Warren Buffett, mwekezaji mwenye mafanikio makubwa na mmoja wa watu matajiri sana duniani, anasema ana sheria kuu mbili za uwekezaji. Sheria ya kwanza ni usipoteze fedha na sheria ya pili ni usisahau sheria ya kwanza.
Tunaweza pia kutumia sheria hii kwenye biashara zetu na ikatusaidia sana. Jiwekee sheria ya kutokupoteza fedha kwenye biashara yako, na usisahau kuhusu sheria hiyo kwenye mipango yako yote utakayojiwekea kibiashara.
Kwenye mipango unayojiwekea kwenye biashara, mara zote angalia ni namna gani unapunguza hatari ya kupoteza fedha. Usikimbilie kufanya kila kitu kwa sababu unaona kuna faida kubwa utapata. Unahitaji kujua hatari iliyopo kwenye kila unachofanya na jinsi gani unapunguza hatari hizo.
Lakini hili halipaswi kukufanya uogope kuchukua hatua kabisa kwa sababu unaogopa kuoteza, badala yake unahitaji kuchukua hatua ukijua ya kwamba kama kuna hatari, unaipunguzaje. Unahitaji kuwa na mbadala wa kila hatari inayoweza kujitokeza.
Kazi yako kubwa kama mfanyabiashara ni kutengeneza mfumo bora kwenye biashara yako, ambao utaiwezesha biashara yako kukua na kupunguza hatari mbalimbali za kibiashara.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,