusaidia wengine, anza na kutoa nguvu zako, halafu kila kiasi cha fedha unachopata usitumie, badala yake weka akiba kwa ajili ya kupiga hatua zaidi. Hivi ndivyo unavyokua, ndivyo unavyotoka kwenye umasikini mpaka utajiri.

Mwisho kabisa rafiki nikuambie kitu kimoja, linapokuja swala la fedha, njia ya mkato ndiyo njia ndefu na njia ngumu. Ukishashawishika tu kwamba unaweza kupata fedha kwa njia ya mkato, njia ya haraka ambayo haihusishi fedha, jua umeshapotea na utasumbuka sana. Pita njia ndefu, jipe muda, weka juhudi na utalipwa kadiri ya thamani unayozalisha.

Na kwa wale wanaosema kwamba lakini watu wanashinda kamari na michezo ya kubahatisha, na kutumia hiyo kama sababu ya kucheza, basi naweza kusema hawa ndiyo akili zao zina matatizo makubwa zaidi. Usiwe mmoja wa hao, okoa muda wako, tengeneza thamani na achana na njia za mkato.

Huduma inayoweza kukusaidia kwenye fedha.

Zipo huduma ninazotoa ambazo zinaweza kukusaidia kwenye eneo la fedha.

Moja ni kitabu cha KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, hichi kitakupa sababu 25 kwa nini unaendelea kuwa masikini na njia ya kuondokana nazo.

Mbili ni kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA, hichi ni kitabu kitakachokuwezesha kuanzisha na kukuza biashara yako ukiwa bado umeajiriwa, hivyo kama una changamoto ya kipato kuwa kidogo kwenye ajira yako, unaweza kuanzisha biashara na ikakusaidia.

Tatu ni SEMINA YA ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, hii ni semina ambayo ipo kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambayo ina masomo 10 muhimu sana kuhusu kujijengea uhuru wa kifedha na utajiri. Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kupata masomo haya.

Kupata huduma yoyote au zote hizi niandikie ujumbe kwa njia ya wasap namba 0717396253 kwa ile huduma unayotaka na nitakupa maelekezo ya namna ya kuipata. Karibu sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA www.kisimachamaarifa.co.tz/kujiandikisha

Kupata huduma za Ukocha; www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

Kujiunga na Kundi la kusoma vitabu; www.amkamtanzania.com/kurasa

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog