Wengi hufikiria mafanikio makubwa ni kuchagua eneo moja na kuwa vizuri kabisa, bila ya kujali maeneo mengine wapo vizuri kiasi gani. Na hili limetengeneza watu wengi ambao wapo vizuri sana eneo moja na maeneo mengine wapo vibaya sana.
Kama umewahi kusikia ile watu wanasema mafanikio siyo kila kitu, jua hapo umekutana na watu ambao walipuuza maeneo mengine na kukazana na eneo moja walilochagua.
Kama utakuwa na biashara yenye mafanikio makubwa sana, lakini kiroho ukawa upo chini kabisa, hutaweza kufurahia mafanikio ya biashara hiyo. Kadhalika kama biashara au kazi yako ina mafanikio makubwa, lakini mahusiano yako na wengine siyo mazuri, hutaweza kufurahia mafanikio uliyonayo.
Sisemi kwamba lazima uwe na mafanikio makubwa kwenye kila eneo, ila ninachosema ni unahitaji kuweka vizuri maeneo mengine, usiyasahau na kuyapuuza.
Uwezo mkubwa unaotumia kwenye lile eneo ulilofanikiwa, ukiutumia kwenye maeneo mengine ya maisha yako, lazima utapiga hatua kubwa kwenye maeneo hayo.
Na hayo maeneo mengine yakiwa vizuri, basi mafanikio yako makubwa yatakuwa na maana kwako.
Maeneo yenye umuhimu sana kwenye maisha yako ni afya yako kwa ujumla, kuanzia afya ya mwili, akili na roho. Mahusiano yako ni muhimu pia, usiyasahau wakati unakazana kufanikiwa kwenye yale maeneo uliyochagua. Ukuaji wako binafsi ni muhimu pia, kwa sababu kama utafanikiwa kwenye yale unafanya, lakini ndani yako hakuna ukuaji, utakuwa unajiandaa kushindwa na kuanguka.
Huwezi kuwa bora kwenye eneo moja na kuwa hovyo kwenye eneo jingine kisha ukasema umefanikiwa. Kwanza wewe mwenyewe hutajiamini kwenye ubora ulionao kama maeneo mengine upo hivyo. Kazana kuwa bora kwenye eneo ulilochagua na usisahau yale maeneo mengine ambayo ni muhimu kwa maisha yako pia.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,