Rafiki yangu mpendwa,
Karibu kwenye #TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu ya juma zima, ambapo unakwenda kujifunza na kama utachukua hatua basi maisha yako yatakuwa bora zaidi.
Tunamaliza juma namba 36 la mwaka huu 2018, imani yangu ni kwamba kila juma unapiga hatua zaidi kufikia ndoto kubwa za maisha yako.
Karibu kwenye tano za juma, jiandae kujifunza, tafakari yale unayojifunza jinsi unavyoweza kuyatumia kwenye maisha yako, na nenda kaanze juma namba 37 ukiwa na mkakati wa kufanyia kazi haya uliyojifunza ili uweze kuboresha maisha yako.
#1 KITABU NILICHOSOMA; KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO.
Wote tunajua kwamba safari ya maili elfu moja inaanza na hatua moja, hata umbali uwe mkubwa kiasi gani, hatua moja baada ya nyingine inatufikisha popote tunapotaka kufika.
Kadhalika, mafanikio makubwa kwenye maisha, iwe ni mwaka mmoja kutoka sasa, miaka mitano, kumi na hata hamsini ijayo, inaanza na siku moja.
Kama ukiweza kuiishi siku moja kwa mafanikio makubwa, unachohitaji ni kurudia hivyo kila siku na hakuna kitakachoweza kukuzuia usifanikiwe.
Wengi hawafanikiwi kwa sababu hawana udhibiti wa siku zao, wanaianza siku kwa kuchelewa, kwa kuendeshwa na habari na mitandao, kwa kufanya kazi wasizojali, kwa kuahirisha mambo na mwishowe kuimaliza kwa ulevi au kupoteza muda kwenye mitandao na habari.
Watu wengi wanakuja kustuka miaka imepita, wamekuwa kwenye kazi kwa muda mrefu lakini hakuna kikubwa wanachoweza kuonesha wamefanya. Yote hayo ni kwa sababu wameshindwa kufanya kitu kidogo sana, kutawala siku zao.
Mwandishi Craig Ballantyne kwenye kitabu chake cha THE PERFECT DAY FORMULA ametushirikisha kanuni rahisi sana ya kuweza kuidhibiti siku yako na kufanikiwa kwenye maisha yako.
Ni kitabu kifupi na kinachoeleweka sana, ambacho nimekiona ni mwongozo mzuri sana kwa yeyote anayetaka kutawala siku yake na kufanikiwa. Hasa kwa wale ambao hawawezi kuamka asubuhi na mapema, kitabu hichi kina kanuni rahisi mno, ambayo kazi ni kwako tu kuifuata.
Hapa nakwenda kukushirikisha yale muhimu sana kuhusu kanuni ya siku ya mafanikio, ambayo kama utaanza kufanyia kazi leo, basi maisha yako yatakuwa bora kabisa.
CHIMBUKO LA KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO.
Mwandishi anatuambia chimbuko la kanuni yake ya siku ya mafanikio limetoka kwenye falsafa ya ustoa, falsafa ambayo imekuwepo zaidi ya miaka elfu mbili iliyopita.
Mwandishi anamtumia mwanafalsafa Epictetus, mstoa ambaye alianza kama mtumwa na kuweza kufikia ngazi ya juu sana kwenye kufundisha falsafa.
Chimbuko la kanuni hii ya siku ya mafanikio, linalotoka kwenye falsafa ya ustoa ni hili, kwenye maisha yako, kuna vitu ambavyo vipo ndani ya uwezo wako na vitu vingine viko nje ya uwezo wako. Ni kupoteza muda wako na nguvu zako kama unataka kubadili vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako. Lakini kama utawekeza muda wako na nguvu zako kubadili yale yaliyopo ndani ya uwezo wako, utaweza kuwa na maisha bora sana.
Hatuwezi kubadili jinsi watu walivyo, hatuwezi kubadili hali ya hewa na wala hatuwezi kubadili yale yanayotokea kwenye maisha ya wengine. Lakini tunaweza kudhibiti na kubadili yale tunayofanya kwenye kila siku yetu. Tunaweza kuchagua tufanye nini na tuache nini. Na nguvu hii ndiyo tunayoweza kuitumia kwenye kuishi siku yetu ya mafanikio.
KANUNI YA SIKU YA MAFANIKIO.
Kanuni ya siku ya mafanikio imejengwa kwenye misingi mikuu mitatu;
Msingi wa kwanza; KUDHIBITI. Hapa unahitaji kudhibiti yale yaliyo ndani ya uwezo wako na kupokea yale ambayo huwezi kuyadhibiti. Ili kuwa na siku ya mafanikio, unahitaji kuwa na udhibiti mkubwa kwenye ASUBUHI YAKO.
Msingi wa pili ni KUSHINDA. Unahitaji kushinda kelele na usumbufu wa kila siku ili kuweza kufanya yale muhimu. Ili kuwa na siku ya mafanikio, unahitaji kushinda kelele na usumbufu kwenye MCHANA WAKO.
Msingi wa tatu ni UMAKINI. Hapa unahitaji kuweka umakini kwenye yale ya muhimu zaidi kwako na kupuuza mengine ambayo siyo muhimu. Ili kuwa na siku ya mafanikio, unahitaji kuweka umakini kwenye yale yaliyo muhimu sana kwenye JIONI YAKO.
Ona jinsi ilivyo rahisi;
DHIBITI ASUBUHI YAKO
SHINDA MCHANA WAKO.
WEKA UMAKINI KWENYE JIONI YAKO.
Hiyo ndiyo kanuni ya siku ya mafanikio, ukiweza kuiishi hii, utakuwa na siku bora kila siku na mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Sasa nitakushirikisha kila cha kufanya kwenye asubuhi yako, mchana wako na jioni yako ili uwe na siku ya mafanikio.
DHIBITI ASUBUHI YAKO;
- Amka asubuhi na mapema, angalau masaa matatu kabla ya muda wako wa kuanza kazi au biashara yako.
- Kuwa na sheria za maisha yako na siku yako. Hapa unakuwa na orodha ya vitu unavyopaswa kufanya kwenye maisha yako na vitu unavyopaswa kufanya kila siku. Sheria hizi unapaswa kuzifuata bila ya kujali unajisikia au hujisikii.
- Tengeneza orodha ya vitu unavyokwenda kufanya kwenye siku yako, na orodha isiwe ndefu, maana vitu vikiwa vingi inakupa uvivu wa kufanya vyote. Weka vichache na muhimu.
- Tengeneza orodha ya vitu ambavyo hutafanya kwenye siku yako. Kama kuna vitu ambavyo vimekuwa vinachukua muda na nguvu zako lakini havichangii kwenye mafanikio yako, viorodheshe kwenye orodha ya vitu ambavyo hupaswi kufanya. Hii ni orodha muhimu sana itakayokusaidia kuokoa muda na nguvu zako.
- Tengeneza mazingira yatakayokupa hamasa ya kufanya yale muhimu na kukuondoa kwenye tamaa za kufanya yasiyo muhimu. Mfano usiingie kwenye mitandao ya kijamii muda wa kazi.
- Kuwa na mpango bora wa kiafya kila unapoamka asubuhi, fanya tahajudi, Sali, fanya mazoezi na pata kifungua kinywa cha afya.
- Pata muda wa kujifunza kabla hujaianza siku yako, ni muda tulivu kwako kujifunza unapoamka mapema.
- Fika eneo lako la kazi mapema, utakuwa na utulivu wa kufanya kazi zako kwa mipango yako, kuliko ukichelewa na kujikuta unakimbizana na kila kinachojitokeza.
- Ili kuweza kuamka asubuhi na mapema, lala mapema, pata usingizi bora na weka alam yako mbali na kitanda chako.
- Kanuni nzuri ya kuamka asubuhi na mapema ni hii; 10-3-2-1-0. Masaa kumi kabla ya muda wako wa kulala usitumie kahawa, masaa matatu kabla ya muda wa kulala usile wala kutumia kilevi, masaa mawili kabla ya muda wa kulala usifanye kazi, saa moja kabla ya kulala usitumie vitu vinavyotoa mwanga kama simu, kompyuta na tv na alamu yako inapoita asubuhi, usibonyeze kitufe cha kusubirisha, amka muda huo huo. Ukifuata kanuni hii ya 10-3-2-1-0 utaweza kuamka asubuhi na mapema, ukiwa na nguvu na hamasa ya kufanya makubwa.
SHINDA MCHANA WAKO.
Ili kushinda mchana wako, mwandishi ametushirikisha NGUZO KUU TANO za mafanikio, ambazo zimekuwa zinatumiwa na watu wote waliofanikiwa sana.
Jifunze nguzo hizo hapa na zitumie ili uweze kufanikiwa zaidi kwenye siku yako na maisha yako kwa ujumla.
NGUZO YA KWANZA; MIPANGO NA MAANDALIZI.
Lazima ujue nini hasa unataka na utakipataje, hii ndiyo nguzo ya kwanza muhimu sana kwenye mafanikio yako. kama hujui unachotaka, hutajua hata ukikipata. Na kama hutapanga unakipataje, utakuwa unajifurahisha tu. Jua unachotaka, kuwa na mpango wa kukipata na fanyia kazi mpango huo.
NGUZO YA PILI; NGUVU YA USIMAMIZI.
Ili uweze kufuata mpango uliojiwekea, unahitaji kuwa na mtu wa karibu ambaye anakusimamia na kukuongoza. Kwa sababu wewe mwenyewe ni vigumu sana kuweza kuendelea, hasa pale mambo yanapokuwa magumu. Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na KOCHA ambaye anakusimamia na kukuongoza kwenye mpango wako mpaka pale unapopata unachotaka. Hakikisha una kocha anayekusimamia na kukuongoza kwenye safari yako.
NGUZO YA TATU; JAMII INAYOKUUNGA MKONO.
Jamii inayokuzunguka ni muhimu sana, kupata kile unachotaka, unahitaji kuzungukwa na jamii inayokuunga mkono na kukupa hasama ya kupiga hatua zaidi. Kama utazungukwa na watu wanaokukatisha tamaa, itakuwa vigumu sana kwako kufanikiwa. Hakikisha unazungukwa na jamii inayoamini kwenye kile unachofanya na kwenye mafanikio yako.
NGUZO YA NNE; ZAWADI.
Tabia zetu wanadamu zinajengwa na nguvu kuu mbili; ADHABU NA ZAWADI. Unapokosea na ukaadhibiwa unajifunza kutokufanya tena kile ulichokosea. Na unapofanya vizuri ukapewa zawadi, unajifunza kufanya zaidi kitu hicho ili upate zawadi zaidi. Jipe zawadi pale unapopiga hatua kwenye yale uliyopanga kufanyia kazi, na hiyo itakusukuma kuchukua hatua zaidi ili kupata zawadi zaidi. Kama kuna kitu unapenda sana kufanya au kupata, basi kifanye kuwa zawadi kama utakamilisha kitu fulani kwenye siku yako. Kwa njia hii, utafanya zaidi.
NGUZO YA TANO; JIWEKEE UKOMO WA MUDA.
Ni tabia ya binadamu kuahirisha vitu pale ambapo hakuna ukomo, lakini ukomo unapofikia, mtu anafanya kila namna mpaka akamilishe. Angalia siku za mwisho za kufanya vitu uone jinsi wengi wanafanya kwa juhudi zaidi. Ili kuweza kufanya makubwa, jiwekee ukomo wa muda kwenye kila unachofanya. Ipo sheria ya Parkonson ambayo inasema kazi huwa inachukua muda uliopangwa. Hivyo kama kazi itapangwa kufanywa masaa matano, itakamilika ndani ya masaa hayo matano. Na kama kazi hiyo hiyo itapangwa kufanywa kwa masaa 10, itachukua masaa kumi kufanyika. Na kazi hiyo hiyo isipokuwa na ukomo wa muda, haitakamilika kamwe. Tunafanya kazi pale tunapokuwa na ukomo, jiwekee ukomo wa muda kwenye kila unachofanya na utasukumwa kufanya ndani ya ukomo huo.
WEKA UMAKINI KWENYE JIONI YAKO.
Ipo sheria muhimu sana ya mvutano, ambapo kile tunachopata kwenye maisha yetu, tunakuwa tumekivuta kwa fikra zinazotawala akili zetu. Hivyo pale ulipo sasa na kila ulichonacho, ni zao la fikra ambazo umekuwa nazo huko nyuma. Kama unataka kufika tofauti na hapo ulipo sasa, lazima fikra zinazotawala akili yako ziwe za kile unachotaka. Ndiyo maana hatua ya kwanza na ya muhimu ni kujua nini unachotaka.
Ukishajua kile unachotaka, hicho pekee ndiyo kinapaswa kuwa kipaumbele kwako. Utashawishiwa na vitu vingi ambavyo havihusiani na unachotaka, lazima uwe na nidhamu ya kusema hapana na kuweka umakini wako wote kwenye kile unachotaka.
Haijalishi wazazi wako, ndugu zako, wafanyakazi wenzako na hata jamii inasema na kufanya nini, jua hakuna yeyote kati ya hao mwenye maono uliyonayo wewe, anayejua wapi hasa unapotaka kufika na maisha yako. Hivyo pamoja na maoni mengi mzuri ambayo wengi watakuwa nayo juu yako na kile unachofanya, kumbuka wewe ndiye utakayeishi maisha yako, na ndiye mtu wa mwisho kufanya maamuzi ambayo utayaishi.
Rafiki, kitabu hiki cha THE PERFECT DAY FORMULA, ni kizuri sana kwako kujijengea kanuni ya kuiishi siku yako ya mafanikio, na kisha kurudia siku hiyo kila siku. Pata muda usome kitabu hichi, kwa sasa anza kufanyia kazi haya uliyojifunza mara moja na utaweza kupiga hatua.
Kupitia kitabu hiki, nimeona nguvu kubwa sana ya KISIMA CHA MAARIFA, japo sikuwahi kufikiria KISIMA CHA MAARIFA kinasimamia NGUZO TANO ZA MAFANIKIO. Kwa kuwa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, unahitaji kujua wapi unaenda na masia yako, Mimi nakuwa KOCHA WAKO kwa karibu sana na unazungukwa na jamii ya watu ambao wana kiu kubwa ya mafanikio hivyo wanakupa hamasa ya wewe kufanikiwa pia. Kama bado hujawa mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, unajichelewesha kufanikiwa.
#2 MAKALA YA WIKI; TATIZO LAKO SIYO HAMASA.
Rafiki, biashara ya hamasa imekuwa biashara kubwa sana duniani. Hamasa inayouzwa kwa njia ya maandishi, sauti na hata video, imekuwa kimbilio la wengi wanaotaka kufanikiwa.
Lakini licha ya kuwepo kwa wahamasishaji wengi, licha ya vitabu vingi kuandikwa kuhusu mafanikio, licha ya kuwepo kwa video nyingi za mafunzo ya mafanikio na hamasa, bado watu wengi hawafanikiwi.
Juma hili nimekuandikia makala ya kukuondoa kwenye mtego huo wa hamasa, nimekuonesha kwa nini tatizo lako siyo hamasa bali tabia. Hivyo kabla hujakimbilia kutafuta hamasa nyingine, hebu soma kwanza makala hii na uanze kujijengea tabia muhimu kwa mafanikio yako; Tatizo Siyo Hamasa, Tatizo Ni Tabia, Jua Jinsi Unavyoweza Kujijengea Tabia Za Ushindi Hapa.
Pia kuna vitu vitatu ambavyo kama utavifanya, basi maisha yako yatakuwa bora sana na dunia itakuwa sehemu bora zaidi ya kuishi, unaweza kusoma vitu hivyo kwenye makala hii; Kama Unataka Kuifanya Dunia Kuwa Sehemu Bora Kabisa Ya Kuishi, Fanya Mambo Haya Matatu.
#3 TUONGEE PESA; AINA TATU ZA VIWANGO VYA FEDHA.
Grant Cardone, mtu ambaye napenda kumsikiliza sana linapokuja swala la fedha, maana huwa hakatishi kona, anausema ukweli kama ulivyo kuhusu fedha, anatuambia kuna aina tatu za viwango vya kifedha.
Aina ya kwanza ni kiwango cha hofu.
Hiki ni kiwango cha fedha ambacho unakuwa nacho, lakini kinakupa hofu zaidi. Hapa mtu unakuwa na akiba yako kidogo, lakini unaogopa kuitumia kwa sababu ikipotea hujui utapataje fedha zaidi. Kiwango hiki cha fedha ni kifungo na utumwa wa kifedha, maana kinakuzuia kupata fedha zaidi.
Aina ya pili ni kiwango cha ukuaji.
Hiki ni kiwango cha fedha ambacho unakuwa tayari kukitumia kwa ukuaji zaidi. Kiwango hiki cha fedha unaweza kuwekeza kwako binafsi na kwenye biashara zako na ukaweza kukuza kipato chako zaidi. Kwenye kiwango cha ukuaji, kipato chako kinaongezeka zaidi na zaidi kadiri unavyowekeza kwako binafsi na kwenye biashara zako pia.
Aina ya tatu ni kiwango cha uwekezaji mkubwa.
Hiki ni kiwango cha fedha ambapo mtu unaweza kufanya uwekezaji mkubwa sana na ukapata faida kubwa kwa baadaye. Kuna fursa nyingi za uwekezaji ambazo zinawanufaisha wale wenye kiwango kikubwa cha fedha wanachoweza kuwekeza. Ukifika kwenye ngazi hii, fedha zako zinazalisha fedha zaidi bila ya wewe kufanya kazi kabisa.
Cardone anatuambia tuwe makini, maana wengi huwa wanakwama kwenye kiwango cha hofu, na hata wale wanaowekeza kwao binafsi au kwenye biashara zao, wakianza kupata fedha zaidi wanarudi kwenye hofu na kulinda fedha zao, badala ya kuzikuza zaidi na kufikia kiwango cha uwekezaji mkubwa.
#4 HUDUMA NINAZOTOA; ZIMEBAKI SIKU 52 TU KUELEKEA TUKIO HILI KUBWA.
Ni tukio kubwa na la kipekee sana kwa wapenda mafanikio wote kwa mwaka huu 2018. Ni SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ambayo itafanyika tarehe 03/11/2018 jijini Dar es salaam.
Ni semina ya kukutana moja kwa moja, ambapo tutajifunza mengi kuhusu maisha ya mafanikio, biashara, fedha na uwekezaji.
Ada ya kushiriki semina ya mwaka huu 2018 ni tsh 100,000/= na mwisho wa kulipa ada ili kushiriki semina hii ni tarehe 31/10/2018. Unaweza kulipa ada hii kidogo kidogo kadiri unavyoweza.
Kama utachagua kulipa kila siku, kuanzia leo itakuwa shilingi elfu mbili. Kama utachagua kulipa kila wiki basi unahitaji kulipia elfu 15 maana zimebaki wiki 7. Na kama unachagua kulipa kila mwisho wa mwezi, mwezi huu wa tisa unahitaji kulipa elfu 50 na mwezi wa kumi ulipe elfu 50.
Kama unachagua kulipa ada yote kwa mara moja, basi unaweza kufanya hivyo mpaka kufikia tarehe 31/10/2018.
Rafiki yangu, sitaki hata mmoja mwenye kiu ya kweli ya mafanikio akose semina hii, ndiyo maana nakupa kila nafasi ya kuweza kufanya malipo.
Pia ili kuhakikisha unapata nafasi ya kushiriki semina hii, nitumie ujumbe kwenye namba 0717396253 wenye majina yako kamili na maelezo kwamba utashiriki semina na mpango wako wa malipo ni upi.
Namba za kufanya malipo ni MPESA 0755 953 887 TIGO PESA/AIRTEL MONEY 0717 396 253. Ukituma fedha tuma ujumbe wenye majina yako na kwamba umelipia SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA.
Rafiki, usipange kukosa semina hii, maana ndiyo nafasi pekee ya mimi na wewe kukaa pamoja kwa ajili ya kutengeneza mikakati muhimu ya mafanikio yako.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; NA KAMA UNA KITU HIKI, UNA MAFANIKIO MAKUBWA.
‘No man is a failure who is enjoying life.’ – William Feather
Kuna madaraja na viwango vingi sana vya mafanikio ambavyo kila jamii imekuwa inajaribu kutengeneza. Lakini kadiri watu wanavyokazana kufikia viwango hivyo, ndivyo wanavyozidi kukosa furaha kwenye maisha yao.
Kama unasikia watu wakisema fedha hainunui furaha, basi jua yeyote aliyepata fedha nyingi na hana furaha, aliacha kukimbiza ndoto yake na akaanza kukimbiza ndoto za wengine. Anafikia ndoto hizo lakini ndani yake bado anakuwa na utupu fulani. Hivyo mtu anakuwa na mafanikio sana, lakini hana furaha.
Kipimo pekee cha mafanikio kwako ni kwa namna unavyoyafurahia maisha yako. Na utayafurahia maisha yako pale tu utakapokuwa unafanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako. Pale utakapojua nini unataka na maisha yako, na kuweka mkakati wa kufikia kile unachotaka.
Na kama anavyotuambia William Feather, hakuna mtu aliyeshindwa kama anayafurahia maisha yake. Ishi maisha yako, na utakuwa na mafanikio siku zote za maisha yako.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu