Rafiki yangu mpendwa,

Moja ya sababu zilizokuwa zinawazuia wengi kufanikiwa siku za nyuma, ilikuwa ni kukosekana kwa hamasa.

Pale mtu anapoishi kwenye mazingira hasi, akiwa amezungukwa na watu hasi ambao hakuna makubwa waliyofanya na hawaamini yeyote anaweza kufanya makubwa, ni vigumu sana kupiga hatua kubwa.

Lakini sasa ujio wa mtandao wa intaneti pamoja na mitandao ya kijamii, umeondoa kabisa kikwazo cha hamasa kwenye mafanikio. Kwa sababu mazingira ambayo mtu yupo hayawezi tena kuwa kikwazo. Kwa sababu anaweza kujifunza kwa walio mbali na pale alipo, kupitia mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii.

Pia ukuaji huu wa teknolojia umezalisha aina nyingi za biashara, moja wapo ikiwa biashara ya kutoa hamasa. Wengi wameweza kutumia vizuri mtandao kutoa mafunzo ya hamasa.

Iwe ni kupitia hadithi za wale waliofanikiwa au kwa jumbe fupi fupi za matumaini, kwa sasa tunaweza kusema kabisa kwamba hakuna uhaba wa hamasa.

Lakini sasa, pamoja na wingi wa hamasa, bado wengi hawafanikiwi. Watu wengi wanajua hadithi za wengi walioanzia chini na kuweza kufika juu zaidi. Lakini wao hawawezi kutoka pale walipo.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Na wengi wanapoona hawawezi kutoka pale walipo, wanakazana kutafuta hamasa zaidi na zaidi. Hivyo kinachotokea ni kundi kubwa la watu ambao wamekuwa wateja wa hamasa, wamekuwa walevi wa hamasa, na wanataka kila muda wawe wanahamasishwa na hadithi mbalimbali za mafanikio.

Leo nataka kukuambia kitu kimoja rafiki yangu, kama hujafika unakotaka kufika, kama hujaweza kutoka pale ulipo sasa, tatizo siyo hamasa, bali tatizo ni tabia. Hamasa ni muhimu sana, lakini hamasa haina nguvu ya kukutoa hapo ulipo.

Hivyo badala ya kuendelea kukazana na hamasa zaidi, hebu kaa chini na utengeneze tabia za ushindi. Tengeneza tabia ambazo unajifunza kwa wengine ambao wamefanikiwa, na kazana na tabia hizo kila siku mpaka ziwe sehemu ya maisha yako.

Tatizo la hamasa ni kwamba unaona vitu kwa nje, lakini ili kitu kitokee nje, lazima kianzie ndani. Yeyote unayemwona amepiga hatua, alipitia kipindi kirefu cha kujijengea tabia na nidhamu ya hali ya juu. Mafanikio yanayoonekana sasa hayakuwepo siku za nyuma.

Hivyo jua nini unataka kwenye maisha yako, kisha tengeneza tabia ya kukufikisha unakotaka kufika.

Kwa mfano kama unataka kuwa mwandishi, unajua kabisa waandishi wanafanya kitu kimoja, WANAANDIKA. Hivyo kila siku, ije mvua lije jua, ujisikie usijisikie, utapaswa kukaa chini na kuandika. Haijalishi utaandika nini, bali unahitaji kukaa chini na kuandika.

SOMA; Kama Umewahi Kucheza Kamari Au Bahati Nasibu Nina Maneno Makali Kwako, Yasome Na Yatakusaidia.

Kadhalika kwenye kazi na biashara zako nyingine, jua ni vitu gani unapaswa kuvifanya kila siku ili uweze kufika kule unakotaka kufika. Na ukishajua unavyopaswa kufanya, unavifanya bila ya kuangalia kama unajisikia kufanya au hujisikii kufanya.

Mwisho kabisa kuna tabia ambazo kila anayetaka kufanikiwa kwenye maisha lazima awe nazo. Hapa naorodhesha chache katika tabia hizo.

  1. Tabia ya kuamka asubuhi na mapema na kujiandaa kwa siku husika.
  2. Tabia ya kujali na kulinda sana muda, kutokupoteza muda kwa mambo yasiyo muhimu.
  3. Tabia ya kwenda hatua ya ziada kwenye kila ambacho mtu anafanya.
  4. Tabia ya kujifunza kila siku.
  5. Tabia ya kuweka akiba kwenye kila kipato anachoingiza.
  6. Tabia ya kuwekeza kwenye kila kipato.
  7. Tabia ya kujenga mahusiano imara na wale ambao wanahisiana naye.
  8. Tabia ya uaminifu na uadilifu wa hali ya juu sana.
  9. Tabia ya kutokukata tamaa hata kama nini kimetokea.
  10. Tabia ya kukubali majukumu yake.

Rafiki, kazana na kujijengea tabia ambazo zitakufikisha kwenye ushindi. Hamasa ni nzuri, lakini ni kwa muda na haitakutoa pale ulipo sasa. Unahitaji kujenga tabia. Endelea kupata hamasa kila siku, lakini usiishie kwenye hamasa tu, weka kazi kwenye kujenga tabia zitakazokuwezesha kufanikiwa zaidi.

Na kwa kuwa hamasa kwa sasa imeshakuwa kama kilevi, kwa sababu mtu anaweza kujikuta anatumia muda mwingi kutafuta hamasa kuliko kufanya, jiwekee ukomo kwenye muda unaotumia kupata hamasa kwa siku. Tenga muda mfupi wa kupata hamasa na ukiisha huo achana na hamasa na nenda kafanye. Itakuwa haina maana yoyote kwako kama utatumia masaa kusoma na kuangalia vitu vya hamasa kila siku.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji