Rafiki yangu mpendwa,

Watu wengi wanasema wanataka kuibadili dunia, wanataka kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi. Lakini zoezi la kuibadili dunia siyo rahisi kama wengi wanavyosema.

Na hata wale wanaojinadi kwamba wanataka kuibadili dunia, hakuna hatua yoyote kubwa wanayochukua ambayo inaonesha kweli wanaibadili dunia. Na kitu kingine kigumu zaidi ni kwamba, wale wanaojinadi kutaka kuibadili dunia, maisha yao pekee yanahitaji mabadiliko makubwa sana.

Pamoja na ugumu wa kuibadili dunia, kuna mambo matatu ambayo kila mtu akiyafanya, dunia itakuwa sehemu bora kabisa ya kuishi. Sasa wewe huna haja ya kufikiria kila mtu, bali unahitaji kuanza kuyafanyia kazi wewe, na wengine wakiona namna unavyofanya mambo hayo matatu na wao watashawishika kuyafanya.

NUFAIKA NA MABADILIKO

Kwenye makala hii, nimekushirikisha mambo hayo matatu na jinsi ya kuyafanya ili kuhakikisha kila mmoja wetu anaifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi.

MOJA; ISHI KWA MFANO.

Jambo la kwanza kabisa la kufanya ili kuifanya dunia iwe sehemu bora kabisa ya kuishi ni wewe kuishi kwa mfano. Ishi kile unachohubiri, onesha kwa vitendo kile ambacho unataka wengine wafanye.

Kwa kifupi, unahitaji kuwa mtu wa vitendo na siyo mtu wa maneno pekee, unahitaji kuonesha kwa mfano kile ambacho unajua ni sahihi kwa kila mtu kufanya.

Changamoto ni kwamba kila mtu ni msemaji mzuri, kila mtu ni mlalamikaji mzuri, kila mtu anaweza kulaumu wengine kwa chochote kinachotokea. Lakini maneno hayataibadili dunia, vitendo ndiyo vitakavyobadili dunia.

Kuwa mfano wa kile unachojua ni sahihi kwa watu kufanya, na kifanye hata kama wengine hawafanyi. Kadiri utakavyoishi kwa mfano, ndivyo watu watakavyoona matunda mazuri unayopata na wao wenyewe watashawishika kufanya yale unayofanya pia.

MBILI; ONGEZA THAMANI.

Jambo la pili ambalo tunahitaji kufanya ili kuifanya dunia kuwa sehemu bora kabisa ya kuishi ni kuongeza thamani kwa chochote tunachofanya au kugusa. Kitu chochote kile ambacho mtu unafanya au kugusa, ongeza thamani zaidi, acha kitu kikiwa kizuri kuliko ulivyokikuta.

Kama umeajiriwa, weka juhudi kubwa kwenye kazi zako na ongeza thamani kwa wale wanaotumia kile unachotengeneza au huduma unayotoa. Kadhalika kama upo kwenye biashara, ongeza thamani zaidi kwa wateja wako.

Hakikisha mtu yeyote anapokutana na wewe au kukutana na kazi yako, habaki kama alivyokuwa awali. Yeye mwenyewe akiri kwamba kile alichokutana nacho kimeyafanya maisha yake kuwa bora zaidi.

Ifanye mikono yako kuwa ya maajabu, kwa kubadili kila inachogusa kuwa dhahabu, kwa kufanya vitu kuwa bora zaidi kuliko vilivyokuwa awali.

Tatizo kubwa la watu ni uvivu na tamaa, na hii imewafanya wengi kuwa waharibifu wa dunia, kitu ambacho kinamwathiri kila mtu. Ukiondokana na uvivu na tamaa, na ukawa tayari kujituma na kuongeza thamani, dunia itakulipa kulingana na thamani unayotoa.

SOMA; Jinsi Ya Kuongeza Thamani Kwenye Kile Unachofanya Ili Uweze Kulipwa Zaidi.

TATU; SAMBAZA UPENDO.

Jambo la tatu kwetu kufanya ili dunia iwe sehemu bora kabisa ya kuishi ni kusambaza upendo. Upendo ni kitu ambacho kama kila mmoja wetu akikitoa kwa wengine, basi dunia itakuwa sehemu bora mno.

Matatizo yote tunayoyaona kwenye jamii, nchi na hata dunia kwa ujumla, ni zao la kukosekana kwa upendo. Na upendo unapokosekana watu wanakuwa na hofu na kufanya maamuzi ambayo siyo mazuri kwao wala kwa wengine.

Unapokuwa na upendo unakuwa na imani juu ya wengine na imani hiyo inajinega baina ya watu na hilo linaifanya dunia iwe sehemu bora kabisa ya kuishi.

Sambaza upendo, anza kujipenda wewe mwenyewe, kwa jinsi ulivyo, usijiambie kwamba ungekuwa kwa namna fulani ndiyo ungejipenda. Jipende sasa. Kisha wapende wale wote wanaokuzunguka, jua ni watu ambao wanakazana kupata kile wanachotaka, wengine hawana maarifa sahihi ndiyo maana wanakosea. Pia yapende mazingira na penda sana kile unachofanya, ukipenda unachofanya, utakifanya kwa moyo, utaongeza thamani sana na utaishi kwa mfano.

Mambo haya matatu yanashabihiana, ni mambo ambayo unahitaji kuyafanya yote kwa pamoja kama unataka maisha yako yawe bora. Huwezi kufanya moja ukaacha jingine. Huwezi kuwa na upendo halafu ukaacha kuongeza thamani, upendo wako utakuwa wa maneno na siyo wa vitendo.

Kila mmoja wetu anaweza kufanya mambo haya matatu, kwa sababu hayachagui umri, rangi, dini wala kabila. Na muhimu zaidi, yafanye mambo haya kuwa msingi wako wa maisha ya kila siku, ishi kwa mfano, ongeza thamani na sambaza upendo. Wewe anza hata kama wengine wanaonekana kuishi kinyume na msingi huo. Kadiri unavyokwenda, kadiri unavyofanikiwa, watu watataka kuwa kama wewe na wataanza kufanya kama unavyofanya.

Wanasema kila mtu anapenda dunia ibadilike, lakini hakuna anayependa kubadilika. Anza kubadilika wewe na dunia itabadilika.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji